WAZIRI MKUU AAGIZA UCHUNGUZI WA FEDHA ZA DAWA MPWAPWA

 

Na Stephen Noel @Dar mpya MPWAPWA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri kuchunguza matumizi ya sh. Milioni 70 zinazotelewa na serikali kwenye wilaya hilo kila mwezi kwa ajili ya kununulia dawa.

Majaliwa alitoa agizo hilo juzi jioni wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mpwapwa.

Kwenye mkutano huo wananchi wamelalamika kuhusu ukosefu wa dawa ambapo dawa pekee ambazo hupatiwa ni za kutuliza maumivu.

“Nilidhani wabunge wanachosema Bungeni sicho nikasema nakuja niyasikie, Kweli wananchi hawaridhiki nimeona.

“Sasa mkuu wa wilaya shughulika na hili kubaini fedha za dawa zinakwenda wapi,” aliagiza.

Alisema lengo la Serikali kutoa feha hizo kila mwezi ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kokote walipo badala ya kufunga safari kwenda kwenye makao makuu ya wilaya.

“Zaidi ya sh Milioni 70 zinazotolewa kila mwezi kununuliwa dawa kwenye wilaya hii, kuna fedha ya mfuko wa afya Milioni 60 pia zipo fedha za matokeo mazuri ya afya sh. Milioni 300 kwa mwaka. Shida ya dawa isingeweza kujitokeza,” alibainisha.

Amefafanua kuwa Serikali inatimiza mambo ambayo wananchi wanayahitaji kwa lengo la kuwatumikia kwa kuleta fedha hizo za dawa.

Awali kabla ya mkutano huo, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpwawa, Paul Swea kuwahamishia vijijini baadhi ya watumishi waliopo kwenye idara ya kilimo.

Amechukua hatua hiyo baada ya kubaini idara hiyo kuwa na watumishi saba ambao wote wapo ofisini badala ya kufanyakazi vijijini kuwasaidia wananchi kwenye shughuli za kilimo.

Amemtaka Mkurugenzi huyo kuandika barua za uhamisho kwa watumishi hao kwenda vijijini kisha nakala za barua hizo akabidhiwe kabla hajaondoka wilayani hapo.

Amesisitiza watumishi hao wanapaswa kwenda kufanyakazi na wakulima kwa karibu na kuhakikisha wanawapa elimu ya kutosha itakayowawezesha kulima kwa kisasa.

 

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.