WABUNGE WAZIDI KUIKOMALIA SERIKALI KUHUSU UKOSEFU WA AJIRA KWA WAHITIMU VYUO VIKUU

Wabunge wameendelea kuikomalia serikali kuhusu tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wanaohitimu elimu ya juu, ambapo katika nyakati tofauti wameonyesha kutoridhishwa na majibu ya serikali kuhusu mikakati yake ya kuiondoa changamoto hiyo.

Mjadala huo uliibuliwa tena bungeni na Mbunge wa Momba, David Silinde ambapo wakati akiuliza swali amesema majibu ya serikali yameshindwa kutatua tatizo la ajira nchini.

“Majibu ya serikali ni ya siku zote ambayo yameshindwa kutatua tatizo la ajira nchini, na unaweza kuonyesha mifano midogo, sera ya uchumi na viwanda kwenye bajeti peke yake serikali imeshindwa kupeleka fedha kuwezesha viwanda kuanzishwa na wananchi kupata ajira, katika kipengele cha tano serikali inasema serikali moja ya mkakati wake ni kutoa mikopo nafuu kwa vijana, kwenye bajeti serikali tuliyopitisha unakuta mfuko wa maendeleo ya vijana umetengewa  bilioni 1,” amesema Silinde.

Mjadala huo ulikolezwa na Mbunge wa Vunjo, James Francis Mbatia aliyehoji mkakati wa serikali katika kuhakikisha inaanzisha mfumo wa elimu unaoandaa vijana kuwa wabunifu na uwezo wa kujiajiri ikiwemo kuandaa mitaala maalumu ya masomo shuleni na vyuoni.

Naye Mbunge Viti Maalumu (CCM)Catherine Magige, amehoji kwamba, kwa kuwa waajiri wengi wanapotoa nafasi za ajira wanakipa kipaumbele kigezo cha uzoefu,  serikali ina mpango gani wa kusaidia vijana wanaotoka vyuoni waajiriwe pasipo kuulizwa uzoefu.

Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula amehoji mkakati wa serikali katika kurasimisha vijana wenye ujuzi ambao hawajapitia mfumo rasmi wa mafunzo kitendo kinachopelekea kukosa ajira .

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde amesema “Katika kuhakikisha wahitimu kuongeza fursa za ajira,serikali inaendelea  kusimamia utekelezaji wa sera ya ujenzi wa viwanda, utekelezaji miradi mikubwa, kutoa elimu kwa vijana kuhusiana na masuala ya ajira kuwaongezea ujasili wa kujiajiri, kuendelea kuwezesha vijana kujiajiri kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana.”

Mavunde amesema serikali chini ya ofisi ya waziri mkuu ina mpango wa miaka 5 wa ukuzaji ujuzi kwa vijana ambapo lengo ni kufikia vijana milioni 4.4 ifikapo mwaka 2021 kupitia mfumo wa urasimishaji ujuzi kwa vijana wenye ujuzi ambao hawajapitia mfumo rasmi wa mafunzo.

“Sisi na wizara ya elimu tunafanya kazi ya pamoja ili kuona namna bora ya kuja na mitaala ili kijana wa kitanzania anapohitimu elimu awe ana sifa ya kuajirika ili apate nafasi ya kuajiriwa,” amesema.

Kwa upande wake Naibu Waziri Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema kuna haja ya kuhakikisha vijana wanakua wabunifu na kwamba sasa wizara hiyo ina mkakati wa kuhakikisha inakuza stadi za kazi  shuleni ili vijana wakimaliza waweze kujiajiri.

“Sio kazi zote zinahitaji uwe unapata uzoefu, kuna kazi zinatangazwa hazihitaji uzoefu, lengo la kuanzisha mfumo unaofundisha stadi za kazi ili vijana wahitimu wawe tayari wameanza kupata mafunzo ili wakienda kwenye ajira wawe tayari wanauwezo kuajirika,” amesema.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.