SERIKALI YA TANZANIA YAPATA TUZO YA KIMATAIFA YA KUPAMBANA MA MAGONJWA YASIYO AMBUKIZA(NCDs).

 

New York,Marekani.

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na watoto imepata tuzo ya kimataifa ya kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza(NCDs) kama vile Kisukari,Shinikizo la Damu,Magonjwa ya Moyo na Saratani.

Tuzo hiyo ya kimataifa,imekabidhiwa jana tarehe 27 Septemba,2018,kwa waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu na kikosi kazi maalumu cha Umoja wa Mataifa mahsusi kwa kupambana na Magonjwa Yasiyo ya kuambukiza (UN Interagency Task Force on the Prevention & Control of NCDs-UNIATF).

Hii ni kutokana na juhudi za Wizara ya Afya za kupambana dhidi ya Magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs),hususani katika kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara.

Tuzo hiyo ya kimataifa ya mwaka 2018,imekabidhiwa kwenye mkutano wa viongozi wa juu wa umoja wa Mataifa (United Nations High Level Meeting on NCDs) unaofanyika Mjini New York, Marekani.

Tanzania ni miongoni mwa nchi nchi tisa Duniani ambazo zimefanikiwa kupata tuzo hiyo ambayo imetolewa kwa mara ya kwanza katika ngazi ya kiserikali Duniani,Tanzania ilichagulia kupata tuzo hiyo baada ya mapendekezo yaliyoandikwa na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyo ya kuambukizwa Tanzania (TANCDA).

Hii ni kutokana na juhudi zinazofanywa na serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais Dr. John Pombe Magufuli katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata habari ya namna ya kujikinga na magonjwa haya.

Timu ya UNIATF imeipongeza Tanzania kwa kuanzisha programu ya kuhamasisha jamii kufanya mazoezi kama sehemu ya maisha yao.

“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NDC) ndiyo yanayoongoza duniani kwa sasa kwa kusababisha ulemavu na vifo vingi.Nchini Tanzania asilimia 34 ya vifo vilivorekodiwa hospitalini mwaka 2017 vimesababishwa na magonjwa haya,Isitoshe kupambana na NCD ni miongoni mwa mikakati ya Mpango wa kimataifa wa Maendeleo Endelevu (SDG) ya kupunguza kwa theluthi moja vifo vya mapema vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ifikapo mwaka 2030”.Amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni magonjwa sugu au ya muda mrefu,ambayo hayawezi kuambukizwa kwa maana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.

Magonjwa haya yapo mengi nayo ni kama vile Kisukari,Saratani,Shinikizo la damu na mishipa ya fahamu,Magonjwa sugu ya mfumo wa hewa,Magonjwa sugu ya figo,Macho ma meno,Selimundu (siko cell) na mengineyo.

Waziri Ummy Mwalimu amelishukuru shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyo ya kuambukiza la Tanzania (TANCDA) baada ya kuandika andiko la kuitambulisha Dunia kuhusu juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza,na dunia kuona umuhimu wa juhudi hizo.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.