WAZIRI AZINDUA MBIO ZA BAISKELI, ACHANGISHE Mil 280 KUSAIDIA SEKTA YA ELIMU

NA MWANDISHI WETU
NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda amezindua mpango wa mashindano ya mbio za baiskeli na kufanikisha kukusanya Sh milioni 280 kati ya Sh milioni 340 zinazotarajiwa kukusanywa kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini.

Mashindano hayo yaliyopewa jina la ‘Imara Pamoja Cycle Challenge’, yameandaliwa na Kampuni ya Uchimbaji wa Madini nchini -Acacia kwa kushirikiana na Tasisi binafsi kutoka nchini Canada – CanEducate.

Akizungumza katika uzinduzi wa uchangiaji wa mashindano hayo juzi jijini Dar es Salaam, Kakunda alitoa wito kwa wadau mbalimbali nchini kujitokeza kuchangia mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 3, mwaka huu katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kakunda ambaye alimwakilisha Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, alisema malengo ya mashindano hayo yanaenda sambamba na malengo ya serikali katika kurahisisha mazingira ya utoaji elimu nchini.

“Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani na kufuta ada za shule pamoja na ada za ziada, hadi mwaka jana kumekuwapo na ongezeko la asilimia 44 la uandikishaji wanafunzi wapya wa elimu ya awali, ongezeko la asilimia 33 la uandikishaji wanafunzi wapya wa darasa la kwanza na wanafunzi wapya wanaojiunga na elimu ya sekondari wameongezeka kutoka 366,396 mwaka 2015 hadi 483,216 mwaka 2017”, alisema.

Alisema hatua hizo zinahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali kama wanavyofanya Acacia katika kufikia malengo ya serikali.

Aidha, Mkurugenzi wa Acacia nchini, Asa Mwaipopo alisema kwa mwaka jana pekee kampuni hiyo imejenga madarasa na kukarabati mabweni yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 100 wa kike katika Shule ya Sekondari Mwendakulima iliyopo wilayani Kahama.

Pia imefanikisha ujenzi wa maktaba sita katika shule zinazozunguka migodi ya kampuni hiyo.

“Tangu tuanze kushirikiana na CaEducate mwaka 2011 katika kuboresha sekta ya elimu nchini, Acacia imetumia zaidi ya sh milioni 450 zilizofikia shule 20 na wanafunzi zaidi ya 5000.

“Acacia pia imewekeza katika mfumo maalumu wa utoaji wa mafunzo kwa vitendo (IMTT) kwa vibarua au wanagenzi wanaotoka katika vijiji vinavyozunguka migodi yetu.

“Mafunzo hayo yaliyoanza mwaka 2009 kwa kushirikiana na Veta na Chama cha Wachimbaji wa Madini nchini, Acacia imetumia zaidi ya Sh bilioni 3.3 kutoa mafunzo hayo kwa wanagenzi 744 katika migodi yake mitatu ya Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi,” alisema.

Pia alisema tangu mwaka 2008 Acacia imetumia Sh bilioni moja kusaidia wanafunzi wa elimu ya juu wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili (MUHAS).

Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi wa kampuni ya kimataifa ya Ernst and Young iliyotolewa mwaka jana, ilionesha kuwa Acacia imechangia Sh trilioni 1.61 katika uchumi wa Tanzania sawa na asilimia 1.5 ya Pato la Ndani la Taifa.

“Kutokana na hali tunatoa wito kwa wadau wote kujitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi za Acacia katika kuboresha sekta ya elimu nchini, ” alisema.

Naye Rais wa taasisi ya CanEducate, Rishi Ghuldu alisema kila mwaka taasisi hiyo huwezesha kielimu wanafunzi 270 na kutoa nafasi 11 za udhamini wa masomo ya elimu ya juu katika vyuo mbalimbali duniani.

Alisema tasisi hiyo imelenga kuboresha sekta ya elimu ili kusaidia familia maskini kupiga hatua kimaendeleo.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha alitoa wito kwa Acacia kuelekeza nguvu zaidi katika ujenzi wa mabweni na hosteli ili kuwasaidia wanafunzi wanaotumia umbali mrefu kufika shuleni.

Wakati mmoja wa wanufaika wa mpango huo wa CanEducate, Yunista Marwa ambaye ni mhitimu wa kidato cha sita, alitoa wito kwa Acacia kuendelea kuwasaidia wanafunzi wanaotoka katika kaya maskini ili waweze kuzisaidia familia zao na jamii kwa ujumla.
Mwisho.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.