MSHINDANO ya riadha mkoani Iringa maarufu kama Ruaha Marathon yanayotaraji kufanyika Julai 21 mwaka huu yamelenga kusaidia kuchangia pesa kiasi cha shilingi milioni 700 kwa ajili ya upanuzi wa kituo cha afya Ngome katika Manispaa ya Iringa.
Mratibu wa mashindano hayo Frank Mwaisumbe ameyasema hayo wakati akizungumza na wanahabari kuhusiana na maandalizi ya mashindano hayo ,kuwa wamekusudia kukusanya pesa kwa ajili ya Ruaha Marathon na sehemu ya makusanyo ya pesa hizo yatatumika kuchangia upanuzi wa kituo cha afya cha ngome kilichopo kata ya Kihesa mjini Iringa .
“Kama mnavyofahamu kuwa mbio hizi za Ruaha Marathon Tanzania zimeanza kufanyika toka mwaka 2011 kabla ya kusimama mwaka 2014 kutokana na changamoto mbali mbali ila sasa zimeanza tena kwa sura tofauti na hizi ni mbio kubwa sana Tanzania kwani mbio hizi zimekuwa zikifanya mambo makubwa manne ambayo yote yamelenga kuiunga mkono serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Magufuli”
Kuwa mbio hizo za Ruaha Marathon zimekuwa zikihamasisha utunzani wa mazingira kwa kutunza mto Ruaha ambao ni mto mkubwa na tegemeo kwa Taifa kwa mahitaji ya umeme ,kutangaza utalii katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha ,kuibua vipaji vya vijana kwani toka 2011 mashindano hayo yamekuwa yakiibua vipaji vya wanariadha nchini na kujiunga na mbio za kulipwa pia ni sehemu ya kutambua na ukuzaji wa vipaji kwa vijana na kuwatengenezea ajira “
Alisema kuwa mashindano hayo yameweza kurejea kwa kasi kutokana na jitihada za uongozi wa serikali ya wilaya na mkoa wa Iringa pamoja na chama ha mapinduzi (CCM) na kuwa wanataraji katika mashindano hayo ambayo yamedhaminiwa na makampuni mbali mbali kama Asas, Ivory , Kwetu NET ,Tawaqal Hoteli na wengine kuwa na sura yenye kuvutia wengi zaidi .
Mratibu huyo alisema kuwa mashindano hayo yatakuwa na mbio za aina mbali mbali kama kilomita 5 kwa ajili ya wakimbiaji na watembeaji mbio zitakazo husu familia na wengine ,nusu marathon kilomita 21 zitahusu wale ambao ni wanariadha ambao watapewa zawadi pia kilomita 42 kwa kuanzia manispaa ya Iringa hadi Igingilanyi na kuwa wote watakao maliaza kukimbia watapewa cheti cha heshima ya udau wa maendeleo mkoa .
Mwaisumbe alisema katika makusanyo ya fedha hizo asilimia 30 zitaelekezwa katika upanuzi wa kituo cha afya Ngome kata ya Kihesa kwa ajili ya kuufanya mji wa Iringa kuepukana na msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa .
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Iringa ambae ni mmoja kati ya viongozi weyeji na washiriki wa mashindano hayo aliwataka wananchi wote kujitokeza kushiriki mbio hizo .
Kwani alisema kituo hicho cha afya ngome kinahitaji zaidi ya milioni 700 kwa ajili ya kupanua kwa kujenga jengo la ghorofa na kuwa wote wanaoshiriki watambue kuwa wanachangia upanuzi wa kituo hicho cha afya ,pia ni sehemu ya kujua afya za wananchi wote na kuwa watatumia mbio hizo kupima afya .
Afisa habari wa mshindano hayo Denis Nyali alisema kuwa hadi sasa zaidi ya watu 100 wamejiandikisha na kati yao wapo kutoka mataifa mbali mbali na watanzania na kuwa zoezi la kujiandikisha na uuzaji wa furana linaendelea.