UBUNGO KUUPOKEA MWENGE WA UHURU KWA KISHINDO

Wilaya ya Ubungo iliyopo mkoani Dar es Salaam imesema ipo tayari kuupokea Mwenge wa Uhuru kwa kishindo kikubwa, na kuwa tayari wananchi wamejiandaa vya kutosha kupamba mapokezi ya mwenge huo.

Hayo yamesemwa asubuhi ya leo Julai 9, 2018 na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Kisare Makori alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,  Kibamba jijini Dar es Salaam.

Mhe. Makori amesema kuwa wilaya yake itaupokea mwenge huo siku ya kesho tarehe 10 Julai, 2018 ukitokea wilaya ya Kinondoni, ambapo baada ya kutoka wilayani Ubungo mwenge huo utaelekea katika wilaya ya Temeke.

Mhe. Makori amesema mapokezi hayo yatafanyika Goba katika viwanja vya Tripple B, ambapo maandalizi yote yamekwisha kamilika, na kuwa wananchi wa Ubungo wanausubiri mwenge huo kwa shauku kubwa.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mhe. Makori, Jumla ya miradi saba inategemewa kuzinduliwa kupitia mbio hizo za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu katika wilaya ya Ubungo, ambapo ametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa maji, mradi wa ujenzi wa shule, barabara, na vituo vya afya.

Aidha Mhe. Makori amewashukuru wananchi wa wilaya ya Ubungo kwa kujitoa kwao kwa hali na mali kuchangia kwa hiari mbio hizo, ambapo jumla ya fedha za kitanzania shilingi millioni 26, 526, 000/= zimepatikana kupitia michango hiyo ya wananchi.

Katika hatua nyingine Mhe. Makori ametumia wasaa huo kuwaomba wananchi wa Ubungo kujitokeza kwa wingi siku ya kesho kuanzia majira ya saa mbili asubuhi katika maeneo ya Tripple B, Goba , kwaajili ya mapokezi ya mwenge huo.

Mhe. Makori amehitimisha kwa kuwahimiza watanzania kuendelea kupiga vita vitendo vya rushwa, huku akirejelea kauli ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli aliyoitoa siku ya jana wakati wa mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeng kuwa, ‘Tanzania imeweza kufikia hatua ya kununua ndege hiyo baada ya kudhibiti mianya ya rushwa’.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.