NHIF YAJIVUNIA UPATIKANAJI WA HUDUMA BORA NCHINI

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umejivunia kuongeza wigo wa wanufaika kwa kuwafikia Wananchi mbalimbali ikiwemo Wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika kwenye huduma ya Ushirika Afya na watoto kupitia huduma ya Toto Afya Kadi.

Mfuko pia umewezesha upatikanaji wa huduma za Madaktari Bingwa katika mikoa ya pembezoni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa katika Hospitali hapa nchini.

Hayo yameelezwa na Meneja uhusiano wa mfuko huo Bi. Anjela Mziray wakati wa ziara maalum ya Maafisa Habari wa Wizara ya Afya na taasisi zake katika kampeni maalum ya ‘Tumeboresha sekta ya afya’ inayolenga kueleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.

Wakiwa makao makuu ya NHIF, maafisa hao waliweza kutembelea maeneo mbalimbali ya mfuko huo kujionea namna huduma zinazotolewa na mfuko huo sambamba na mafaniko waliyofikia katika sekta ya Afya.

Bi. Anjela Mziray aliwaeleza maafisa hao kuwa Serikali inakusudia kuwafikia wananchi wote na huduma bora za afya. Katika kutekeleza hili Mfuko umewezesha madaktari bingwa wa magonjwa ya mbalimbali kama ya wanawake, watoto, moyo, macho, kinywa na pua na mabingwa wa upasuaji kutoa huduma katika mikoa ya pembezoni kwa kipindi maalum.

“Kwa ujumla watu zaidi ya 20,289 wamefikiwa na huduma hii na kati ya hao watu 938 wamefanyiwa upasuaji wa kitalaam na hii ni katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa, Lindi, Mara, Manyara, Geita, Njombe na Ruvuma huku baadhi ya mikoa tukienda mara mbili” alieleza Bi. Anjela Mziray.

Aidha,katika mafanikio mengine ya kuboresha upatikanaji wa huduma,mfuko unashiriki juhudi za Serikali za uwekezaji katika viwanda. Mfuko kwa kushirikiana na baadhi ya taasisi zingine unawekeza katika kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa za hospitali zitokanazo na malighafi ya pamba na kiwanda hiko kitajengwa Bariadi Mkoani Simiyu huku kikitarajiwa kuzalisha aina 24 za bidhaa hizo.

Wadau wengine wanaoshiriki katika uwekezaji huu ni pamoja na Serikali ya mkoa wa Simiyu, WCF, TFDA, TBS, MSD, TIB, TIRDO na taasisi zingine.

Katika jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma, alieleza kuwa mfuko kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani umenawezesha wamama wajawazito kupata bima ya afya ili waweze kupata huduma katika hospitali.

Mpaka sasa wajawazito wapatao 1,044,000 wameshafikiwa na mpango huu katika mikoa ya Tanga, Mbeya, Njombe, Lindi na Mtwara.

Mfuko huo pia umeweza kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa kutumia mifumo ya Tehama inayowezesha kutambua wanachama katika vituo, kurahisisha ulipaji wa madai ya watoa huduma kwa wakati, kurahisisha usajili wa wanachama na kuharakisha utoaji wa vitambulisho.

Akizungumzia hilo Meneja wa Mifumo ya Tehama Bw. Bakari Yahaya alisema kwa sasa mifumo inamwezesha mwanachama kupata ujumbe mfupi kwenye simu yake mara tu kadi yake au ya mtegemezi wake inapotumika kwa matibabu.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.