Serikali kuwashughulikia wazazi ambao watoto wao watakeketwa

Ni msimu wa ukeketaji kwa wasichana na Tohara kwa Wavulana ukiwa umeanza wilayani Tarime, Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imesema itawakamata na Kuwafikisha mahakamani Wazazi ambao watoto wao wakike watakeketwa.

Hayo yameelezwa hivi karibuni na Mkurugenzi msaidizi kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii  kitengo cha malezi na Familia,Grace Mwangwa alipokuwa akitoa tamko la Serikali kwenye mkutano wa kujadili namna ya kukomesha ukeketaji ulioandaliwa na shirika la Utu wa Mtoto CDF uliofanyika ukumbi wa Blue Sky mjini Tarime.

Mwangwa anasema kuwa kitendo cha kuwakamata Mangariba pekee hakiwezi kusaidia kutokomeza ukeketaji hivyo ni lazima kuwakamata wazazi kwakuwa wao ndiyo wanaowaruhusu watoto wao kukeketwa na kuwagharamia katika sherehere za ukeketaji.

“Chanzo cha watoto kukeketwa ni wazazi,ndugu ndiyo wanaishi na mtoto mangariba upewa fedha na wazazi ili kumkeketa mtoto,mimi nimeolewa Musoma lakini hakuna hata siku moja mtoto wangu atakeketwa,akina mama kataeni ukeketaji usiogope kutengwa mbona yesu alisulubiwa kwa ajili yetu sisi! akina mama tunaogopa nini kuwasimamia watoto wakike kwa mwaka huu tuwe mfano” anasema Mwangwa.

Mwangwa anaongeza kuwa mzazi ndiye mlinzi wa kwanza wa mtoto anayepaswa kusimamia haki zote za mtoto pamoja na kutekeleza sheria ya mtoto ya 2009 nakwamba kitendo cha ukeketaji ni kosa la jinai.

Mkuu wa wilaya ya Butiama Anna Rose Nyamubi akizungumza kwa niamba ya mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima, anasema kuwa baadhi ya kesi za ukatili wa watoto uchakachuliwa na baadhi ya Polisi jambo linalochangia kuendelea kwa vitendo vya ukatili.

” Kuna mtoto mmoja wa kike alibakwa kesi ikaenda polisi ikachakachuliwa kwakuwa mtuhumiwa alikuwa na pesa lakini baada ya mkuu wa mkoa kuisimamia kesi hiyo mtuhumiwa alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jera”alisema Nyamubi.

Nyamubi anasema kuwa suala la ukeketaji linafanywa makusudi kwani maeneo yote kunakofanyika ukeketaji yanajulikana na watu wanakuwa wamejipanga kwa kutoa kadi za sherehe za ukeketaji.

” Kuna wanawake wengine hawakuolewa kwasababu tu hawajakeketwa wanaishi tuu na watoto wao na wana maisha mazuri ukienda mjini ndiyo wana maduka makubwa ya biashara wana Mara tuchukue hatua dhidi ya ukeketaji” alisema.

Mkuu huyo anayaataka mashirika kuwekeza katika kutoa elimu za ujasilia mali na uanzishaji wa viwanda vidogo ili kusaidia jamii kuinuka kiuchumi.

” Mashirika yabadilike tukiangalia tatizo la ukeketaji chanzo ni kipato wazazi wanakeketa watoto ili wawaozeshe wapate mali,kuna baadhi ya watoto ukimbilia kwenye kituo cha Masanga kumbe si kwa sababu za kukeketwa bali ni kujifunza ujasilia mali wapo waliokimbia tuliwarudisha kwao walikuwa ni wa kutoka Shinyanga na Simiyu naomba mashirika yawekeze katika maswala ya ujasiliamali na yaanzishe viwanda vidogo ili kusaidia ajira na watu wapate ujuzi ” anasema.

Mkuu wa wilaya ya Rorya awalalamikia Wazee wa Mila.

Mkuu wa wilaya ya Rorya Simon Chacha anawalalamikia Wazee wa mila kwa madai kuwa wao ndiyo chanzo cha ukeketaji kuendelea licha ya kila mara kupewa elimu.

” Kila leo tumekuwa tukijadili hii mada lakini yanaishia humuhumu ndani,Mkoa wa Mara ifike wakati tubadilike tuone ni kwa namna gani tutaondokana na hii tabia,Mimi ni mkurya nawafahamu vizuri hawa wazee wa mila nitasema ukweli hawa ndiyo tatizo ni mara ngapi mashirika yamewapa semina na wakati mwingine kuwasafirisha nje ya mkoa kuwapa elimu lakini ukeketaji bado haushi!” anasema

Chacha anaongeza ” Wazee hawa wana umoja wao wa koo 12 za kabila la wakurya na niwawakilishi naomba wawe wakweli haya wanayojifunza je uwafikishia wazee wenzao wa mila huko kwenye koo zao ambako ndiko kuliko na wazee wengi na je huafikiana na kama wanaafikiana mbona ukeketaji bado unaendelea? Alihoji Chacha.

Chacha anayataka Mashirika kwenda moja kwa moja kwa wazeee wa mila kwenye koo hizo kuwapa elimu kwa madai kuwa hana hakika kama wazee hao wawakilishi wa wazee wa koo kama ufikisha wanachojifunza kwa wazee wenzao.

Anasema kuwa Sheria ikitumika vikali haitaondoa tatizo bali Elimu itolewe zaidi yenye lugha laini ili kuleta mabadiliko kwa madai kuwa imekuwa ikitumika sheria lakini ukeketaji unaendelea  hivyo ni vyema kutumia lugha rafiki katika kubadili tamaduni za watu.

Wazee wa Mila wawa mbogo wamwijia juu mkuu wa wilaya Rorya.

Baada ya mkuu wa Wilaya ya Rorya Simon Chacha kudai kuwa Wazee wa mila kuwa sehemu ya kuendeleza vitendo vya ukeketaji kwa kupewa semina mbalimbali lakini wameshindwa kukomesha ukeketaji,Mwenyekiti wa wazee wa mila koo 12 za jamii kabila la Wakurya wilayani Tarime Nchagwa Mtongori ambaye pia ni mwenyekiti koo ya Wachari anakanusha madai ya mkuu wa wilaya.

Mtongori anasema kuwa anasikitika kwa kitendo cha Serikali kutothamini mchango wa wazee wa mila licha yakuwa wao wamesaidia kupunguza vitendo vya ukeketaji ikilinganishwa na miaka iliyopita.

” Serikali ilianzisha kanda maaulum ya Polisi kutokana na kuwepo vita,mapigano ya koo wizi wa mifugo,viongozi wa Polisi  haohao walitufata sisi wazee wa mila kutuomba ushirikiano baada ya wao kushindwa kudhibiti na sisi tumewashughulikia kimila waovu,na umoja wetu unashirikiana na wazee tunachopanga tunakubaliana wote.anasema Mtongori.

Anaongeza”sisi wazee ndiyo tulisaidia mapigano ,wizi kupungua maana jamii inatuamini wazee tulikuwa tukiagiza jambo linatekelezwa mara moja,lakini leo hii Serikali ina wapongeza tu Polisi na kuwaacha Wazee wa Mila kana kwamba wao hawakuwa na mchango wowote kwenye jamii haitoshi mkuu huyu wa wilaya ambaye ni mkurya na ameshuhudia jitihada za wazee leo anasema wazee wa mila ndiyo wanachochea ukeketaji ” anasema.

Boniface  Meremo aliyekuwa Katibu wa mila koo 12 tangu kuanzishwa mkoa wa kipolisi Tarime/ Rorya Julai, 2009 anaeleza kuwa Serikali inapaswa kutambua juhudi za wazee wa mila ndani ya jamii.

” Saizi ukeketaji umepungua zamani mtu alikuwa anakeketwa kicccm wanakata chote anakaa mwezi mzima ndiyo anapona badae wazee tukakaa tukasema tupunguze makali wakatwe kidogo ,siku zimeendelea sasa wanapaka tuu unga wanaokeketwa ni kwa hiari yao. anasema.

” Tulikubaliana na Serikali kuwa hii mila kuisha kwa ghafla ni ngumu tukasema watoto wawe wanaenda jandoni wakifika huko wanawapaka tuu unga kama kudumisha tu na watu washerekee basi ,hivi mtu akeketwe leo kesho unamuona anakimbia anacheza mpira!wanaokeketwa wanataka wao wenyewe hawalazimishwi na wazee wa mila ” anasema.

Ngariba wanena.

Baadhi ya mangariba akiwamo Angelina Ong’oso kutoka Kijiji cha Kangariani Kata ya Itiryo aliyekuwa akikeketa na kisha kuachana na kazi hiyo baada ya kupata elimu ya athari za kumkeketa msichana anasema kuwa umasikini ndiyo sababu ya ukeketaji kutoisha.

“Mimi nilianza kukeketa mwaka 2012  na baada ya kupata elimu kutoka shirika la Masanga wakanifundisha ushonaji wa nguo nikaamua kuacha ukeketaji 2016 niliacha kwa hiari,gharama za ukeketaji na Tohara ni 20,000 kati ya fedha hizo 15000 ni ya ghariba na 5000 ni ya wazee wa mila na kwa siku ukeketa kati ya watu 50-100 “anasema

Bhoke Marwa anasema kuwa kuna haja ya ghariba,wazee wa mila kuwezeshwa ili wajikwamue kiuchumi lakini pia familia duni zikiwezeshwa itasaidia ukeketaji kuisha kwamba yeye baada ya kupatiwa elimu sasa ni mjasiliamali wa kutengeneza sabuni jambo lillomfanya aache ungariba.

Viongozi wa Dini  Wadau waeleza sababu za ukeketaji kuendelea na nini kifanyike kukomesha ukeketaji.

Juma Abdallah  mkazi wa Kijiji cha Borega B kata ya Mbogi anasema kuwa bado ushiriki wa maafisa ustawi wa jamii ni mdogo hasa wanapofikishiwa taarifa za vitendo vya ukatili kwa watoto hawawajibiki vilivyo kuwasaidia wahanga kisheria.

Ester Charles mkazi wa Mbogi anasema kuwa siyo watoto wote ulazimishwa na wazazi bali wao wenyewe utoroka na kwenda kukeketwa ili wapate zawadi kama pesa,vitenge na kanga lakini pia uogopa kudharauliwa na wenzao.

Piter Ojwang’ kutoka Idara ya Elimu halimashauri ya wilaya ya Tarime anasema kuwa bado wenyeviti wa vitongoji,Vijiji na Kata hawajashirikishwa vyakutosha katika kupewa elimu hivyo wakipata elimu watakuwa mstari wa mbele kuwaripoti wazazi ambao watoto wao wamekeketwa kwakuwa matukio hayo yanatokea ndani ya vitongi vyao na wanawafahamu wananchi wao.

Afisa Tarafa ya Inchugu Meshack Aligawesa yeye anasema kuwa jamii nyingi za vijijini bado hazijafikiwa na elimu hivyo ni vyema Mashirika yakaenda moja kwa moja vijijini kungea na wananchi ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara badala ya kufanya vikao mjini na washiiki walewale huku wakitumia fedha nyingi kukodi kumbi za mikutano.

Viongozi wa Dini waeleza

Makamo Mwenyekiti wa Umoja wa  Viongozi wa Dini wilayani Tarime Fransis Makori ambaye ni mchungaji wa kanisa la Menonite anaeleza kuwa dini hazikubaliani na ukeketaji nakwamba kazi ya viongozi wa dini ni kuielimisha jamii ili watu wapingane na mila potofu .

” viongozi wa dini tulianza kupinga ukeketaji hata kabla ya mashirika kuna baadhi ya waumini walitengwa na makanisa yao baada ya kuhusika kukeketwa au wazazi walioshiriki kukeketa watoto wao tunaomba waumini wawe na hofu ya mungu nawaomba wazee wa mila wasaidie kupiga ukeketaji.”anasema.

Sheikh msaidizi kutoka Baraza kuu la Waislan wilayani Tarime (Bakwata) Tawfiq Hussein  anataja sababu za ukeketaji kutoisha kuwa mila hiyo ilikuwa ilishaota mzizi katika jamii  nakwamba elimu nyingi utolewa mjini badala ya vijijini kuliko na wahanga na aliwataka wananchi kukubali kubadilika.

Polisi Serengeti wadai walivyochezewa lafu na wananchi kukeketa wakati wa mbio za mwenge.

Mkuu wa Dawati wa Polisi wilayani Serengeti Titus Mufuruki anaeleza  kuwa wilaya ya Serengeti inajitahidi kupambana na ukeketaji nakwamba 2016/2017  zimeripotiwa  kesi 20 za ukeketaji kati ya hizo 10 zilifikishwa mahakamani .

Anasema kuwa kati ya hizo kesi 5 zilihukumiwa  kifungo cha kati ya miaka 2- 10 jela na kwamba polisi wanakabiliwa na changamoto ya ushahidi wa kutoka ambapo watendewa kosa ukataa kuwataja wahusika huku wakidai kujikeketa wenyewe.

Anaongeza kuwa pamoja na juhudi za polisi bado wananchi ukeketa kwa siri ambapo wakati wa mbio za mwenge wilayani Serengeti wananchi walitumia mwanya huo na kukeketa wasichana.

“Ukipanga hivi wananchi nao wanapanga mikakati yao,siku ya mbio za mwenge  Septemba 11,2018 tukiwa bize na mwenge siku hiyohiyo watu walikeketwa tumelijua hilo baadae ambapo zaidi ya wasichana 200 wanadaiwa kukejetwa ,sisi kama polisi tunaendelea na upelelezi tumefanya msako mpaka sasa zimeripotiwa kesi 7 kati ya hizo kesi 4 ziko mahakamani zinaendelea kusikilizwa” anasema.

Wakati huo mkuu wa dawati la Polisi mkoa wa Polisi Tarime /Rorya Saumu Ngoma alisema taarifa za ukeketaji zirizoripotiwa Polisi mwaka 2016/2017 ni kesi 23, kati ya hizo 13 zilifikishwa mahakamani  ambapo  kesi 2 washtakiwa walikiri kosa na kuhukumiwa  jela.

Huku wilaya ya Butiama ikiripotiwa kesi moja ya mwanamke kukeketwa akiwa ameolewa  ambapo hata hivyo baada ya  mmalamikaji kufungua kesi aliishia mitini.

Afisa Maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya ya Tarime  Ochieng Wayoga anazungumzia mikopo nakusema kuwa  halmashauri utoa fedha za mikopo kwa ajili ya wanawake na vijana ambapo kwa mwaka 2017/2018 ilitoa zaidi ya 307 milioni kwa vikundi 118 nakwamba anawashauri wananchi kuanzisha vikundi ili viwezeshwe mikopo.

Mkurugenzi wa Shirika la Utu wa Mtoto Tanzania CDF Konshuma Mtengeti anasema lengo la mkutano ulilenga kijadili jinsi gani wanaweza kuzuia ukeketaji nakwamba matarajio  ni kuona mafanikio na aliwataka wadau mbalimbali kuungana pamoja ili kutokomeza vitendo vya ukatili ili mwaka huu  uwe ni mwaka wa mfano kwani elimu zimetolewa sana kilichobaki ni kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ukeketaji.

Kabila la Wakurya wilayani Tarime  lina koo 12 za jamii ya kabila hilo ambao kila mwaka unaogawanyika kwa mbili udumisha tohara kwa wavulana na Ukeketaji kwa wasichana ufanyika jandoni na kwa sherehe kubwa kwa kile kinachoaminiwa kuwa ni kumtoa mtoto katika hali ya utoto na kuwa mtu mzima kisha kuolewa.

Kwa mujibu wa kabila hilo huamini kuwa mtoto wa kike akikeketwa uheshimika,na kuolewa haraka kwa mali nyingi lakini pia kushiriki sherehe mbalimbali kama za jandoni,arusi na asipokeketwa udharauliwa na jamii inayomzunguka ikiwa ni pamoja na kuitwa msagane(asiyekeketwa) jambo linalochochea wasichana wengi kukeketwa.

Pia Inaelezwa kuwa mtoto wa kiume akitahiriwa jandoni ndiyo uheshimika na uonekana jasiri na hivyo kupendwa na wasichana wengi jambo ambalo umfanya kupata mchumba haraka.

Jumla ya koo 12 za jamii kabila la wakurya wilayani Tarime udumisha mla ya ukeketaji na Tohara kila mwaka unaogawanyika kwa mbili kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba. Koo hizo ni

Wasweta,Wairege,Wanyamongo,Wanyabasi,Wakira,Warechoka,Wamera,Wahunyaga,Watimbaru,Wanchari,Watobori na Wakenye.

 

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.