SIMULIZI: SHANTELL-01

Na Pastory Raymond

Ilikuwa ni Jumatatu kama Jumatatu zingine. Pilika pilika zilikuwa nyingi Kama ilivyo katika miji mingi Duniani. Mwanzo wa wiki tena! Wanafunzi wanaonekana nadhifu, Kila mtu mjini anaonekana mwenye shauku ya kutekeleza adhma aliyojiwekea katika wiki mpya. Wakati wengine wakiwa wana adhma zao wengine walikuwa wana uchovu kwa kusakata rumba wikiendi na kunywa vileo mbalimbali. Huku wengine wakiilani kwanini Jumatatu ilifika mapema. Wengine wakifurahi hasa wafanya biashara ndogondogo ambao washitiri wao wengine ni wale waliopo maofisini kwani wikiendi huwa wapo majumbani mwao na hivyo kutokuambulia mia mbili mia tatu kutoka kwao.

Siku hii itabaki katika kumbukumbu za maisha ya Shantell pengine mpaka mwisho wa uhai wake! Ni siku ambayo ilifungua milango ya mapenzi, mafanikio, usaliti, maumivu, visasi na kubwa Siri nyingi zilizojificha katika maisha yake.

Baada ya kujitazama kwa muda kwenye kioo alijiridhisha kuwa amependeza. Hakuridhishwa na nywele zake. Hakujua azibane au aziachilie. Akajaribu kuzibana kwa juu mtindo wa “kidoti” akaridhika na mtindo huo. Shati yake nyeupe yenye michirizi meusi aliichomekea katika suruali yake nyeusi iliyofungwa vizuri na mkanda. Shingoni alikuwa amejivingirisha skafu. Alivuta pumzi na alijiona tayari kabisa kwa usaili.

Shantell hakuwa binti mrembo ila alistahili neno zaidi ya urembo. Hakuwa mweupe Wala mweusi na kamwe hakuwahi kutumia mkorogo wowote ili ngozi yake ing’ae Nivea ilimtosha. Alikuwa na nywele ndefu za singa ambazo nazo hazikujua kemikali yeyote. Alikuwa mrefu mithili ya twiga. Kiuno Cha nyigu. Kifuani alikuwa amehifadhi dodo zilichomoza twii! Mwendo wake ulikuwa mithili ya mtu mwenye funza miguuni. Huenda ungehisi hakanyagi chini. Mfereji mdogo katikati ya meno yake ilimfanya avutie pale akikenua. Macho yake remburembu yangekufanya uhisi Kama amekurembulia na kukuchombeza kumbe alikuwa akikutazama tu. Huyo ndiye Shantell Mwaimu.
Baada ya kujiridhisha alibeba mkoba wake.
“Mama naenda zangu!”
“ Hutasubiri hata chai jamani”
“Asante mama nahofia kuchelewa”
Mama Shantell alimsogelea na kumkumbatia mwanaye.
“Kila la heri mwanangu! Mungu akutangulie mwanangu!”
“Amina, Asante mama!” alisema huku akikazana kama mtu mwenye kutaka kuwahi.

Mama Shantell hakuweza kushindana na chozi liliokuwa limemshinda nguvu. Alijikuta akitabasamu huku machozi yakimtiririka. Binti yake amekuwa sasa. Angesahauje unyama aliofanyiwa na Daniel Akkufor Mghana aliyeahidi kumuoa na kumuacha solemba kanisani siku ya harusi? Angesahauje fedhea aliyoipata? Angesahauje mshtuko alioupata baada ya kujigundua mjamzito baada ya Mghana huyo kumkimbia? Angesahauje jinsi alivyojaribu kuitoa mimba ya Shantell na asiweze? Na Leo anamuona akiwa amemeea kama shina la mgomba. Tunda la mwanaume pekee aliyewahi kumpenda na kuwa naye mpaka Sasa akiwa na umri wa miaka Arobaini na kenda.
Itaendelea kesho….

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.