VYAMA VYA SIASA VYAALIKWA KUTOA MAONI MUSWADA WA SHERIA YA VYAMA.

Na,Mwandishi wetu.

Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria inatarajia kukutana na wawakilishi wa vyama vya siasa Januari 19 na 20, 2019 kuwasikiliza na kupokea maoni yao kuhusu muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2018.

Kamati hiyo itapokea maoni yao baada ya kumaliza vikao vyake na wadau wengine vitakavyofanyika Januari 17 na 18, 2019 mjini Dodoma kuhusu muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2018 na kufuatiwa na mkutano wake na wawakilishi wa kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu hapa nchini ambao wanapinga muswada huo.

Bunge litapokea maoni hayo wakati leo kesi iliyofunguliwa kupinga Bunge kujadili muswada huo ikiwa imetolewa uamuzi mahakamani.

Kesi hiyo ilifunguliwa Mahakama Kuu na wanasiasa watatu ambao ni kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, Joram Bashange na Salim Bimani kutoka Chama cha Wananchi (CUF) kwa niaba ya wanachama wa vyama 10 vya siasa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) .

Katika maamuzi ya leo, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeifuta kesi hiyo iliyofunguliwa na Kiongozi wa ACT Wazalendo na wenzake wa vyama vya upinzani waliyokuwa wakiitaka mahakama hiyo kuzuia kusomwa kwa Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa wakidai kuwa uko kinyume na katiba ya nchi.

Mahakama imetoa uamuzi huo leo Jumatatu, Januari 14, 2018 ambapo walalamikaji, Zitto na wenzake wamekubali maamuzi hayo na kusema sasa nguvu yao ni kwenda kuupinga muswada huo kwenye kamati za bunge.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.