MWILI WA MTOTO ALIYEPOTEA WIKI MBILI ZILIZOPITA WAKUTWA KATIKA PORI NJOMBE

Mwili wa mtoto wa miaka 6 anayefahamika kwa jina la Godluck Mfugale aliyepotea wiki mbili zilizopita mkoani Njombe wakutwa katika pori lililopo karibu na shule ya sekondari Njombe (NJOSS) ukiwa umeharibika.

Akizungumza wakati wa Ibada ya kuuaga mwili huo iliyofanyika katika kanisa la KKKT mtaa wa Melinze mjini Njombe,mchungaji wa KKKT jimbo la Njombe Bernad Sagaya amesema kuwa mwili wa mtoto huyo ulipatika siku ya jana ukiwa umeharibika hali ambayo imewashtua wakazi wa mji wa Njombe kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya mauaji ya watoto.

Aidha kiongozi huyo wa kanisa amewaomba waumini wa kanisa hilo pamoja na wananchi kushirikiana na kuunga mkono jitihada ambazo zinaendelea kufanywa na viongozi wa serikali katika kukabiliana na wanaohusika na vitendo hivyo.

“Niombe tusaidiane kuweka ulinzi wa kutosha maana wanaofanya matukio haya ni vijana wetu na mimi sielewi kama watakuwa ni wazee kama mimi yaani hawa watukuwa ni vijana wadogo wanaotafuta maisha kwa hiyo wanajaribu kila eneo kama wanaweza kufanikiwa”alisema Sagaya

Kwa upande wao baadhi ya wananchi akiwemo Erasto mpete waliohudhulia katika mazishi ya mtoto huyo wameonyesha kusikitishwa na kitendo cha kuuawa kwa mtoto huyo kwani imekuwa ni tofauti na desturi za wananchi wa mkoa wa Njombe.

“kwa kweli linauma na inasikitisha sana mpaka sasa tumeamua kuanza kutembea na watoto kila sehemu na katika hali ya kawaida kwa imani tulizo nazo mimi naona moja kwa haya mambo ni ya ushirikina na haijawahi kutokea hapo mwanzo katika maeneo yetu”alisema Mpete mmoja wa wananchi

Aidha mtandao huu kimefanikiwa kuzungumza na mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth msafiri ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya na kutoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanakuwa karibu na watoto ili kuimalisha swala la ulinzi wa Watoto.

“Vyombo vya usalama naomba viendelee kushirikiana na wananchi ili ulinzi wa mtoto uwe juu, na jamii ifahamu kuwa hawa watoto ni wetu sote kila mmoja aone wajibu wa kumtunza mtoto unamhusu tuwatunze,tuwalinde kila wanapohitaji msaada”alisema Ruth msafiri

Mpaka sasa zaidi ya watoto wanne mkoani Njombe wamepoteza maisha kwa kuuawa kikatili ndani ya miezi miwili huku matukio hayo yakiendelea kuongezeka hali inayofanya kuhusishwa na vitendo vya ushirikina

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.