ALIYEZINI NA DADA YAKE AKANA MAELEZO YA AWALI MWINGINE ASOMEWA SHTAKA LA MAUAJI.

Na,Naomi Milton
Serengeti.

Gabriel Nyantori(25) mkazi wa Kijiji cha Kibeyo wilayani hapa ambaye ni mshtakiwa katika shauri la jinai namba 138/2018 amekana maelezo ya awali mara baada ya kusomewa maelezo yake katika mahakama ya wilaya ya Serengeti.

Mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya Ismael Ngaile mwendesha mashtaka wa Jamhuri Faru Mayengela kabla ya kusoma maelezo ya awali alimkumbusha mshitakiwa makosa yake .

Mwendesha mashtaka alisema katika shauri hilo mshtakiwa anashitakiwa kwa makosa mawili kosa la kwanza ni Kuzini kinyume na kifungu 158(1)(a) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kosa la pili ni kumpa mimba mwanafunzi kinyume na kifungu 60 A(1)(3) sheria ya Elimu sura 353 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kwa mtu aliyeoa au kumpa mimba mwanafunzi.

Mara baada ya kumkumbusha mashtaka Faru alisema mnamo April 4/2018 majira ya saa 11 jioni katika Kijiji cha Kibeyo mshitakiwa alifanya mapenzi na mdogo wake wa kike mwenye umri wa miaka 16(jina limehifadhiwa)ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Kibeyo.

Mara baada ya kufanya mapenzi na mdogo wake kwa tarehe hiyo hiyo aliweza kumpa mimba mwanafunzi huyo,mwendesha mashtaka aliendelea kusema kuwa Juni 5/2018 mshtakiwa alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi Mugumu na Juni 6/2018 alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka ambapo alikana.

Hata hivyo baada ya kusomewa maelezo hayo ya awali mshitakiwa alikana,Hakimu Ngaile ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 29 mwaka huu itakapoanza kusikilizwa .

Wakati huo huo mshtakiwa Abel Julius(29) mkazi wa Kijiji cha Nyankomogo wilayani hapa amepandishwa mahakamani hapo na kusomewa shitaka moja la mauaji.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Ngaile mwendesha mashtaka wa Jamhuri Faru Mayengela alisema katika shauri la Mauaji namba 1/2019 mshitakiwa anashitakiwa kwa kosa moja la kuua kinyume na kifungu 196 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Faru alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo Novemba 28/2018 katika Kijiji cha Rigicha baada ya kumuua mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Nzugu Rushinge hata hivyo baada ya kumsomea shtaka hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Hakimu Ngaile ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 29 mwaka huu itakapotajwa tena na mshitakiwa amepelekwa mahabusu.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.