TUCTA YAITAKA SERIKALI KUKAA MEZA MOJA KUHUSIANA NA MAFAO YA WASTAAFU

Na Heri Shaban,Morogoro

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) limesema linatarajia kukutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, ili kukaa pamoja kuhusiana na vikokotoo vya Pensheni

Tamko hilo limetolewa katika kikao cha 35 cha shirikisho la wafanyakazi mkoani Morogoro Desemba 05, 2018 na Rais wa TUCTA, Dkt. Tumaini Nyamhokya, wakati akitoa tamko la Kamati ya Utendaji ya TUCTA Taifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na wa kikokotoo cha mafao ya pensheni yaliotolewa na mifuko ya hifadhi ya Jamii Tanzania.

“TUCTA ni Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi 13 nchini, kikao chetu kimeazimia kwenda kumuona Waziri mwenye dhamana mjini Dodoma kuhusiana na masuala ya vikokotoo, ili tukae meza ya pamoja kuzungunzia masuala ya mafao kufuatia mifuko kuunganishwa wafanyakazi wamepokea kwa mtazamo tofauti “alisema Dkt Tumaini.

Dkt Tumaini alisema hoja kuu ya mifuko ya hifadhi ya Jamii nchini iliyoanzishwa na wafanyakazi tangu mwaka 2004, ilikuwa na lengo la kuboresha mafao ya wafanyakazi na wastaafu.

Aidha, kiongozi huyo aliongeza kuwa wafanyakazi waliamini kuwa mifuko ya hifadhi ya Jamii ikiunganishwa gharama za uendeshaji na ushindani isiyokuwa na tija kwa mfanyakazi ingepungua, hivyo mifuko kuokoa fedha nyingi ambazo zingeelekezwa kuboresha mafao ya Wafanyakazi.

“Serikali na wadau wengine wakiwemo waajiri walipokea hoja ya wafanyakazi na kuanza mchakato wa uunganishwaji wa mifuko, ambapo TUCTA kwa niaba ya wafanyakazi tulishirikishwa katika mawasiliano ya Utatu kupitia vikao vya kisheria,

“Pia vilitoa fursa ya wawakilishi wa wafanyakazi kukutana na kujadiliana na wadau wote wakiwemo waajili, Serikali, Kamati za Bunge, NGOs, watumishi wa mifuko iliyokuwepo kabla kuunganishwa na wafanyakazi wenyewe.” alisema Dkt Tumaini.

Aidha, Dkt Tumaini alisema TUCTA kama Mwakilishi wa wafanyakazi nchini, wao walishiriki katika mchakato mzima wa kutungwa kwa sheria ya PSSSF namba 2 ya mwaka 2018, kwa kutoa maoni na msimamo wao katika vikao mbalimbali vya wadau.

Ambapo amefafanha wajibu na haki yao kwamba, mapendekezo hayo kwenye sheria hiyo yalizingatiwa kwa kiwango kikubwa sana, lakini tatizo limekuja kujitokeza kwenye utungwaji wa kanuni kwa mujibu wa kifungu cha 25 A cha sheria ya SSRA ya 2018, ambapo Waziri mwenye dhamana amepewa mamlaka ya kutunga kanuni za sheria za mufuko na kanuni za vikokotoo vya mafao ya kustaafu nchini.

Akifafanua namna walivyo (TUCTA) shirikishwa, Dkt Tumaini alisema baada wasilisho la TUCTA la hoja ya Wafanyakazi katika vikao hivyo vya wadau, Serikali na TUCTA walishindwa kukubaliana, hivyo serikali iliamua hoja za pande zote ziwashirishwe kwenye baraza la utatu la ushauri (LESCO), ambalo lina wawakilishi mbalimbali na mapendekezo hayo katika baraza hilo hayakukubaliwa na serikali.

Kiongozi huyo wa alimalizia kwa kusema kuwa, kwa kuzingatia hekima na busara, na kwa kutambua mchango mkubwa wa wafanyakazi hapa nchini, ni vyema serikali ikaliona hilo, na kuchukua hatua za haraka na za makusudi za kurudi katika meza ya mazungumzo na vyama vya wafanyakazi kwa lengo la kuhakikisha suala hili linapatiwa ufumbuzi utakaoleta tija kwa wafanyakazi na taifa kwa jumla.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.