‘TUMETEKELEZA AHADI KWENYE KATA ZINAZOONGOZWA NA CHAMA CHETU’, ACT WAZALENDO.

Mapema siku ya leo Julai 11, 2018, chama cha ACT Wazalendo kimetoa taarifa ya utekelezaji wa ahadi ilizozitoa katika kata zinazoongozwa na chama hicho, wakati wa ziara maalumu ya kutembelea kata hizo kati ya tarehe 19 Februari hadi tarehe 9 Machi mwaka huu.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa ahadi hizo kwenye ofisi za makau makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam, Katibu Bunge na Serikali za Mitaa, ACT Wazalendo, mama Janeth Rithe amesema kuwa mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo, chama kilianzisha harambee kwa wanachama na viongozi kwa ujumla kwaajili ya kuchangia fedha za ujenzi na ukarabati wa shule, zahanati, miundombinu ya maji, na barabara.

Kupitia harambee hiyo kiasi cha jumla ya shilingi milioni arobaini na mbili sitini na mbili elfu (42,062,000/=) kilipatikana ambapo fedha hiyo imeweza kutumika katika kununulia vifaa mbalimbali ili kutatua changamoto zinazopatikana kwenye kata walizotembelea.

Rithe amesema kuwa kiasi hicho kimewawezesha kununua mabati 1337 kwa ajili ya ukarabati wa shule na zahanati kwenye kata zao walizotembelea, vilevile wameweza kununua vifaa vya kukarabatia miundombinu ya maji kama vile ‘valve’ kwenye kata ya Sale iliyoko Ngorongoro mkoani Arusha.

Ametaja vifaa vingine vilivyonunuliwa kuwa ni vifaa vya kukarabati barabara kwenye kata ya Kikeo iliyoko Mvomero mkoani Morogoro.

Aidha, Rithe amesema pia licha ya upatikanaji wa vifaa hivyo, bado wanahitaji kiasi cha shilingi milioni thelathini na tatu laki mbili themanini na nane elfu (33, 288, 000/=) ili kuwawezesha kupata vifaa kama saruji mifuko 252 na nondo kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa madarasa, zahanati, na ujenzi wa madaraja ili kufungua mawasiliano ya barabara  katika baadhi ya kata zilizosalia.

Akitoa sababu za kwanini chama cha ACT Wazalendo kimeamua kufanya shughuli ya utekelezaji kero za wananchi ambalo kimsingi ni jukumu la serikali inayoongoza, Rithe amesema kuwa wameamua kufanya hivyo kwani chama chao kimejengwa katika misingi ya kijamaa ya kuwasaidia wananchi wanyonge.

“Kwa kuwa ACT Wazalendo ni chama cha kijamaa na kinasumumwa na falsafa yake ya Siasa ni Maendeleo, chama kinao wajibu wa kuwaunga mkono wananchi wanyonge katika mapambano ya kushughulikia kero zinazowakabili, kiliamua kutafuta njia mbadala za kutatua baadhi ya kero hizo”, amesema Rithe.

Mama Rithe amehitimisha kwa kuendelea kuwakaribisha wanachama na wananchi kuendelea kukichangia chama ili kiweze kutatua kero zote zilizosalia, huku akitaja kuwa wanapokea pia michango ya vitu au vifaa husika kama mabati, saruji na nondo.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.