RAIS MAGUFULI, JAFO NA LUKUVI WAPONGEZWA NA THRDC.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umempongeza Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Suleiman Jafo kwa kuwaonya wakuu wa wilaya na mikoa kutojichukulia sheria mkononi kwa kuwakamata na kuwaweka watu ndani.

Akizungumza na waandishi wa habari Mratibu, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Olengurumwa amesema hatua ya waziri Jafo pamoja na Katibu mkuu wa wizara hiyo Mhandisi Musa Iyembo kuonya wakuu wapya wa wilaya na wakurugenzi kutojichukulia sheria mkononi kwa kuwaweka ndani baadhi ya wananchi ni mfano mzuri wa kuigwa na viongozi wengine ili kuleta utawala bora.

Mratibu, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Olengurumwa akizungumza na waandishi wa habari.

“Kitendo cha waziri wa TAMISEMI kukemea jambo hili la baadhi ya viongozi kutumia vyeo vyao kuwaweka ndani wananchi bila sababu za msingi na kufanya wananchi kujenga chuki kwa serikali yao sisi kama mtandao tunampongeza kwani tunaamini tamko lake litakuwa limetoka juu maana wizara yake ipo chini ya Mhe. Rais Magufuli, na tunaamini vitendo hivi havitajirudia tena” – Onesmo Olengurumwa.

Vile vile mtandao huo umempongeza Waziri wa Nyumba Ardhi na Makazi William Lukuvi kwa kuondoa kodi ya ardhi kwa taasisi zinazofanya kazi za kijamii bila kujiingizia faida na kukiri hatua hiyo itasaidia kuzipa motisha asasi za kiraia kusaidia jamii. Hata hivyo walipongeza pia bunge la bajeti la mwaka huu kuondoa kodi ya taulo za kike (Pads).

Aidha THRDC wamefurahishwa na kitendo cha Rais Dkt John Pombe Magufuli kuwaondoa baadhi ya viongozi wasiokuwa waadilifu na kuteua viongozi wapya kwa ajili ya kuhakikisha utawala wa kisheria na misingi ya haki za binadamu unafuatwa na kuleta maendeleo kwa taifa.

Akiongeza, wito wao kwa serikali ni pamoja na kusisitiza sheria ya tawala za mikoa ya mwaka 1997 baadhi ya vifungu vyake vifanyiwe marekebisho kwani vinatumiwa vibaya na baadhi ya viongozi wasio waadilifu.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.