GAMBOSI KIJIJI KILICHOSIFIKA KWA UCHAWI CHAFANYA MAPINDUZI YA MAENDELEO

 

Na Dinna Maningo,Bariadi.

Ukifika Kijiji cha Gambosi Kata ya Gambosi maarufu (Gamboshi)kilichopo km 50 Magharibi mwa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu utakutana na madhari nzuri yenye kuvutia iliyo sheheni miti ya kijani ya asili.

Pia kuna hewa safi na maeneo mengi yaliyowazi huku maeneo mengine zikionekana  Nyumba za wananchi,mazao ya Pamba Mpunga,Mahindi na Viazi,Njegere,Choroko na Mbaazi.

Kijiji hiki kwa miaka mingi Watanzania walio wengi wamekuwa wakiwa na hofu wakiamini kukithiri kwa imani za ushirikina na uchawi jambo ambalo linaelezwa kuwa kwa sasa hakuna uchawi imebaki tu historia au hadhithi ya miaka 58 iliyopita.

Wananchi wa Wagambosi katika kuonyesha kuwa kijiji hicho si cha wachawi sasa wanafanya juhudi katika maendeleo huku kipaumbele kikubwa kikiwa ni Elimu na kilimo,wanasema kuwa tuhuma za Uchawi kwa sasa si hoja nakwamba kwa asiyeamini anakaribishwa kutembelea Gambosi ili kuona hali halisi ya kijiji hicho.

Elimu.
Kijiji cha Gambosi kina Vitongoji 8 ambavyo ni Gambosi,Mwanshela,Makungulu,Mwalugobi,Isebanda,Mabatini Bugabu na Mwabuki, Wananchi wa Vitongoji hivi wanasema sasa hakuna kulala ni kuchapa kazi huku wakiitaka Serikali kuwaunga mkono wanapochangia maendeleo ikiwemo maswala ya Elimu,Afya na Kilimo.

Lukuba John (30) ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwanshela anasema Kijiji hicho kina shule moja ya msingi iitwayo Gambosi ambayo wanafunzi kutoka vitongoji vyote wanasoma kwenye shule hiyo jambo linalowafanya Wanafunzi wengine utembea mwendo wa zaidi ya  kilomita  2-3.

John anasema Wananchi wa Kitongoji cha Mwanshela wanampango wa kuchangishana fedha  ili kujenga shule ya msingi ’’ Tuna mkutano wakuwakutanisha wananchi ili kupanga kiasi cha fedha tujenge shule yetu ili kuwapunguzia watoto mwendo,umbali unamfanya mtoto achoke kwenda shuleni’’anasema.

Anaongeza’’Wananchi wameamua kujitolea kupitia mikutano ya wananchi  tunachangishana kila Kaya 10,000  tunasomba mchanga kutoka mto Bariadi na mawe tunapasua wenyewe  kokoto, tumeongeza madarasa 3,Nyumba moja ya Mwalimu na vyoo matundu 12 shule ya msingi Gambosi’’anasema John.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Gambosi Simon Kanyerere anasema kuwa kijiji hicho kina wakazi  zaidi ya 5,000,hakuna shule ya Sekondari wanafunzi wanaofaulu darasa la saba kutoka shule ya msingi Gambosi  usoma shule ya Sekondari  Miswaki Kata ya Mwasubuya ambapo wengine utembea mwendo wa kilomita  hadi 5 kutegemea na umbali atokako mwanafunzi.

‘’ Wananchi wametumia nguvu zao na michango  na kujenga  shule ya Sekondari itakayoitwa Gambosi iliyojengwa Kitongoji cha Magungulu Madarasa 2,Nyumba moja ya mwalimu,Jengo la Utawala,vyumba 3 vya maabara na choo matundu 8 Tunaomba Serikali ikamilishe usajili ili mwakani watoto wasome’’anasema.

Mkuu wa shule ya Msingi Gambosi Buya Magege anasema shule hiyo ilianzishwa 1,975 ina wanafunzi 1,304 kati ya hao wavulana ni 614 na wasichana 690 ikiwa na walimu 17 kati ya hao wanaume 11 na wanawake 7 nakwamba wazazi wana ushirikiano na waalimu.

Mwenyekiti  huyo wa Kijiji anasema  kuwa upande wa Afya  Zahanati ya Gambosi kila kitongoj wananchi walisomba mchanga na kufanikiwa kupata tripu 10 wakafyatua matofari na wamejenga vyumba viwili vitakavyokuwa wodi ya Wajawazito.

Kilimo.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bugabu Nyarari Ngika  anasema kuwa Wananchi wa Kijiji cha Gambosi ni wakulima wa mazao ya Pamba,Mpunga,Mahindi,Viazi vitamu,Choroko,Mbaazi na Dengu.

‘’ Zao kubwa ni Pamba,Mpunga,Viazi vitamu na mahindi mtu mmoja analima kati ya heka 1-5  kuna mazao mengine kama choroko,Mbaazi,Mtama na Dengu kilimo ndiyo mkombozi wa wananchi waishio vijijini hivyo ni vyema maafisa kilimo wakawatembelea wakulima ili kuwapa ushauri wa kitaalamu wakati wa msimu wa upandaji na kutupatia mbegu za kitaalamu’’anasema Ngika.

Mifugo.
Mkazi wa kitongoji cha Gambosi Mayunga Kidoyayi anasema kuwa licha ya wanachi kufuga mifugo hakuna mahali pa kuuza maziwa anawakaribisha wawekezaji kuwekeza kujenga kiwanda cha maziwa,Nyama na Ngozi ili kuwawezesha wafugaji kuuza mifugo yao na Maziwa, kwani uishia tu kunywa maziwa.

Miundombinu ya Barabara ,Maji na Maasiliano ni changamoto .

Pamoja na jitihada za wananchi bado wanakabiliwa na tatizo la miundombinu ya barabara , Maji  na kutokuwepo kwa mawasiliano mtandao wa Airtel na hivyo kuziomba mamlaka husika kutatua changamoto hizo.

Minza Saguda mkazi wa Kitongoji cha Mabatini anasema kuwa wanatumia maji ya visima vya asili, wakati wa kiangazi ukauka na hivyo wananchi wa Vitongoji hivyo  kulazimika kufata mto Bariadi na hivyo kujikuta wakichelewa kufanya shughuli zingine za uzalishaji.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Gambosi Saimon Kanyerere anasema kuwa kijiji hicho kwa miaka mingi hakikuwa na barabara zaidi ya njia ila mwaka 2015 Serikali ilitengeneza barabara ya km 7 kutoka Kijiji cha Nyamuswa hadi Senta ya Gambosi ambayo sasa imeharibika huku akishauri ijengwe barabara nyingine ya kutoka Kituo cha Afya Isanga hadi shule ya msingi Bugabu.

Diwani wa Kata ya Gambosi Kaliwa Bahame kata yenye Vijiji 2 cha Gambosi na Nyamuswa  anasema kuwa Halmashauri inaendelea na ujenzi wa kisima kirefu  kikichangiwa na nguvu za wananchi katika uchimbaji ambapo kiasi kisichozidi 20 milion kimetumika na kiko hatua za mwisho kitakachosaidia na maji yatasambazwa senta ya Gambosi.

‘’Tuna mkakati wa kuchimba visima vingine 3 Kijiji cha Gambosi na 2 Kijiji cha Nyamuswa wananchi watachimba mimi nitagharamia pampu,na kitasaidia kunywesha mifugo kwakweli wananchi wanajitahidi katika maendeleo tunaomba Serikali isiwe nyuma ili kutowakatisha wananchi tamaa.

Bahame anaitaka Serikali kuboresha miundombinu ya barabara  na  kusajiri shule ya Sekondari Gambosi ili kupata wasomi na wanasayansi wa kitaalamu wanaotoka Gambosi ambao watakuwa waelimishaji wakubwa ndani ya jamii kwakufanya hivyo itasaidia kuwaondoa wanasayansi wa kienyeji walioichafua Gambosi kwa ushirikina na uchawi.

DC Kiswaga awasifia wananchi Gambosi kwa maendeleo.

Mkuu wa wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga  anasema kuwa Shule ya Sekondari Gambosi inatarajiwa kufunguliwa mwakani 2019,nakwamba ikianzishwa itasaidia vizazi vijavyo kuondokana na imani potofu kwakuwa watakuwa wanaelimu.

Anaongeza kuwa Gambosi ni sawa na maeneo mengine  hivyo wananchi wasihofu kuko salama na Serikali inatoa fursa kwa wanaohitaji kuwekeza  wanakaribishwa,napia wasiogope kwakuwa kuna ulinzi wa kutosha na ni mahali salama na uchawi ulishabaki kuwa historia ya kale.

Tuhuma za Ushirikina ,Uchawi zawatesa Wananchi.

Kitendo cha Watanzania kuendelea na imani kuwa wananchi wa Gambosi ni wachawi kinawaumiza mioyo nakuathiri maswala mbalimbali ya kimaendeleo huku baadhi ya watu vijiji na Mikoa mbalimbali wakionekana kuwatenga  punde wanaposikia mtu huyo anatoka kijiji cha Gambosi.

Ngoma za asili za msimu wa mavuno(Mbina)chanzo cha ushirikina,Uchawi Gambosi.

Inaelezwa kuwa ushirikina na uchawi ulikuwepo kwa miaka ya nyuma kabla ya uhuru na miaka 1970 na chanzo ni ngoma za asili lakini kadri siku zilivyosonga uchawi ulipungua kutokana na vinara wa uchawi na dawa za  ushirikina kufariki na sasa uchawi umebaki kama hadithi tu.

Madulu Mabula Mkazi wa Kijiji cha Gambosi anasema kuwa ni desturi kwa kabila la Wasukuma wakiwamo Jamii ya Wanyantuzu kusherekea kwa kucheza ngoma wakati wa msimu wa mavuno ucheza ngoma kipindi cha  mwezi Apili hadi Juni vikundi vya watu ucheza ngoma zao kusherekea mavuno.

‘’Sasa hivi hakuna uchawi imebaki hadithi tuu uchawi iliopo ni sawa na maeneo mengine zamani ulikuwepo kwa sababu ya mashindano ya ngoma watu walikuwa wanatumia madawa ili kupata ushindi kulikuwa na ngoma kubwa mbili ya Ng’wanamakulyu na Ng’wanamabula,sawa ilivyo Simba na Yanga kila ngoma ilitaka ipate ushindi dhizi ya nyingine.

Anaongeza’’Wakawa wanatumia  dawa za kishirikina (Super Power) walizitumia kuvutia watazamani ushindi ulitokana na ngoma yako kuungwa na watu wengi kadri wanavyocheza vizuri ndivyo watu wanatoa pesa nyingi na kusherekea timu yako jambo lililosababisha kila mtu kutafuta ushindi kwa njia yoyote anayojua yeye.

Nkamba Masunga anasema’’kulikuwa na ngoma mbili kubwa zilizoongozwa na wanawake wawili ambao walikuwa vinara wa dawa za ushirikina  Ng’wanamakulyu  wa Ngulyati na Ng’wanamabula wa Gambosi na wote walikuwa ni waganga wa Kienyeji walishafariki,’’anasema Masunga.

Masunga anazidi kueleza kuwa walikuwa na ngoma zao walishindana na Ng’wanamabula alikuwa mtaalamu zaidi wa dawa na ndiyo chanzo cha Gambosi kusifika kwa ushirikina anasema.

Anaongeza’’Kwenye hizo ngoma ulikuwa unashangaa ngoma zikichezwa ghafla mvua inanyesha upande tu wa ngoma nyingine,siku nyingine ngoma nyingine inafanya madawa yake wakati wa kucheza jua linawaka kali linawachoma wachezaji pinzani hadi wanashindwa kucheza wakati huo linawaka upande mmoja upande mwingine hakuna jua na hivyo timu kumshinda mpinzani wake.

Kija Kitanda anasema ili ngoma zicheze vizuri inambidi mmiliki wa ngoma awapikie chakula cha kutosha, inachinjwa ng’ombe.

“Unashangaa nyama iko jikoni lakini haiivi wakati huohuo ngoma nyingine wao wanakula nyama za hiyo ngoma ambao wao wanaona haiivi kumbe imeiva wenzao wanakula bila wao kujua.

Kitanda anaongeza kuwa ngoma hizo zikasababisha kuwepo kwa ushirikina mkubwa kwa kile anachoeleza kuwa wakati mwingine shuka lilifungwa kwenye miti na kuwasha moto juu ya shuka hilo kisha linakalishwa sufuria likiwa na nyama zinaiva lakini shuka haiteketei.

Kitanda anazidi kueleza’’wakati mwingine wakati wa ngoma ukifika unashangaa wachezaji  wa  upande mwingine wa ngoma hawaonekani kumbe wamefichwa kimazingara ili timu pinzani ndiyo icheze ngoma na kujitwalia ushindi,ngoma ikiisha ndiyo unawaona wachezaji waliofichwa wanafika na muda wa mchezo umekwisha.

Telezia Maghanyali (65) mkazi wa Kijiji cha Ngulyati ambaye ni binti wa Marehemu Ng’wanamakulyu naye anasema alikuwa mchezaji kwenye Ngoma ya mama yake na  wakati wakicheza ngoma kulikuwa kukitokea matukio ya hajabu yakiwemo ya watu kupotea kishirikina kwenye mashindano ya ngoma.

‘’ Ngoma zilikuwa zinachezwa kwa kushindana kwa madawa,Watu walikuwa wanapotea iwe usiku au mchana unajikuta unakimbia hujui unapokwenda unakimbia baadae ndiyo unashtuka na kuuliza watu hapa niko wapi nimepotea ndiyo mtu anakuelekeza kwenu unarudi ni zamani sana ’’anasema.

Hata hivyo Maghanyali anasema kuwa kwa sasa alishaacha kucheza ngoma za asili za mavuno sasa ni muumini wa kanisa la Romani Kathoric aliyebatizwa 1998 anamwimbia Mungu na Kucheza ngoma za mikutano ya CCM na anawataka wachawi na washirikina kuacha na kumrudia mwenyezi Mungu.

Tuhuma za uchawi zilivyoathiri wananchi wa kijiji cha Gambosi.

Kitendo cha Gambosi kuendelea kutuhumiwa kwa uchawi kimewaathiri wananchi na kusababisha kutofanyika maendeleo kwa mika mingi iliyopita,watumishi kuogopa wanapopangiwa kazi huku jamii ikiwaogopa.

Elizabeth Charles ni mwalimu wa shule ya awali kanisa la Romani Parokia ya Ngulyati anasema kuwa baada ya kuwapokea watoto wa Gambosi wazazi waliwaogopa  wakiwazuia watoto wao kuchangamana nao.

‘’Kutokana na imani hizo tuliwachukua watoto baadhi wa kijiji cha Gambosi wakiwa hawajui Kiswahili zaidi yakuongea kisukuma wamefundishwa na huwezi amini wanafanya vizuri darasani kuna wengine wanashika namba kwenye shule wanazosoma wana adabu wamelelewa mazingira ya asili japo mwanzoni na mimi niliwaogopa’’anasema.

Sunge Salanya anasema baadhi ya Waganga wakienyeji ujifanya ni Waganga wanaotoka Gambosi kutokana na sifa yake na kufanya utapeli kujipatia fedha na wengine wakitumia jina hilo kufanya uharifu.

‘’yaani ukienda kijiji nje ya Gambosi au Mikoani ukasema unatoka Gambosi unatengwa mtu anakuogopa,kama unataka kuoa ukasema ni wa Gambosi hupewi mwanamke wala nayeye hapati mme sijui ni kwanini watu wanakua na fikra potofu waje kijijini watashuhudia hakuna hayo yanayosemwa anasema Salanya’’

Anaongeza ‘’ Mara eti ikifika usiku kijiji kinakuwa pori nyumba hazionekani mara usiku kijiji kinakuwa kimejaa maghorofa basi watu wasingeishi hata walimu na Wauguzi wasingekuwepo hapa kijijini’’anasema.

Joseph Mungu (45) mkazi wa Kitongoji cha Mwashela Kijij cha Gambosi anasema’’ mwaka 1990 Nilienda Mbeya nikaulizwa ni wa wapi nikasema Gambosi wao wanaita Gamboshi wakaniambia kumbe Gamboshi kuna watu wenye miguu miwili akanishangaa wakasema au umekuja kwa ungo walidhani nadawa nilipata changamoto mpaka kuja kunizoea ilichukua muda’’anasema.

Hali hiyo inaelezwa kusababisha hata baadhi ya Viongozi wa Serikali kutofika kijijini hapo kuzungumza na wananchi kwenye mikutano ya hadhara wakiwemo viongozi wa kisiasa ambao uonekana kijijini wakati wa kampeni Pekee au kunapotokea dharura kutokana na hofu na fikra potofu  jambo linalosabbaisha wanachi kukosa huduma.

Mungu anasema kwa miaka mingi Kijiji kilitengwa  hata viongozi wa Serikali waliogopa kuwatembelea wananchi walipofika waliishia shuleni na zahanati.

‘’ hata barabara yenyewe tangu kijiji kiumbwe ndiyo imejengwa mwaka juzi tunampongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka kututembelea na kutuchangia na mifuko 50 ya simenti kwa ujenzi’’anasema.

Je bado kuna ushirikina na uchawi Gambosi?.

Wananchi wa Gambosi wanasema kuwa sasa hali ni shwari hakuna uchawi na yanayoelezwa ni hadithi za zamani miaka iliyopita ambazo zinapaswa kupuuzwa kwakuwa hazina ukweli ndani yake .

Agnes Malima (20) aliyehitimu shule ya msingi Gambosi 2012 anasema kuwa amekuwa akisikia kuwa kuna uchawi lakini yeye hajawahi kuwaona hao wachawi au mwanafunzi kudhurika,kupotea wala kupata shida yoyote  bali usikia tuu kuwa zamani kulikuwepo Uchawi.

Mkuu wa shule ya Msingi Gambosi Buya Magege anasema‘’ nimehamia hapa 2005 sijawahi kuona ushirikina shuleni wala mwalimu au mwanafunzi kufanyiwa ushirikina ni uvumi kinachotusumbua ni Wasichana kuozeshwa shule  baada ya kumaliza darasa la saba kisa mahari jamii yaWanyantuzu wasomeshe watoto wa kike’’anasema Magege.

Muuguzi Mkunga katika Zahanati ya Gambosi Deus Kimasa anasema kuwa amekuwa mtumishi wa Zahanati hiyo  na hakuna ushirikina na wananchi wakiugua ufika kupata matibabu tofauti na zamani walikwenda kwa Waganga wakienyeji kupata tiba kutokana na imani za kulogwa .

Benadeta Maduhu (70) anasema kuwa zamani baadhi ya wamiliki wa Ngoma walikuwa ni wachezaji na pia Waganga wa Kienyeji lakini sasa mambo yamebadilika nakwamba anajisikia vibaya kuona kijiji chao kikituhumiwa kwa ushirikina licha yakuwa maeneo mengi nako kuna ushirikina.

‘’Uchawi umeisha zamani nyakati za usiku ulikuwa unaona moto unawake shuleni,unasikia mashine yakusaga unga inaunguruma ukienda mungurumo unapotea’’anasema.

Anaongeza’’Mgeni alikuwa akifika akiondoka tuu anapotea hata wewe Mwandishi uchawi ungekuwa bado upo yaani wakati wa kuondoka ungejikuta unapotea nakujikuta huko vijiji vya mbali’’anasema Maduhu.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ngulyati Reonard Masuka aliyeongoza kwa miaka 20 anasema  kuwa kwa sasa vijiji hivyo vina maendeleo mazuri wananchi niwatafutaji japo zamani vilisifika kwa uchawi.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwashela Kijiji cha Gambosi Lukuba John (30) anasema kwa sasa watu wameelimika na hata yeye uchawi amekuwa akisikia yakisemwa tuu lakini hajashuhudia.

Dini zachangia kupungua kwa ushirikina.

Ezekiel Holela ni Mwalimu wa nidhamu wa shule hiyo anasema kuwepo kwa dini kijijini hapo zimesaidia watu kubadilika  watu umwabudu Mungu katika makina ya Roman,SDA,Anglican,PAGT na mengineyo.

John Ninga ni Padri Makao makuu ya Parokia ya Ngulyati yenye vigango 15 anasema kuwa Viongozi wa dini bado wanapaswa kuendelea kuwaelimisha wananchi na kuwapa mafunzo ya dini na maombi kwani Viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika jamii .

‘’Watu wa Gambosi ni wapole wakarimu,hata mimi nilipofika huku watu walizani nataka Ubunge wengine wakasema nina njama zangu watu waligoma kusali lakini siku zilivyokwenda walianza kuhudhuria kanisani makanisa yalikuwepo lakini watu walikataa kusali kutokana na ushirikina sasa wamebadilika wanamwabudu Mungu”anasema.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.