RAIS ESSEBSI ATOA SALAMU ZA MWAKA 2019 KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

Tunis, TUNISIA.

Rais wa Tunisia, Beji Caid Essebsi, amezungumzia uchaguzi ujao wa rais na bunge nchini humo na kusema kuwa mwaka 2019 utakuwa mwaka muhimu kwa nchi hiyo.

katika ujumbe wake mwaka mpya wa 2019, Rais Essebsi ameeleza kuwa jitihada kubwa zinapaswa kufanyika kuandaa mazingira bora ya kufanyika uchaguzi wa wazi, huru na wa kidemokrasia katika mwaka huu wa 2019.

Aidha, Kiongozi huyo amewataka wananchi wa nchi hiyo kutumia haki yao ya kikatiba na kushiriki kwenye chaguzi hizo, ambapo amewataka Watunisia kuwachagua watu wanaofaa kwa ajili ya kushika nyadhifa za kuiongoza nchi hiyo.

Rais Essebsi ameongeza kuwa mwaka 2018 ulikuwa mwaka mgumu kwa nchi hiyo kutokana na maandamano ya wananchi, ghasia, mashinikizo ya kiuchumi, kuongezeka idadi ya watu wasio na ajira na kupungua sana uwezo wa kifedha wa wananchi wa kununua bidhaa muhimu.

Tunisia kwa siku kadhaa sasa imekumbwa na maandamano ya wananchi dhidi ya serikali yaliyopewa jina la Vizibao Vyekundu, maandamano ambayo yalipata mwamko kutokana na yale ya nchini Ufaransa ya harakati ya Vizibao vya Njano.

Wanaharakati wa vizibao vyekundu nchini humo wanasema kuwa wataendelea kufanya maandamano wakilalamikia utendaji wa serikali na hali mbaya ya uchumi nchini humo kuitaka serikali itekeleze baadhi ya marekebisho ili kuboresha hali ya maisha ya wananchi.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.