MKUU WA MKOA WA IRINGA AGOMA KUZINDUA ZAHANATI BAADA YA KUONA DALILI YA RUSHWA

Mufindi, Iringa.

Mkuu wa mkoa wa Iringa, Ally Hapi, amegoma kuzindua jengo la kliniki katika Kituo cha Afya cha Mgololo kilichopo kata ya Makungu tarafa ya Kasanga wilayani Mufindi, baada ya kuona dalili za rushwa katika ujenzi wa mradi huo.

Tukio hilo limetokea leo Septemba 09, wakati kiongozi huyo akiwa katika ziara yake kikazi ndani ya tarafa ya Kasanga mkoani hapo, ambapo amegoma kuzindua kituo hicho, baada ya kuona kua kuna dalili ya rushwa kutokana na kiasi cha fedha kilichotumika kwenye mradi kuwa tofauti na mradi wenyewe.

Baada ya kugundua kuwepo kwa viashiria vya rushwa, RC Hapi amemtaka meneja wa Wakala wa Majengo nchini (TBA) kuandaa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo na kumpelekea ofisini kwake, ili kujiridhisha na ujenzi wake, na baada ya hapo ndipo atazindua zahanati hiyo.

Kiongozi huyo anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani humo yenye kauli mbiu iitwayo ‘Iringa Mpya’ na leo alikuwa katika tarafa ya Kasanga ambapo mbali na kutembelea majengo ya kituo cha Afya cha Mgololo, pia ametembelea kiwanda cha kuzalisha karatasi cha Mufindi Paper Mills (MPM).

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.