RAIS SALVA KIIR WA SUDAN KUSINI AONGEZEWA MUDA KUBAKIA MADARAKANI

JUBA. Nchini Sudan Kusini Bunge la nchi hiyo, limepiga kura kurefusha muda wa Rais Salva Kiir kubakia madarakani kwa miaka mitatu zaidi hadi mwaka 2021, hatua ambayo bila shaka huenda ikatatiza juhudi za kuleta amani katika nchi hiyo changa duniani kwa kudhoofisha mazungumzo ya amani na makundi ya upinzani.

Bwana Kiir amekuwa madarakani tangu Sudan Kusini ipate uhuru wake mwaka 2011 na uchaguzi wa mwaka 2015 nao ulihairishwa. Makundi ya upinzani nchini humo hivi karibuni katika siku za nyuma yalishutumu hatua kama hiyo kuwa inakwenda kinyume na sheria.

“Mswada wa mabadiliko ya katiba katika kipindi cha mpito No. 05 kwa mwaka 2018 umepitishwa na bunge la taifa,” alisema spika wa bunge Anthony Lino Makana baada ya wabunge kwa kauli moja kupiga kura kupitisha mswada huo ambao si lazima utiwe saini kuwa sheria na Kiir.

Sheria hiyo itamruhusu Kiir kubakia madarakani hadi mwaka 2021 hata wakati akiwa anajishughulisha na duru ya hivi karibuni kabisa ya majadiliano ya kimkoa ya amani pamoja na makamu wake wa zamani ambaye hivi sasa ni kiongozi wa waasi Riek Machar katika kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka minne sasa.

Uchaguzi ulikuwa ufanyike mwaka huu, lakini mzozo umesababisha muda wa kufanyika uchaguzi huo kushindikana. Waziri wa sheria Paulino Wanawilla , ambaye aliwasilisha mswada huo, alisema utazuwia serikali kutangazwa kuwa si halali, wakati muda wake wa kuwapo madarakani utakapomalizika.

Rais Kiir na Machar waliingia vitani Desemba 2013, na tangu wakati huo mamia kwa maelfu ya watu wameuwawa na mamilioni wengine wamelazimika kukia makaazi yao na kuzusha mzozo mkubwa wa wakimbizi katika kanda hiyo pamoja na kiasi kikubwa cha njaa.

Duru kadhaa za mazungumzo, yaliyosimamiwa na kundi la mataifa yanayofanya biashara ya kanda hiyo linalojulikana kama Intergovernmental Authority on Development(IGAD), ama mamlaka ya ushirikiano wa serikali katika maendeleo, hadi sasa zimeshindwa kuleta amani ama hata makubaliano ya muda mrefu ya kusitisha mapigano.

Mazungumzo ya mwisho yameshuhudia makubaliano mengine ya kusitisha mapigano wakati mapendekezo, ikiwa ni pamoja na kugawana madaraka na Machar kurejea katika wadhifa wake wa makamu wa rais, bado yanajadiliwa.

Hali ya wakazi wa Sudan kusini sio nzuri kwani karibia watu Milioni 07 zaidi ya nusu ya idadi jumla ya wakaazi wa nchi hiyo, wanahitaji msaada wa chakula katika mwaka huu 2018, kwa mujibu wa Umoja wa mataifa.

Wakati huo huo baraza la Usalama la Umoja wa mataifa linatarajiwa kupiga kura wiki hii kuweka vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan kusini, ikiwa ni pendekezo la Marekani ambalo linafuatia makubaliano ya kugawana madaraka baina ya viongozi hao wawili wanaogombana.

Marekani ni mfadhili mkuu wa misaada kwa Sudan kusini, na ilikuwa muungaji mkono mkuu wa uhuru wa nchi hiyo uliopatikana mwaka 2011.

Lakini uvumilivu wa washirika wa kigeni wa Sudan kusini umekwisha baada ya juhudi kadhaa kushindwa kuleta amani nchini humo, ambayo hivi sasa imo katika mwaka wa nne wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyolenga mauaji ya kikabila, ubakaji wa makundi pamoja na madhila mengine yanayotokea.

Related posts

One Thought to “RAIS SALVA KIIR WA SUDAN KUSINI AONGEZEWA MUDA KUBAKIA MADARAKANI”

  1. Rogers

    Huo ni msaada kwa afrika nzima kama maraisi wote wa afrika wangechukuwa hatua kama hiyo pasingekuwa na vita na nizozano ya hapa na pale kama nchi nyingi zilivyo sasa.

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.