MAHAKAMA YATUPILIA MBALI KESI YA ZITTO NA WENZAKE KUPINGA MUSWADA

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeifuta kesi iliyofunguliwa na Kiongozi wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe na wenzake wa vyama vya upinzani waliyokuwa wakiitaka mahakama hiyo kuzuia kusomwa kwa Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa wakidai kuwa uko kinyume na katiba ya nchi.

Mahakama imetoa uamuzi huo leo Jumatatu, Januari 14, 2018 ambapo walalamikaji, Zitto na wenzake wamekubali maamuzi hayo na kusema sasa nguvu yao ni kwenda kuupinga muswada huo kwenye kamati za bunge.

Jaji Benhajo Masoud amesema Mahakama imeliondoa shauri hilo baada ya waombaji kuchanganya mashataka mawili kwa pamoja.

“Mahakama imeondoa shauri letu dhidi ya serikali kupinga muswada wa sheria ya vyama vya siasa na kifungu cha 8(3) cha sheria ya Haki na Wajibu ( BRADEA ) kwa sababu ya maombi hayo mawili kuunganishwa. Kufuatia uamuzi huo wa mahakama tumeagiza mawakili leo wafungue kesi mpya ya BRADEA” amesema Zitto na kuongeza kwamba;

“Tunaheshimu maamuzi ya mahakama na tunaamini mahakama imetenda haki. Hivyo tumeamua kurudi mahakamani kwa ombi moja la kupinga kifungu cha 8(3) cha sheria ya Haki na Wajibu. Kifungu hiki kinakiuka katiba kwa kuzuia mashauri ya kupinga miswada ya sheria. Mahakama ni chombo cha haki.

Aidha Zitto Kabwe amesema hawatokata tamaa na wataendelea kuupinga muswada huo.

“Tutaendelea kuupinga muswada wa sheria ya kurekebisha sheria ya vyama vya siasa mbele ya kamati za bunge na ndani ya bunge. Muswada ukipita kuwa sheria kama ulivyo au kuwa mbaya zaidi, tutaupinga mahakamani tena. Hatutakata tamaa katika kudai haki,” amesema Zitto.

Katika hatua nyingine, Kesi ya ‘uchochezi’ inayomkabiili Mbunge wa Kigoma Mjini, Zito Zuberi Kabwe imeahirishwa mpaka Januari 29, itakapoitwa kwa ajili ya kwenda kusikilizwa

Kesi hiyo ya Jinai namba 327 ya Mwaka 2018 inayomkabili Kiongozi huyo, leo tarehe 14 Januari 2019 katika Mahakama ya Kisutu, Jijini Dar es salaam ilifika kwa ajili ya kutajwa na kutolewa maamuzi ambayo yalitolewa na Hakimu Mkazi, Janeth Mtega baaada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili (Mashtaka na utetezi).

Upande wa Mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Adolf Kissima ulidai kwamba kesi hiyo leo ilikwenda kwa ajili ya kutajwa lakini upande wa mashtaka hawakuwa na jalada halisi la kesi hiyo.

Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili wa Zitto, Steven Mwakibolwa uliikumbusha mahakama kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na mahakama hiyo kupitia Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama, Huruma Shaidi na ilishapanga tarehe ya kuanza kusikilizwa, ambayo ni Januari 29, 2019.

Inadaiwa kuwa Oktoba 28,2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo, kiongozi huyo alitumia maneno yenye kuleta kuleta chuki miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la Polisi.

Mbunge huyo alifikishwa Mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza, Novemba 2, 2018, bado anaendelea na dhamana.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.