RAIS MAGUFULI “WANANGU NENDENI MKASHINDE, NENDENI MKAPEPERUSHE VIZURI BENDERA YA TANZANIA, LENGO LETU IWE NI KUSHINDA TU”

Ikulu Dar es salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wachezaji wa timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars) kuongeza juhudi za kupata ushindi katika michuano mbalimbali inayoshiriki ikiwemo ya kufuzu fainali za michuano ya Afrika (AFCON) itakayofanyika mwakani nchini Cameroon.

Mhe. Rais Magufuli amesema hayo alipokutana na kuzungumza na wachezaji wa Taifa Stars na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Magufuli ambaye amechangia Taifa Stars shilingi Milioni 50 na baadaye kula chakula cha mchana na wachezaji hao, amesema kiu yake na kiu ya Watanzania ni kuona timu yao inapata ushindi na kuitangaza vyema Tanzania kimataifa na kwamba matokeo mabaya ya timu hiyo hukatisha tamaa.

“Wanangu nendeni mkashinde, nendeni mkapeperushe vizuri bendera ya Tanzania, lengo letu iwe ni kushinda tu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya matumizi mabaya ya fedha, rushwa na uongozi mbaya katika vyama vya michezo hali iliyosababisha TFF kunyimwa fedha za ruzuku kutoka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na amewataka viongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, TFF na BMT kushugulikia dosari hizo ili Tanzania iendelee kupata ruzuku hiyo.

“Nawapa shilingi Milioni 50, nataka zikatumike kuimarisha timu na sio kunufaisha viongozi, na hizo fedha tunazonyimwa na FIFA fuatilieni kwa pamoja tuzipate ili zitusaidie kuendeleza timu zetu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Pia amewataka wachezaji kujenga umoja wanapochezea timu ya Taifa na kutanguliza mbele maslahi ya Taifa badala ya maslahi ya timu zao, na amewasihi viongozi kutoingilia majukumu ya mwalimu wa timu ili aweze kuipanga timu yake kitaalamu kadiri atakavyoona inafaa kupata ushindi.

Katika maelezo yake Rais wa TFF Bw. Wallace Karia amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukutana na wachezaji wa Taifa Stars na amemueleza kuwa TFF imejipanga kushirikiana na wadau kuhakikisha timu hiyo inafuzu kucheza AFCON mwakani nchini Cameroon, na pia ameeleza kuwa juhudi kama hizo zinafanywa kwa timu nyingine za Taifa zinazojiandaa kwa michuano ya kimataifa ambazo ni Serengeti Boys, Ngorongoro Heroes, Kilimanjaro Heroes na Twiga Stars.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars Bw. Emanuel Amuneke amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kupata heshima ya yeye na wachezaji wake kukutana nae na amemhakikishia kuwa Taifa Stars ina wachezaji wazuri na wenye uwezo wa kushinda, na kwamba ana imani kuwa kwa michuano iliyobaki itafanikiwa kupata tiketi ya kushiriki AFCON mwakani.

Mmoja wa Makepteni Wasaidizi wa Timu ya Taifa Bw. Erasto Nyoni amemkabidhi Mhe. Rais Magufuli zawadi ya jezi ya Timu ya Taifa na amemuahidi kuwa watahakikisha wanapambana katika michezo iliyobaki kufuzu kucheza AFCON mwakani, ikiwa ni miaka 38 tangu Tanzania ilipofuzu kucheza michuano hiyo mwaka 1980.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga na Mwenyekiti wa BMT Bw. Leodgar Tenga.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.