MILIONI 433.46 KULIPA WAKANDARASI WA MIRADI YA MAJI NGARA

Na Mwandishi wetu, Ngara.

Naibu waziri wa maji,Juma Aweso ameahidi wizara yake kuwalipa wakandarasi wa miradi ya maji inayofadhiliwa na benki ya dunia katika wilaya ya Ngara mkoani Kagera kiasi cha Sh433.46 milioni baada ya kucheleweshewa fedha hizo kutoka serikalini tangu mwaka 2014.

Naibu waziri huyo pia amepongeza uongozi wa wilaya hiyo kwa kusimamia miradi ya maji katika vijiji inayofadhiliwa na benki ya dunia na kwamba halmashauri hiyo imedhibiti matumizi mabaya ya fedha za serikali zinazoelekezwa kwa wananchi kupata maji safi na salama.

Aweso ametoa pongezi hizo Januari 13, 2019 katika ziara ya siku moja wilayani Ngara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa kaimu mhandisi wa maji wa halmashauri ya wilaya ya Ngara Simon Ndyamukama aliyesema wananchi wanapata maji kwa asilimia 63.

Pia ameagiza wahandisi na wakandarasi ambao miradi yao imeonekana kuwa na changamoto za utekelezaji pamoja na wahandisi wa halmashauri za wilaya ya Muleba na Misenyi kufika ofisini kwake mkoani Dodoma kujieleza kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria

Alisema wahandishi wa halamshauri hizo za Misenyi na Muleba wamelalalamimikiwa kwa kulipa fedha za miradi ya maji lakini haijakamilika na miradi mingine inavuja aidha matanki au mabomba na kwamba mhandisi wa Ngara ameonekana kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu.

“Atakayeshirikiana na wakandarasi kutafuna fedha za serikali za miradi ya maji kila halmashauari nchini atazitapika na sisi watendaji wa wizara tutamchukulia hatua za kisheria na wala hatutamuhamisha ahtawajibishwa kwenye kituo chake cha kazi”alisema Aweso.

Alisema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji 10 wilayani Ngara na kushauri baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo kumthibitisha kaimu mhandisi wa maji Simon Ndyamukama kushikilia ofisi na kutimiza majukumu yake ipasavyo.

Katika taarifa aliyosomewa kuhusu upatikanaji wa maji wilayani humo,amelazimika kutembelea mradi wa maji Muhweza utakaogharimu Sh559.4 milioni ambao umetekelezwa kwa asilimia 80 licha ya kuwepo changamoto ya ucheleweshaji wa fedha toka serikali tangu 2014.

Amesema mradi huo umesimamiwa ipasavyo na halmashauri haina budi kumpandisha cheo kaimu mhandisi wa maji Simon Ndyamukama kwa kutekeleza vizuri majukumu yake na mipango ya serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Awali Kaimu mhandisi wa maji wa wilaya ya Ngara Simon Ndyamuakama alisema halmashauri ya wilaya ya Ngara ni miongoni mwa halmashauri zinazotekeleza ujenzi wa miradi ya Vijiji 10, katika Mwaka wa Fedha 2017/2018 Halmashauri ilipokea fedha kutoka serikalini Sh314.3 milioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Vijiji hivyo.

Alisema Sh235.26 milioni ilikuwa ya kupeleka umeme kwenye miradi ya maji Kanazi/Kabalenzi, Muhweza/Murugarama na Mbuba na Sh60. 89 milioni zilitumika kulipa deni la mkandarasi huku Sh18.15 milioni zililipa deni la Mhandisi Mshauri wa maji wilayani humo .

“Fedha zilizotoka wizara ya maji baadhi zimeelekezwa kupeleka umeme katika eneo la mitambo ya kusukuma maji ili kubadili teknolojia kutoka kwenye mitambo inayotumia dizeli kwenda kwenye mitambo inayotumia umeme ili kurahisisha uendeshaji” alisema Ndyamukama.

Alisema wakazi wa wilaya ya Ngara wanapata maji ya bomba bubujiko, maji ya kusukumwa na mitambo, vyanzo vya maji ya asili vilivyoboreshwa, Visima vya pampu za mikono, maaji ya mvua pamoja na maji ya bomba ya yanayosukumwa na niashaiy ya umeme wa Tanesco au jua.

Awali wakazi wa kijiji cha Muhweza wilaya ya Ngara waliiomba serikali kukamilisha mradi wa maji uliojengwa kijijini humo utakaonufaisha pia kijiji cha Murugalama ambao umeanza kujengwa mwaka 2014 hadi sasa haujakamilika wenye thamani ya Sh559 milioni.

Mkandarasi wa mradi wa maji wa Muhweza Joseph Muherangata amesema, changamoto ya mradi huo ni kukosekana fedha za kuuendesha na kwamba ameishalipwa Sh245.34 milioni na fedha zilizobaki ni Sh313.8 milioni licha ya mradi kufikia asilimia 80 ili kukamilika.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.