WAZIRI MKUU WA UINGEREZA THERESA MAY ANUSURIKA KURA YA KUTOKUWA NA IMANI NAYE

London, UINGEREZA.

Waziri mkuu wa Uingereza, Theresa May, amenusurika kura ya kutokuwa na imani naye kutoka kwa wabunge wa chama chake cha Conservative, baada ya hapo jana Wabunge 200 dhidi ya 117 kupiga kura kumuunga mkono.

Wabunge (117) hao ambao ni sawa na theluthi moja hawakumpigia kura Bi May kusalia kuwa kiongozi mkuu wa chama hicho na waziri mkuu, hali inayomaanisha kuwa kiongozi huyo amepoteza uungwaji mkono wa wabunge wengi ndani ya chama chake.

Hatua hiyo inaashiria Bi May bado anakabiliwa na changamoto kubwa kutekeleza mpango wake kuhusu mchakato wa Uingereza kujiengua kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya ujulikanao Brexit.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa, May amesema amefurahi kupata uungwaji mkono wa wanachama wenzake wa Conservative katika kura hiyo iliyopigwa jana usiku.

Mbunge Jacob Rees Mogg, mmoja wa wabunge 48 waliowasilisha barua ya kutaka kura hiyo ya kutokuwa na imani na uongozi wa May amesema matokeo hayo ni ya kusikitisha akisitiza May anahitaji kujiuzulu mara moja.

Kabla ya kura hiyo, May aliwaahidi wabunge wa chama chake kuwa hatawania muhula mwingine wa kukiongoza chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2022.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.