RAIS AL BASHIR KUGOMBEA TENA, KUFUATIA BUNGE LA SUDAN KUUNGA MKONO MAREKEBISHO YA SHERIA ZA UCHAGUZI.

 

Kartoum, SUDAN.

Kiongozi wa muda mrefu wa Sudan, Omar Hassan al Bashir anakaribia kupata idhini ya kugombea tena kiti cha Urais wa nchi hiyo, baada ya wawakilishi wa Bunge la nchi hiyo kuunga mkono pendekezo la kufanyika marekebisho ya sheria za uchaguzi.

Marekebisho hayo yatakayoondoa ukomo wa muda wa urais, hivyo yatamuwezesha Rais Omar al Bashiri kugombea kiti cha rais wa Sudan baada ya kumalizika muda wake wa sasa mwaka 2020.

Kwa mujibu wa katiba ya sasa ya Sudan, Al Bashir, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1989 haruhusiwi kugombea tena kiti hicho baada ya kumalizika muhula wake wa vipindi viwili ulioainishwa mwaka 2005 baada ya marekebisho ya sheria za uchaguzi.

Spika wa Bunge la Sudan, Mhe Ibrahim Ahmed Omar, amesema amepokea barua iliyosainiwa na idadi kubwa ya wabunge wanaounga mkono marekebisho ya katiba yatakayomruhusu al Bashir kugombea tena kiti hicho.

Mapema mwaka huu chama tawala nchini Sudan cha Kongresi ya Taifa kilitangaza kuwa, kimemteua al Bashir kugombea kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Vyama vikuu vya upinzani nchini Sudan vimepinga hatua hiyo, ambapo katika kipindi kilichopita vilisusia chaguzi za Rais na Bunge zilizofanyika mwaka 2015.

Rais Omar Hassan anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita katika jimbo la Darfur.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.