NYUMA YA GARI KULIKONI RUSHWA BADO KIZINGITI CHA USALAMA BARABARANI?.

 

MAKALA:
Na, Jasmine Shamwepu.

Ilikuwa siku tulivu ya Alhamisi majira ya saa nne asubuhi nilipoanza safari yangu kutoka Dodoma kuelekea Bagamoyo kupitia Jiji la Dar es salaam.

Niliitwa kuhudhuria mafunzo ya usalama barabarani, yaliyokuwa yakiendeshwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ubia na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Nikiwa najiandaa kwa safari niliweka mizigo yangu kwenye buti na kuelekea kwenye kiti namba 6 kilichokuwa upande wa kushoto wa dereva kando ya dirisha.

Nilipendelea kukaa karibu na dirisha kama abiria wengine wanavyokimbilia dirishani.

Baada ya kukaa na kufunga mkanda nilipepesa macho yangu na kuona abiria karibu wote wakiwa wameketi bila kufunga mikanda.

Nilitamani kuwaasa abiria na maafisa wa gari lile kuchukuwa tahadhari, Nilijuwa abiria wengine hawana elimu ya usalama barabarabani, Nilijua kila ajali inaweza kuwa na kinga ikiwa tahadhari itachukuliwa mapema.

Lakini niliamua kukaa kimya nisioneka abiria mwenye kiherehere, Bahati nzuri muda mfupi kabla ya kuanza safari aliingia askari wa usalama barabarani maarufu kama trafiki alisimama mlangoni na kuomba abiria watulie, aliwataka abiria wote kufunga mikanda na kisha kuwatakia safari njema.

Nilishukuru kwani alifanya kazi niliyotaka kuingilia huku nikiwa abiria wa kawaida. Niliona ameniepusha na matusi ya baadhi ya abiria ambao kila mara hawakosi la kusema hata kama ujumbe unalenga jambo lenye nia njema.

Basi lilianza safari baada ya kukaa muda mrefu pale standi ya Nanenane Nzughuni katika Jiji la Dodoma na kuzua makelele ya abiria waliotaka kuwahi shughuli nyingine.

Muda wa kuanza safari kadri ilivyoandikwa kwenye tiketi ulikuwa umepita kwa saa nzima lakini dereva na maafisa wake wa gari hili walikuwa nje wakipiga siasa hadi abiria walipochachamaa na kutishia kudai nauli na kuteremka au kuwaita  maafisa wa usalama waje kushuhudia kero yao.

Niliangalia tiketi yangu na kuichunguza kwa makini nikabaini jina nililoandikwa limekosewa herufi badala ya Jasmine limeandika Jasnene tena limeandika jina moja tu Jina la ubini lilikuwa limeachwa swali hili lilinifanya nimuite kondokta na kumkabidhi tiketi yake afanye marekebisho.

Nilimkumbusha faida ya kuandika jina kamili ili “Lolote likitokea niweze kutambuliwa kwa urahisi kwenye orodha ya abiria wako.” Kondokta hakuwa mbishi ingawa alidai hakuna shida.

Niliposisitiza alikubali huku akidai nisimfunze kazi yake, Abiria wengine walidakia “Madai yako ni sahihi, Makondakta wa siku hizi wazembe utakuta wanaajiri wapiga debe kutafuta abiria bila kuzingatia kuandika majina ya abiria vizuri,”alisema abiria mmoja mwanaume aliyekaa jirani akisoma gazeti.

Alipoingia mkaguzi wa tiketi wa kampuni ya basi lile alimaliza ugomvi wetu na kunikabidhi tiketi nzuri nikatoa simu yangu na kufungua ukurasa ulioniongoza kwenye mjadala mkali.

Wakati nikiwa nimezama kwenye arafa zilizokuwa zinaingia kwenye mfumo wa mawasiliano ya kijamii wa Whats App abiria wote walikuwa kimya huku wengi wakichapa usingizi.

Dereva alishituliwa na honi kali ya gari iliyotoa mlio wa tahadhari kwa kuzidisha mwendo kasi, Nilimsikia abiria mmoja akihoji kulikoni? Mwingine alihoji tuko wapi? Niliinua kichwa kutazama nje ya dirisha niliona bango lililoandikwa sasa tunaingia Gairo niliinua kichwa na kuangalia ndani ya gari.

Jambo la kushangaza karibu abiria wote walikuwa wameshavua mikanda huku wakichapa usingizi nilijiuliza kwanini abiria wanavaa mikanda na kuvua?
Baada ya muda maafisa wawili wa usalama wa barabarani walisimamisha basi letu.

Mara hii hakuna aliyeingia ndani ya gari nilichoshuhudia sasa ni dereva na kondakta wake kuteremka na kuzunguka nyuma ya gari.

Walichofanya huko hakuna mara gari likaruhusiwa na kuondoka mtindo ukawa huo huo katika safari nzima huku Kondakta akitoka mara nyingi zaidi kukutana na matrafiki pembezoni au nyuma ya gari.

Kila baada ya kituo mbele kidogo walikaa maaskari wa usalama barabarani wakipumzika kando ya barabara na chini ya kivuli cha mti vichakani, Kondakta atateremka haraka haraka na kuwafuata huku wakimalizana huko huko.

Nilipomuuliza anawafuata kwanini, alijibu, “Usipopeleka mzigo wao wanakuona wewe noma, huna nidhamu,” alijibu akicheka nilitamani kumuuliza zaidi, lakini alinikwepa akajifanya hakusikia swali.

Nilimuuliza kama anajua sheria ya rushwa inayohusisha wote  mtoaji na mpokeaji? Niliona thamani ya maisha ya abiria katika rushwa ndogo, Nilijiuliza alitoa ngapi?

Nilitamani kumfuata huko na kuona kinachofanyika kabla ya kufuatilia suala hilo nilihitaji kujiridhisha kwa kuongea na abiria mwenzangu kujua kama alikuwa na habari kwanini matrafiki hawana aibu ya kupokea rushwa?

Mzee wa makamu, mwenye kipara na mvi zilizoenea kichwa kizima hadi kwenye sharafa na sharubu alikuwa bado amekazia macho kwenye gazeti la udaku huku akisoma habari za michezo.

“Unadhani rushwa ya barabarani itakwisha leo?” nikamjibu “Kwanini isiishe Babu? akanijibu  “Imekuwa sehemu ya maisha yao ,tena wapo wanaodai rushwa kama haki yao.” Nikamuuliza “Kwamba usipompa anaweza kukufungulia kesi mahakamani?”                                             Akanijibu “Mnh! Kama ulikuwepo manaa hata asipokufungulia kesi, kesho utapita wapi?” Nikamwambia “Lakini tukiikataa rushwa nani atadai?”.

Mazungumzo yalikuwa marefu alisema maaskari wametengeneza mtandao wa mawasiliano kwa njia za kisasa ambapo dereva akitoka kituo kimoja hawezi kuvuka kituo cha pili akiwa salama.

“Lazima watakukamata tu kwani gari lina makosa zaidi ya thelathini wanadai ndege mjanja hunaswa kwenye kamba nyembamba.” Alisema mzee yule mwenye masharubu meupe.

Yeye mwenyewe amewahi kuwa dereva wa malori ya mizigo yanayosafiri masafa marefu anakumbuka adha na changamoto za rushwa alizokumbana nazo hadi alipostaafu miaka mitatu iliyopita.

“Lazima ubebe mzigo wa kutosha kwani wamejipanga wengi kukukwamisha usipite,” alisema akafungua ukurasa wa nyuma wa gazeti.

Tulipofika Standi ya Msamvu, Morogoro, baadhi ya abiria waliteremka kutafuta chakula na wengine kuelekea msalani, Mimi nilisimama kujinyoosha kidogo na kushuka kwenye basi.

Nilielekea maliwatoni hali ya afya ya mazingira haikuwa kila kona walitapakaa wadudu Inzi waalikuwa wakishangilia.

Baadhi ya abiria tuliozungumza nao wanahoji maaskari wanatafutanini wanapozunguka nyuma ya gari? Abiria wachache wanatoa ushauri maaskari kuwa na vituo vya ukaguzi vinavyofahamika na waingie ndani kukagua gari na siyo makondakta kuwafuata nyuma ya gari.

“Hiyo inaweza kuchangia rushwa wanapozunguka nyuma ya magari, badala yake waingie ndani kukagua na kuangalia kinachotakiwa.

Vinginevyo ni ishara wazi ya kupeana rushwa na madereva waache tabia ya kushuka kwenye gari kwani hakuna sheria inayowataka wafanye hivyo,”abiria aliyejitambulisha kwa jina moja la Mkirika alisema alipozungumza na mwandishi wa makala haya.

“Kila baada ya hatua kadhaa maafisa wa usalama barabarani wanasimamisha gari na mtindo wa kuzunguka nyuma ya gari unaendelea kama kawaida”.

Baadhi ya abiria wanalalamika mfumo huo unatoa mwanya wa rushwa na unaonyesha vituo gani ambavyo vimekithiri kwa rushwa, na kwamba kinachotakiwa ni hatua dhidi ya maafisa wanaopenda kupokea rushwa. Ikiwa Serikali itaamua kupambana dhidi ya rushwa ya barabarani ni rahisi kwa kuwa inafanyika hadharani kwenye mabasi makubwa ya abiria,daladala, magari madogo ya abiria na malori ya mizigo kwa kuwa huu ndio mfumo wa askari wanaopenda rushwa na kuchafua jeshi la polisi kwa kuendekeza rushwa.

Kutojiamini kwa madereva na makondakta kumekuwa kisababishi cha rushwa mwakati mwingine bila hata kuombwa na maaskari wenyewe wamekuwa wakitoa vitisho kwa dereva na kondakta wasioacha mchango.

Zipo tetesi kuwa hata wakubwa na hasa maafisa usalama barabarani wa mikoa (RTO) na maafisa wengine chini yao wametengeneza mfumo wa kupanga askari kwenye maeneo ya barabara kwa kuzingatia mgao Askari anayekusanya michango mikubwa na kusambaza kwa wakubwa wake ndiye anayepewa upendeleo wa kupangwa kwenye njia zenye msongamano wa magari.

Kimsingi ajali nyingi za barabarani zimekuwa zikitokea muda mfupi baada ya gari kukaguliwa na kuleta mashaka ni aina gani ya ukaguzi umefanyika kama siyo rushwa?

Baadhi ya abiria wanashauri gari linapopata ajali askari aliyekagua mwisho kabla ya ajali ahojiwe katika uchunguzi na abiria wahusishwe kutoa ushahidi kwa kile walichokiona kabla na baada ya ajali.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) jumla ya ajali milioni 125 zinakadiriwa kutokea kila mwaka na Tanzania ina 32.9% kati ya hizo ajali.

Hesabu za haraka haraka zinaonyesha wastani wa ajali milioni 41 kwa mwaka (sawa na wastani wa ajali 112,600 kwa siku) zinatokea duniani, Familia nyingi zinaendelea kulia, kwa sababu ya wimbi la watoto yatima walioachwa kutokana na vifo vya ajali vya wazazi na walezi wao na wengine wengi ni majeruhi huku wengine wakibaki na ulemavu wa kudumu na maradhi sugu.

Tanzania inatajwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), kuwa miongoni mwa vinara wa ajali za barabarani na kwa maana hiyo, kuna kundi kubwa la watu wanaopata matatizo ya afya, chanzo ni kwenye usafiri na usafirishaji.

“Ni jambo la kusikitisha na kuhuzunisha kuona kuwa Tanzania inatajwa katika ripoti ya Shirika la Afya Duniani, kuwa nchi inayoongoza ikiwa na asilimia 32.9 (ya ajali zote) na wengi wanaopoteza maisha ni vijana wetu wenye umri wa miaka 18 hadi 29 na wengi wao wakiwa ni wanaume.” Alitamka Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya kilele cha wiki ya Nenda kwa usalama (Nipashe, Oktoba 26, 2017).

“Muda umefika wa sisi kama taifa kujitathimini kwani asilimia hizi zinaashiria kuwa ajali zinazosababisha vifo ni nyingi kuliko magonjwa, ingawa natambua ubovu wa barabara unachangia asilimia nane na ubovu wa magari na matatizo ya kiufundi, yanachangia asilimia 16.”

Kwa mujibu wa takwimu za Polisi Tanzania Bara kati ya Januari hadi Septemba mwaka jana imerekodi jumla ya ajali za pikipiki 4,272, zikiwemo zilizoua watu 1,613. Vifo hivyo vya pikipiki ni sawa na asilimia 37. 7.  Takwimu ya Wizara ya Mambo ya Ndani iliyotolewa Bungeni Novemba 7, mwaka huu imeonyesha vifo zaidi ya 8000 kutokana na pikipiki tangu ziliporuhusiwa kisheria kufanya huduma za kusafirisha abiria takriban miaka 10 iliyopita.

Lakini katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka jana ajali hizo zimesababisha majeruhi 1,597 (sawa na asilimia 37.3) ikiwa na maana ya wastani wa 29 % tu ndio wanaotoka salama au kuponea chupuchupu katika ajali hizo.

Ili kukabili changamoto za wimbi la ajali za barabarani, mambo ya msingi yanayotakiwa kufumuliwa katika Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ni pamoja na visababishi vikubwa vya ajali kama vile; Mwendo kasi, ulevi wa madereva, waendesha pikipiki kutovaa kofia ngumu, kutofunga mikanda ya usalama na ukosefu wa vifaa vya kuwalinda watoto ndani ya gari.

Kwa mujibu wa taaifa ya utafiti wa Jeshi la Polisi na Baraza la Usalama Barabarani, ajali nyingi zinasababishwa na magari kupishana zikiwa katika mwendo mkali na mwelekeo mmoja(overtaking) katika sehemu isiyoruhusiwa, kutofunga mikanda, kutovaa kofia ngumu, ulevi wa madereva na uendeshaji vyombo vichakavu.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.