ZITTO: KWANINI SERIKALI INAOGOPA WACHUNGUZI WA KIMATAIFA? USHAURI WA LEMA NI MZURI.

 

Jana Jumanne, siku ya 6 tangu Mohammed Dewji, mfanyabiashara na mlezi wa Klabu ya Simba atekwe nyara, Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani Bwana Godbless Lema alitoa pendekezo kuwa Serikali ya Tanzania iombe msaada wa nje kuongeza juhudi za kumtafuta na kumwokoa Mohammed, Jana hiyo hiyo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Masauni alijibu kuwa Serikali haitafanya hivyo kwa sababu jeshi la polisi nchini lina uwezo na utaalamu wa kutosha kuendelea na uchunguzi.

Naibu Waziri hayupo sahihi kukataa pendekezo la Waziri Kivuli nashauri kuwa pendekezo la Waziri Kivuli lichukuliwe kwa uzito unaostahili chunguzi wa kutekwa kwa Mohammed Dewji unapaswa kuwa wa nguvu kubwa ili kuondoa taswira iliyoanza kujengeka nchini kuwa watu wanaweza kutekwa na hakuna kinachofanyika, Uchunguzi huru wa kimataifa utasaidia sana kurejesha imani ya raia na kuwaondolea hofu kuwa wakati wowote wanaweza kutekwa au hata kushambuliwa.

Kupotea kwa afisa utafiti na sera wa CHADEMA Ben Saanane, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kibondo Simon Kanguye, Mwandishi wa Habari wa gazeti la Mwananchi Azory Gwanda na kushambuliwa kwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu yanadhihirisha kwa kiasi kikubwa sana vikwazo kadha wa kadha ambavyo polisi wetu wanakumbana navyo katika Uchunguzi wa masuala kama haya ya jinai.

Vikwazo hivi ambavyo vingine ni vya kitaasisi, vinaonekana pia kwenye suala la utekwaji nyara wa Mohammed Dewji,
Nilifuatilia kwa kina sana suala la Ben Saanane na Simon Kanguye, Pia nilipata taarifa za awali za kupotea kwa Azory Gwanda kabla ya taarifa hizo kujulikana kwa Umma niligundua kuwa Jeshi letu la Polisi lina watu wenye nia ya dhati ya kukomesha matukio haya lakini wanafika mahala wanakwama, Jeshi la Polisi lilifuatilia suala la Ben Saanane kwa kina Lakini walikwama mahala ambapo waligundua kuwa taasisi nyingine ya Serikali ina mkono, Polisi waliishia hapo na hawakuendelea tena na suala la Ben Saanane.

Vile vile suala la Simon Kanguye, Polisi kuanzia Kibondo mkoani Kigoma mpaka makao makuu ilifika mahala walifungwa mikono na kutoendelea na suala hilo, Nilifuatilia pia suala la Tundu Lissu kwa kina kwa kutumia mahusiano yangu na vijana wapelelezi wazuri ndani ya jeshi la Polisi na kugundua kuwa Polisi walikatazwa hata kufungua file la Uchunguzi.

Mazingira haya yanaonyesha kuwa wakati mwengine huwa tunashambulia sana Jeshi la Polisi na wao hawawezi kujitetea lakini wanakuwa wameshikwa mikono, Hata hivyo kwa kuwa wao ndio wenye mamlaka ya usalama wetu hawana namna lazima wapokee lawama zote, Njia pekee ya wao kuondokana na lawama hizi ni Serikali kuruhusu uchunguzi wa Kimataifa kwenye suala la kutekwa kwa Mohammed Dewji.

Nimeshangazwa sana kuwa Waziri na Polisi amekuwa mbele kukataa pendekezo hili, Kuna maswali hayana majibu katika uchunguzi wa suala la Mohammed Dewji, Baadhi ya vyombo vya habari wameanza kuyachambua mambo ambayo baadhi yetu waliyahoji mapema sana Kwa mfano rafiki yangu mmoja aliamua kuhesabu CCTV camera kuanzia mataa ya Kanisa la Mtakatifu Petro mpaka panapoitwa kilimanyege na kukuta camera 30 zikiwemo camera zenye nguvu sana kutoka makao makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa yaliyopo mtaa huo wa Haile Selasie, Haiwezekani kuwa mpaka leo ‘footages’ za camera hizi hazijachunguzwa na kupata namba za gari zilizotumika kufanya utekaji huu na kisha kutambua umiliki wa gari hizi na kupata njia ya kumfikia Mohammed Dewji alipo, Jeshi la Polisi linasema camera za hoteli ya collosium zilichezewa, Watekaji hawawezi kuchezea camera za mtaa mzima,
Polisi wakipata msaada wa wenzao kutoka nje wanaweza kupata jawabu ya hili.

Jambo lingine ni kuwa kuna kauli tata Kuhusu utekwaji wa Mohammed Dewji, Mwanzoni kabisa Polisi walisema kuwa alitii kukamatwa hakufanya harakati zozote, Hata hivyo ukweli umeanza kutoka kuwa Mohammed Dewji alipambana Katika kupambana alipiga kelele walinzi wasifungue geti la kutokea collosium ndio maana watekaji wakapiga risasi juu na kufungua geti wenyewe, Vile vile kiatu chake kimoja kilivuka na pia kofia ilivuka, Mohammed Dewji katika kuona anazidiwa alidondosha funguo ya gari yake na simu ( naamini kuwa alidondosha funguo ya gari makusudi ili watu wachukue gari kukimbiza watekaji) bahati mbaya hapakuwa na mtu aliyethubutu kuwakimbiza watekaji wale.

Kwanini hizi taarifa hazikutolewa kwenye press ya Mkuu wa Mkoa wa ZPC? Kwanini Umma uliambiwa kuwa Mohammed Dewji alikubali tu kubebwa?

Jambo la mwisho kwa leo, ni la kawaida kwenye mambo ya uchunguzi, ni ganda la risasi ambayo ilitumika, Limeokotwa na Polisi? Kinachoitwa ‘ballistic report’ kimetolewa na kusambazwa duniani kwenye kanzidata za watengeneza silaha hii ingesaidia sana kuweza kujua umiliki wa silaha iliyotumika na kuwa na njia ya kuwapata watekaji na pia kumpata Mohammed Dewji, Jeshi la Polisi likipata msaada kutoka nje ya nchi laweza pia kufanikisha hili.

Mwisho, kumekuwa na kauli za kusema kuwa ‘wanasiasa wasitake umaarufu’ kwenye tukio hili hii ni kauli ya hovyo na inapaswa kupuuzwa, Mamlaka za Serikali zimejengwa kusimamiana, Waziri Kivuli Mhe. Godbless Lema ana wajibu wa kumhoji Waziri wa Mambo ya Ndani bila kuonekana anaingiza siasa, Hakuna kipindi Serikali imepewa fursa ya kupumua kwenye tukio kama tukio hili la kutekwa kwa Mohammed Dewji.

Wanasiasa wa upinzani tulikaa kimya kupisha vyombo kufanya kazi zake, Serikali kuanza kuweweseka pale wabunge wanapotimiza wajibu wao kuhoji kunatia mashaka kwamba kuna kitu Serikali inaogopa, Serikali inaogopa nini? Wanachokiogopa ndio kinaogopesha kukaribisha Wachunguzi wa kimataifa?.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.