WAZIRI WA NISHATI DKT. KALEMANI AMETOA AGIZO HILI KWA TANESCO MTWARA.

 

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ameuagiza uongozi wa juu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuteua na kupeleka meneja atakayesimamia halmashauri ya Nanyamba wilayani Mtwara, ili pamoja na mambo mengine aharakishe zoezi la uunganishaji umeme kwa wananchi.

Ametoa agizo hilo jana, Disemba 5 akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi wa Mtaa wa Kilimanjaro, waziri Kalemani alisema ukosefu wa ofisi ya TANESCO katika eneo hilo ni mojawapo ya sababu zinazochelewesha zoezi la kuwaunganishia umeme wananchi.

“Najua hapa hakuna Ofisi ya TANESCO. Mtu wa kuwahudumia anatoka Tandahimba. Hivyo naagiza, kuanzia kesho awepo Meneja hapa ambaye atasimamia Nanyamba peke yake” amesema Dkt Kalemani.

Miongoni mwa majukumu makuu ambayo waziri ameelekeza yatekelezwe na meneja atakayeteuliwa ni pamoja na kuhakikisha ndani ya siku 20 kuanzia kutolewa kwa agizo, wananchi wote waliolipia wawe wameunganishiwa huduma ya umeme.

Pia amesema meneja husika atawajibika kumsimamia mkandarasi anayeunganisha umeme katika eneo hilo kuongeza kasi ya kazi ili kushawishi wananchi wengi zaidi kulipia na kuunganishwa.

Aidha waziri Kalemani amewaahidi wananchi wa Mtaa wa Kilimanjaro kuwa watapatiwa umeme kupitia mpango wa umeme vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutokana na uhalisia wa eneo hilo kuwa na sifa za kijiji zaidi badala ya mtaa kama ulivyoainishwa.

“Mtaa wa Kilimanjaro na vitongoji vyake mtaunganishiwa umeme wa REA ambao gharama yake ni shilingi 27,000 tu,” amesisitiza.

Kwa upande mwingine waziri Kalemani amewashauri wale wasio na uwezo wa kugharamia utandazaji wa nyaya za umeme katika nyumba zao, kutumia kifaa mbadala cha Umeme Tayari (UMETA) ambacho huuzwa kwa bei rahisi ya shilingi 36,000 tu.

Hata hivyo, Waziri amebainisha kuwa serikali imetoa vifaa hivyo 200 bure kwa ajili ya wananchi watakaowahi kujitokeza ili kuunganishiwa umeme.

Katika ziara hiyo, waziri Kalemani amewasha umeme katika moja ya nyumba ya mwananchi aliyeunganishiwa, na kutembelea na kukagua miradi ya umeme, kuzungumza na wananchi na kuwasha umeme katika maeneo mengine kadhaa ikiwemo Namambi.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.