TADB YANYANYUA HALI YA KIPATO CHA MKULIMA MDOGO NCHINI.

 

 

Na mwandishi wetu, Karagwe Kagera

Benki ya maendeleo ya kilimo nchini (TADB) imesema imejipanga kunyanyua hali kipato cha wakulima wadogo wadogo nchini kupitia ushirika wao kwa kuwapatia mikopo ya gharama nafuu ili waweze kumudu gharama za uzalishaji.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bibi Rosebud Kurwijila, wakati alipotembelea na kufanya mazungumzo na uongozi wa Chama cha Ushirika Karagwe (KDCU) mkoani Kagera ili kujionea namna mkopo uliotolewa na TADB zilivyosaidia katika ununuzi wa zao la kahawa kwa msimu ulioishia mwezi Oktoba mwaka huu.

Bibi Kurwijila amesema kuwa TADB imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inanyanyua hali ya kipato cha mkulima mdogo nchini ili aweze kubadilisha maisha yake kupitia vyama vyao vya ushirika.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunaboresha kipato cha mkulima mmoja mmoja kupitia ushirika wao ili waweze kuinua hali zao kiuchumi,” amesema.

Bibi Kurwijila amesema kuwa TADB imeanzishwa katika kipindi kifupi kisichozidi miaka mitatu, lakini tangu imeanzishwa wamekwishatoa mikopo ya shilingi bilioni 55, ukiwamo wa KDCU wa shilingi bilioni 14, na kuwa hawatoi mikopo kwa mtu au taasisi ambayo haionyeshi mpango wa namna gani wananchi waliomzunguka watanufaika.

“Nimefurahi kutembelea baadhi ya wateja wetu na kukuta fedha walizokopeshwa zimewanufaisha walengwa wa mkopo huu,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa mbele ya Mwenyekiti huyo wa TADB, wakulima wa zao hilo katika wilaya za Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera wamefanikiwa kukusanya kahawa kilogramu milioni 39.4 zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 39.4, katika msimu wa mwaka huu.

Akitoa taarifa hiyo, Mwenyekiti wa KDCU, Bw. Anselimi Kabateleine alisema kuwa kiwango cha kahawa kilichokusanywa katika msimu huu hakijawahi kufikiwa tangu KDCU ilipoanzishwa, na kuwa mafanikio hayo yamewezeshwa na mfumo wa sasa unaovipa vyama vya ushirika vya msingi nguvu za ukusanyaji kahawa.

“Tunaishukuru serikali kwa kubadilisha mfumo wa ukusanyaji wa kahawa, kwa sasa kahawa imekusanywa ya kutosha kupitia vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS), lakini pia tunaishukuru TADB kwa kutupatia mkopo wa shilingi bilioni 14 uliotuwezesha kuwalipa wakulima kwa wakati” amesema.

Pia amesema katika malipo ya awali zimelipwa shilingi 1,000 kwa kila kilo moja ya kahawa, na kuwa kwa sasa kuna kahawa kilogramu milioni tatu haijapata mnunuzi, ambayo ikiuzwa fedha zitakazopatikana zitatumika kuwaongezea wakulima malipo ya pili.

Naye kaimu mkuu wa mkoa wa Kagera Deodatus Kinawilo alisema kuwa serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na TADB katika kuinua wakulima hasa wa zao la kahawa, ambalo ni tegemeo kwa mkoa huo.

“Maprofesa mnaowaona wanaotoka mkoa wa Kagera wamesomeshwa na kahawa, kwa hiyo sisi kama serikali tunaahidi kuendelea kusimamia fedha zinazotolewa na TADB kuwezesha wakulima wa kahawa, ili kuhakikisha zinatumika inavyokusudiwa na kurejeshwa kwa wakati”. amesema Kinawilo.

Kinawilo ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Bukoba amesema kuwa Kagera kuna maeneo mengi ya uwekezaji ikiwamo ardhi ya kutosha, na kuwaomba watu wenye nia ya kuwekeza kujitokeza kwa wingi.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.