MAMA ALIYEMFANYIA MTOTO UKATILI AFIKISHWA MAHAKAMANI.

Na,Naomi Milton
Serengeti.

Mwanamke mmoja aitwaye Penina Petro(20) mkazi wa Kijiji cha Nyamakendo wilayani hapa amefikishwa mbele ya mahakama ya wilaya ya Serengeti kwa kosa la kumfanyia ukatili mtoto mwenye umri wa miaka 6(jina limehifadhiwa).

Mwendesha mashtaka wa Jamhuri Faru Mayengela mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya Ismael Ngaile alisema katika shauri la Jinai namba 5/2019 mshitakiwa anakabiliwa na kosa moja la utesaji wa mtoto kinyume na kifungu namba 169 A cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Mshitakiwa alitenda kosa hilo Januari 12 mwaka huu katika kijiji cha Nyamakendo baada ya kumtesa mtoto huyo mwenye umri wa miaka 6 kwa kumchapa na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake hali ilompelekea mtoto huyo kuwa na majeraha makubwa na maumivu makali .

Baada ya kusomewa shtaka hakimu Ngaile alimtaka mshitakiwa kujibu kama ni kweli alitenda kosa hilo au lah! Hata hivyo mshitakiwa alikiri kutenda kosa hilo na kusema kilichosemwa ni kweli.

Baada ya mshitakiwa kukiri kosa mwendesha mashtaka aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na hatua nyingine kwa kuwa mshitakiwa amekubali kosa .

Hakimu Ismael Ngaile ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 29 mwaka huu itakapoletwa tena kuendelea na hatua nyigine na mshitakiwa amepelekwa mahabusu.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.