ZANZIBAR WAADHIMISHA KUMBUKUMBU YA SIKU YA MAPINDUZI

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein anahutubia taifa leo katika kilele cha miaka 55 ya mapinduzi matukufu kwenye Uwanja wa Gombani uliopo mjini hapa.

Hotuba yake inahitimisha sherehe za mapinduzi ambazo zilianza kuadhimishwa tangu Desemba 31 mwaka jana kwa shughuli za kufanya usafi katika Wilaya za Pemba na Unguja huku akipokea maandamano ya wananchi na paredi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Kwa mujibu wa Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed viongozi wa kitaifa na wawakilishi wa nchi mbalimbali wanahudhuria maadhimisho hayo yanayofanyika kuanzia saa kumi na mbili asubuhi kwa wananchi kuingia katika uwanja wa Gombani.

Uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watu 20,000 pia utakuwa na shughuli za ngoma kuonesha utamaduni wa wananchi wa Zanzibar kwa wageni. Aboud alisema kwamba Rais John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wanahudhuria sherehe hizo zenye kukumbusha kuondolewa kwa nguvu kwa dhuluma na unyanyasaji visiwani hapa baada ya juhudi za kisiasa kushindwa. Alisema sherehe hizo pia zinahudhuriwa na Marais wastaafu nchini Zanzibar na Jamhuri ya Muungano, mawaziri wakuu wastaafu na mawaziri viongozi wastaafu.

Pia alisema serikali imekodi ndege kwa ajili ya kuwaleta Kisiwani Pemba wawakilishi wa mataifa ya nje hapa nchini. Hali ya utulivu imetamalaki katika kisiwa hiki ambacho kinatambuliwa kama ngome ya Chama cha Wananchi (CUF). Kutoka bandarini Mkoani, Pemba hadi kufika mjini Chakechake kumepambwa na bendera za Taifa na CCM na aina mbalimbali za mapambo yenye rangi ya kijani, nyeusi bluu na manjano na mabango yanayosifia mapinduzi matukufu.

Pilikapilika na wananchi katika maeneo mbalimbali ya maadhimisho katika visiwa vyote viwili vikubwa vya Pemba na Unguja vimefanya maadhimisho ya mwaka huu kuwa na heshima ya aina yake ingawa hapakuwepo na rangi za CUF katika maeneo mbalimbali yenye pilika kubwa. Aidha utoaji wa tunu kwa kuenzi mapinduzi uliofanyika Jumatano kulionesha jinsi serikali ya Mapinduzi Zanzibar inavyojali watu wake.

Aidha katika siku takribani 11 za sherehe hizo miradi mbalimbali zaidi ya 68 yenye thamani ya mabilioni ya shilingi ama ilizinduliwa au kuwekewa mawe ya msingi. Akizungumza na gazeti hili Waziri wa Nchi Ofisi ya makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed alisema miradi hiyo ambayo ni ya kimkakati ni pamoja na miundombinu ya barabara, elimu, maji, nishati na afya na kuongeza kuwa uzinduzi wa miradi hiyo ulifanywa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwamo Rais Dk Shein , Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Samia Suluhu Hassanna Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Wengine ni mawaziri katika serikali ya mapinduzi na Jamhuri ya Muungano wakiwemo, Waziri wa Ulinzi na jeshi la Kujenga taifa Dk Hussein Ali Mwinyi, Waziri wa Maji Profesa makame Mbarawa. Upande wa Zanzibar baadhi ya mawaziri waliofanyakazi ya kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kufungua shughuli mbalimbali ni pamoja na Balozi Ali Abeid Karume,ambaye ni waziri wa vijana na utamaduni sanaa na michezo na waziri wa biashara na viwanda Amina Salum Ali.

Baadhi ya miradi iliyozinduliwa ni shule ya msingi Chimba, Kituo cha kuongozea ndege, uwanja wa ndege wa Karume uliopo Chakechake, mradi wa umeme Ungi Msuka, Jengo la taasisi ya utafiti wa afya na kituo cha afya Kiuyu Kipangani. Aidha mawe ya msingi yamewekwa katika ujenzi wa daraja la Kibonde mzungu na shule ya Wawi Msingi. Pia jiwe la msingi liliwekwa katika nyumba ya Makamu wa pili wa rais wa Zanzibar.

Jana katika viwanja vya Tibirinzi wilaya ya Chakechake Pemba na Maisara wilaya ya Mjini Unguja, majira ya saa tano kulikuwa na urushaji wa fashidfashi za maadhimisho ya sherehe za miaka 55 ya mapinduzi. Aliyeshuhudia fashifashi hizo ni makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. Sherehe hizo ambazo zitahitimishwa usiku kwa taarabu rasmi ya kikundi cha Taifa-Zanzibar na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein. Aidha Jumapili kuanzia saa nane kutakuwa na fainali za Kombe la mapinduzi zitakazofanyika uwanja wa Gombani.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.