SHANTELL-02

Na Pastory Raymond

Ilipoishia…..

Angesahauje mshtuko alioupata baada ya kujigundua mjamzito baada ya Mghana huyo kumkimbia? Angesahauje jinsi alivyojaribu kuitoa mimba ya Shantell na asiweze? Na Leo anamuona akiwa amemeea kama shina la mgomba. Tunda la mwanaume pekee aliyewahi kumpenda na kuwa naye mpaka sasa akiwa na umri wa miaka Arobaini na kenda.

Inaendelea….

Mwanamke huyu wa makamo aliyekuwa mbele yake aliivua miwani yake na hivyo kuyafanya macho yake yaweze kuonekana na kumpa mawazo ya kuwa siku zilizopita mama huyu alikuwa kisu kikali kilichokata mioyo ya wanaume wengi. Shantell alikuwa akimsikiliza kwa umakini.
“Honestly I am impressed…Na sioni sababu ya kutokukuajiri katika kampuni yangu…”
“Asante Sana, nashukuru Sana…”Shantell hakuweza kuficha hisia za furaha alizokuwa nazo.
“Easy, Easy…Don’t be so excited Shantell” alimwambia huku akitabasamu jambo liliomfanya Shantell arudi katika hali yake ya kawaida. Na kisha Mrs Williams aliendelea baada ya kugundua kuwa binti huyu ambaye amempa ajira shauku na furaha yake imerudi katika hali ya kawaida akaendelea.
“Kwa miezi kadhaa, kampuni yetu imekuwa haiendi vizuri. Kampuni imekumbwa na madeni makubwa na mauzo yamekuwa madogo. Sitamani kampuni hi ife maana ndio alama yangu, kampuni hi inabeba kumbukumbu nyingi zilizowahi kutokea katika maisha yangu. I was once pretty like you in my days….(anatabasamu) Ilinipasa kumuajiri mtu mwenye uzoefu kukuzidi katika nafasi hii lakini nimeamua kucheza kamari ya kufuatisha moyo wangu. Kwa kushirikiana na mwanangu kipenzi John ambaye siku si nyingi atakuwa akirudi toka Marekani mna jukumu kubwa ya kurudisha hadhi ya kampuni hii Shantell. This company means the world to me”. Sasa mama huyu alimwangalia machoni Shantell na kumpa mkono huku akiwa amemshika mkono.
“Kila la heri Shantell, unaweza ukaanza kazi kesho ila kama utahisi kuwa majukumu haya kwa binti mrembo kama wewe ni magumu usijali usifike nitaelewa…” Alimaliza kwa tabasamu.
“Asante Mrs Williams”.

Alikuwa mwenye furaha iliyochanganyika na hofu! Ni dhahiri kuwa aliitaka kazi lakini kila akiyafikiria majukumu na matarajio ya Mrs Williams alihisi uoga ukimtafuna. Kila akiyafikiria maneno ya mama yule aliona sura ya mwanamke yule shupavu ambaye alikuwa akiongea pasi na mzaha hata kidogo. “Nitaweza” ilikuwa ni sauti kubwa iliyokuwa ikitoka kutoka dhati ya moyo wake na alikuwa amedhamiria kufanya makubwa kama Sales And Marketing Manager katika kampuni hii.
“Mama!!” aliita pale tu alipofika mlangoni.
“Shantee…” alitoka haraka haraka na kwenda mlangoni.
“ Vipi mwanangu, mambo yameendaje mama?…Hata kama umekosa usijali sehemu zipo nyingi utapata….”
“Ma-ma! Huachi hata nizungumze jaman….”
“Embu tuingie ndani maana Alimaua hii umbea watu hawachelewi kutega masikio”
Wakaingia ndani. Mama mtu akiwa na shauku ya kutaka kumsikia bintiye Ana lipi la kumwambia. Binti naye akiwa na fukuto la kumhabarisha mama yake juu ya kupata kwake kazi. Mama Shantell aliufunga mlango na kwenda pale alipokaa binti yake.
“ Longa mwali, nakuskiliza! Kimuhekimuhe kimenishika mtu mzima mimi!” Macho akiwa ameyatoa.
“Nimepata kazi mama”
Mama Shantell alijikuta amepiga magoti.
“Wewe ni Jehova baba, Nalihimidi na kulitukuza jina lako. Umezidi kudhihirisha uaminifu wako katika maisha yangu na ya binti yangu Shantell, nakupa sifa Mungu uketie kiti Cha juu enzini”.
“Amen!” Aliitikia Shantell.
Mama Shantell alikuwa na furaha isiyo na kifani. Waliongea mambo mengi huku akizidi kumpa mawaidha ni kwa namna gani anapaswa kuishi na watu kwa akili. Ukurasa mpya wa maisha ya Shantell ulikuwa umefunguliwa siku hiyo. Ukurasa ambao pengine utaleta sura nyingi katika kitabu Cha maisha yake.

Siku, wiki na miezi vikakatika. Shantell alianza kuzoea mazingira yake ya kazi huku akiwa mfanyakazi wa mfano. Kwa kipindi kifupi alichoanza kazi madeni yalianza kupungua taratibu kwani uzalishaji ulianza kuwa mzuri na mauzo yakaanza kuwa mazuri. Jambo liliomfanya Mrs Williams kuona alikuwa sahihi katika uchaguzi wake. Shantell hakuwa my mwenye makuu wala mawaa. Alikuwa mchangamfu muda wote, mtu mwenye matani, mtu muwazi, mkarimu na kikubwa zaidi hakuacha kuchapa kazi. Wapo waliomuonea soni ila wengi walimpenda na kustaajabu kumuona binti mdogo wa umri kuweza kuhimili majukumu yake ilihali ndani ya muda mfupi wazoefu wengi walipita na kushindwa kudumu hata kwa wiki mbili. Wengi waliondoka aidha kwa kushindwa kazi ama kutibuana na Mrs Williams. Mrs Williams hakuwa na mazoea na wafanyakazi wake. Alijenga misingi ya kazi tu. Hakupenda mazoea pia na watu wengine wa nje pia na hi ndio sababu iliyomfanya awe na marafiki wachache. Alitokea kumpenda sana Shantell. Alihisi anamkumbusha mambo mengi sana. Ndani yake alimuona binti mrembo mwenye akili na kiu ya mafanikio. Alipenda kwenda naye katika sehemu nyingi. Na kila alipokaa na marafiki zake wachache alionao hakuacha kumwaga sifa za Shantell.

Ilikuwa Ijumaa tulivu, mvua nyepesi ilikuwa ikinyeesha kuondoa vumbi liliokithiri jijini Dar-Es-Salaam. Kama ilivyo ada Shantell alikuwa ndio anafika kazini. Alisalimiana na kila aliyekuwa anapishana naye na wakati mwingine ilimlazimu asimame kidogo azungumze mawili matatu na mmoja au wawili ya anaokutana nao katika kuboresha kazi na hata pale anapokosoa usingehisi kama anakukosoa. Hatimaye alikuwa amefika ofisini kwake ambapo alilakiwa na ujumbe kutoka kwa katibu muhtasi wake yaani secretary
“Dada Shantell, mama kasema ukifika tu uende ofisini kwake!”
“Kwema kweli?” swali hili lilikuwa na wasiwasi ndani yake.
“Mimi nahisi itakuwa heri tu, wewe tena kipenzi chake!” alijaribu kumuondoa wasiwasi.
Hakutaka kupoteza muda, Mara moja alienda ofisini kwa Mrs Williams huku njiani akijirekebisha jirekebisha Mara koti Mara suruali mpaka alipofika mlangoni kwa mama huyu. Alibisha na kuingia.

Hakuwa peke yake kama alivyozoea siku zote. Alikuwa amekaa na kijana mwenye umri Kati ya thelathini mpaka thelathini na tatu.
“Unaweza ukakaa Shantell”
Huku akiwaza kijana yule atakuwa nani, Mrs Williams kama aliyekuwa mawazoni mwake akaamua kuuvunja ukimya.
“Meet my son John Marwa!”
“John, She is Shantell. The girl I have been telling you…..”
Itaendelea kesho…

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.