MKUU WA WILAYA KILOLO ASIA ABDALLAH AWATAKA WAFUGAJI KUJENGA NYUMBA BORA

Na Francis Godwin, Darmpya IRINGA.

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Bibi Asia Abdallah, amewataka wafugaji jamii ya Kimasai na wakazi wote waishio wilayani humo kuuza baadhi ya mifugo yao ili kujijengea nyumba za makazi za kisasa.

Hayo ameyasema wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wakazi wa kijiji cha Irindi kilichopo wilayani humo, alipofika kutoa pole kwa msiba wa mwanakijiji mwenzao aliyeuawa na tembo.

Bi. Abdallah Mkuu amesema mbali na kupata maziwa, nyama (kitoweo) na kadhalika katika suala zima la ufugaji, faida nyingine ni pamoja na kuwa na makazi bora na sio kuishi katika nyumba zisizolingana na mali walizonazo.

“Wengi wenu hapa mnaongoza kwa kuwa na ng’ombe nyingi zaidi ya 100 hadi 200 na kuendelea, sasa kuna faida gani kuwa na mifugo mingi huku sehemu ya kulala huna!!?” alihoji Mkuu huyo wa wilaya ya Kilolo

Aidha, kwa kuwa Serikali imeendelea kusogeza huduma muhimu za jamii kwa wananchi, wa Kilolo, kama huduma ya maji safi na umeme, Wakazi hao wametakiwa kuandaa mazingira mazuri kwa kujenga nyumba za kisasa na kuacha kuishi kwenye nyumba za makuti na vibanda vya miti ili kuzifaidi huduma hizo.

Mbali na hivyo, amewaomba wafugaji hao kuanzisha ushirikiano wa kujenga nyumba ya familia moja baada ya nyingine, hadi wote watakapokuwa na nyumba bora.

Mkuu wa wilaya ya Kilolo, Bi Asia Abdallah akitoka ndani ya nyumba ya mmoja kati ya wafugaji wa kimasai kijiji cha Irindi.
Mbunge wa Kilolo Mh. Venance Mwamoto, na askari polisi wakipita nje ya nyumba ya jamii ya wafugaji wa kijiji cha Irindi.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.