MWANAMKE MMOJA NA MTUHUMIWA WA KUNDI LA KIGAIDI NCHINI UJERUMANI AFUNGWA MAISHA

MUNICH. Nchini Ujerumani Mahakama moja ya mjini Munich imemhukumu kifungo cha maisha, Bibi Beate Zschaepe aliyekuwa mwanachama wa kundi la kigaidi la NSU lililokuwa linalojiita Wanazi mamboleo, ambaye ni mtuhumiwa mkuu katika kesi iliyohusu vuguvugu la chini kwa chini nchini humo.

Mahakama ilitoa uamuzi huo leo hii Jumatano ambapo Bibi Zschaepe amepewa hukumu hiyo ya kifungo cha maisha. Mshtakiwa huyo amekutwa na hatia kuhusiana na maujai ya watu 10 wengi wao wakiwa ni wahamiaji wa Kituruki ambao waliuwawa kwa kupigwa risasi kati ya mwaka 2000 na 2007.

“Kesi hii ilisababisha mshtuko hapa nchini Ujerumani na kusababisha malalamiko na lawama nyingi dhidi ya mashirika ya usalama nchini humo, ambayo yalilaumiwa kwa kuwa na ubaguzi katika kutoa huduma zake.” Msemaji wa mahakama Florian Gliwitzky alisema haya baada ya mahakama kutoa uamuzi wake.

Beate Zschaepe mwenye umri wa miaka 43 hakuonyesha hisia zozote wakati Jaji aliyeongoza kesi hiyo Manfred Goetzl alipokuwa anasoma hukumu yake katika chumba cha mahakama kilichokuwa kimejaa watu waliokwenda kufuatilia kesi hiyo huko mjini Munich.

Hata hivyo, Mawakili wa Bi Zschaepe wamesema watakata rufaa dhidi ya hukumu aliyopewa mteja wao Pamoja na wanachama wengine wanne wa kundi hilo la kigaidi, Ralf Wohlleben ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kosa la kusambaza silaha zilizotumiwa kwenye mfululizo wa mauaji.

Mtuhumiwa mwingine akiwa wa tatu, Holger G, atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kuunga mkono kundi hilo la kigaidi, huku wa nne, Andre Eminger, yeye amefungwa miaka miwili na miezi sita kwa kosa hilohilo la kuunga mkono kundi la kigaidi.

Na mtuhumiwa wa tano, Carsten S ambaye alikuwa bado ni mvulana mdogo wakati wa uhalifu huo ulipofanyika, amepewa adhabu ya kuwekwa kizuizini kwa muda wa miaka mitatu kwenye jela ya watu wenye umri mdogo kwa kosa la kusaidia na kushabikia mauaji ya watu tisa.

Aidha, Watu wanaounga mkono mrengo wa mkali wa kulia walipiga makofi kwa furaha kutokana na swahiba wao huyo kupewa adhabu ndogo ambayo hawakutarajia.

Zschaepe alikamatwa mnamo mwaka 2011, muda mfupi baada ya washirika wake wawili (Uwe Mundlos na Uwe Boehnhardt), kujiua pamoja. Hao wawili waliunda kundi lililoendeleza itikadi ya watu weupe wenye chuki dhidi ya wahamiaji, hasa wa asili ya Kituruki.

Kundi la NSU limekuwa likikwepa polisi kwa karibu miaka 14 na yote haya ni kutokana makosa ya mara kwa mara yaliyofanywa na mashirika ya usalama nchini Ujerumani na pia kutokana na wafuasi wa kundi hilo waliokuwa wanawapa taarifa za mapema.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.