SERIKALI YASHINDA KESI DHIDI YA WANAHARAKATI KUHUSU KANUNI ZA MAUNDHUI MITANDAONI

Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara imehukumu kwamba Waziri wa Habari, Utamaduni, sanaa na Michezo hakukosea wala kukiuka Katiba kwa kutunga Kanuni za Maudhui Mitandaoni za mwaka 2018.

Hayo yamejidhihirisha baada ya Mahakama hiyo kusikiliza na hatimaye kuitupilia mbali kesi iliyofunguliwa na Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu, Bodi ya Wadhamini wa Baraza la Habari  Tanzania (MCT),  Mtandao wa Watetea Haki za Binadamu Tanzania (Human Rights Defenders Coalition) dhidi ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Katika shauri hilo walalamikaji wameshindwa kuthibitisha  jinsi gani Kanuni hizo zitakavyo athiri haki za msingi za Walalamikaji katika masuala ya uhuru wa habari na mawasiliano ya mitandaoni.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa leo Januari 9, 2019 Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, imekubaliana na hoja za  Mawakili wa Serikali kuwa Kanuni za Maudhui Mtandaoni zimetungwa kwa mujibu wa sheria na kupelekea Mahakama hiyo kutupilia mbali shauri hilo.

Shauri hilo liliendeshwa na mawakili kutoka Ofisi Mpya ya Wakili Mkuu wa Serikali ambao ni Bibi Alesia Mbuya, Bw. Ladislaus Komanya, Bw. Sylvester Mwakitalu, Bw. Johanes Kalungura, Bw. Killey Mwitasi, Bw. Abubakar Mrisha na Bibi Neisha Shao ambapo upande wa walalamikaji waliwakilishwa na mawakili Fulgence Masawe, James Marenga na Jeremia Mtobyesa.

Kwa hukumu ya kesi hiyo iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Septemba 4, 2018, sasa ni rasmi madai ya kwamba Kanuni hizo zinabana uhuru wa habari na kwamba zilitungwa kimakosa yaaanguka rasmi.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.