RWANDA:DIANA RWIGARA KUPANDISHWA KIZIMBANI LEO, ASEMA HAOGOPI VITISHO.

 

Kigali, RWANDA.

Mwanasiasa wa upinzani na mkosoaji mashuhuri wa Rais Paul Kagame wa Rwanda, mwanadada Diane Shima Rwigara, amesema katu hatasalimu amri mbele ya mashinikizo na vitisho dhidi yake.

Bi Rwigara ambaye leo Alhamis anatazamiwa kufikishwa mahakamani kusikiliza mashitaka yanayomkabili ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, hakuna aina au kiasi chochote cha mashinikizo kitamfanya afumbie macho na kunyamazia kimya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Rwanda.

Hii ni kufuatia hali ambayo, kiongozi huyo wa upinzani ambaye amekuwa akikosoa serikali ya Rais Kagame waziwazi, kuhisi kuwa huenda akahukumiwa kifungo cha miaka 22 jela iwapo atapatikana na hatia katika mashitaka yanayomkabili.

Mapema mwezi Oktoba, Rwigara pamoja na mama yake waliachiwa huru kwa dhamana na Jaji wa Mahakama Kuu ya Rwanda, lakini walitakiwa kutotoka katika mji mkuu Kigali mbali na kukabidhi pasi zao za kusafiria kwa Mwendesha Mashitaka Mkuu wa serikali.

Wawili hao wanadaiwa kukwepa kulipa kodi zinazoihusu kampuni ya tumbaku inayomilikiwa na familia yao, lakini hapo kabla bi Rwigira alituhumiwa kughushi na kufanya udanganyifu katika fomu alizojaza kwa ajili ya kugombea urais mwezi Agosti mwaka jana akitaka kuchuana na Rais Kagame.

Mwanasiasa huyo wa upinzani binti aliye na umri wa miaka 35 na ambaye ni mhasibu kitaaluma amekuwa akimtuhumu Rais Kagame, kwamba anawabinya wapinzani, na kukikosoa chama tawala cha RPF kwa kuweko madarakani tangu kiliposhika hatamu za uongozi baada ya kuhitimisha mauaji ya kimbari nchini humo mwaka 1994.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.