WACHINA WANAONYANYASA WATANZANIA WAFUKUZWA

Waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano, mhandisi Isack Kamwelwe amewafukuza nchini watu wawili raia wa china na kuwataka waondoke mara moja kwa kosa la kuwapiga na kuwanyanyasa watanzania walioajiriwa kufanya kazi katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya –Makongorosi mkoani Mbeya inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Pia waziri amedai kuwa kumekuwepo na ucheleweshaji wa mradi huo ambao hadi sasa uko nyuma kwa mujibu wa ratiba ya mkataba mradi unaotekelezwa na kampuni ya China Railwe Company Limited kutoka nchini China.

Waziri Kamwelwe amefanya ziara ya kushtukiza ya kutembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya – Makongorosi lakini akiwa njiani akasimamishwa na wananchi wa kijiji cha Matundasi wilayani Chunya ambao wamemueleza kuwa wasimamizi wa mradi huo ambao ni raia wa China wanawanyanyasa kwa kuwapiga, kuwatishia kuwaua kwa silaha za moto, kuwakata mishahara yao na kuwafukuza kazi bila sababu za msingi.

Waziri Kamwelwe pia alihoji utendaji kazi wa kampuni hiyo katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, na ndipo mwakilishi wa kampuni Smec Company Limited inayosimamia mradi huo kwa niaba ya Serikali, Gosbert Luburi akaeleza kuwa ratiba ya ujenzi wa barabara hiyo iko nyuma ikilinganishwa na makubaliano ya mkataba.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, waziri Kamwelwe amesema kuwa barabara hiyo inajengwa kwa kodi za watanzania kwa asilimia mia moja, na kwa mantiki hiyo watanzania wa chini ndio waliowaajiri wachina hao kupitia kodi zao, hivyo Serikali haiwezi kuvumilia unyanyasaji wa aina hiyo ambao ameufananisha na ukoloni na ndipo akatoa uamuzi wa kuwatimua nchini watu wawili raia wa China ambao wametajwa na wananchi kuwa ndio vinara wa unyanyasaji dhidi yao.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.