Mbunge Ritta Kabati Mgeni rasmi mchezo kati ya Panama Girls fc na Evergeen kesho uwanja wa Samora

NA mwandishi wetu , IRINGA

MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Iringa Ritta Kabati (CCM) kesho jumatano kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa ligi kuu ya mpira wa miguu wanawake Tanzania maarufu kwa jina la Serengeti Lite Wome’s Premier League 2018/2018 kati ya wenyeji Panama Girls FC (Iringa ) na Evergreen Queens (Dar Es Salaam)

Afisa habari wa Panama Girls Fc, Francis Godwin alisema kuwa mchezo huo ambao ni wa tatu kuchezwa nyumbani utachezwa katika uwanja wa Samora majira ya saa 10 jioni na wamemualika mbunge Kabati pamoja na viongozi mbali mbali wa mkoa wa Iringa akiwemo mwenyekiti wa CCM mkoa Dkt Abel Nyamhanga na viongozi wa serikali ya mkoa wa Iringa chini ya mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi .

Alisema wamewaalika viongozi hao ili kusaidia kuhamasisha wakazi wa mkoa wa Iringa kuendelea kuisaidia timu hiyo ya wanawake ambayo imeendelea kuutangaza vizuri mkoa wa Iringa katika soka .

Alisema timu hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika soka la wanawake na kupelekea mkoa wa Iringa kung’ara katika soka ila tatizo kubwa ambalo timu imekuwa ikikumbana nalo ni ukata mkubwa kwa wachezaji kuishi kwa shida kambini na wakati wa safari za nje ya mkoa wa Iringa .

Hivyo alisema mchezo wa leo dhidi ya Evergreen Queens ni mchezo wa kuwaaga wachezaji hao kuelekea mkoani Arusha kucheza na timu ya Tanzanite mchezo utakaochezwa Januari 13 na baada ya hapo timu itaondoka Arusha kwenda mkoani Pwani kucheza na timu ya Mlandizi Queens mchezo utakaochezwa Januari 17 kisha kuondoka mkoani Pwani kwenda Kigoma kwa ajili ya mchezo wake na timu ya Kigoma Sisterz Fc Januari 19 na kurejea Iringa .

Hivyo alisema kwa sasa timu hiyo ya Panama Girls Fc imeanza mchakato wa kutafuta pesa kwa ajili ya safari ya timu kwenda mikoa ya Arusha ,Pwani na Kigoma kwa ajili ya michezo hiyo na safari hiyo inahitaji kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 15 kwa ajili ya malazi ya wachezaji pamoja na gharama ya kukodi gari kwenda na kurudi Iringa .

Godwin alisema pesa ambayo wanaitegemea kutoka shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) pesa zinazotolewa na mdhamini mkuu wa ligi hiyo ni shilingi milioni 4 pekee kwa ajili ya mwezi huu wa kwanza na sehemu ya pesa iliyopaswa kutolewa mwezi wa 12 mwaka jana wakati timu hiyo ikisafiri kwenda Mwanza kucheza na Alliance .

Hivyo alisema siku zimekaribia na hawana pesa ya kutosha hivyo viongozi wameanza kutembeza bakuri ili kupata pesa ya kuwezesha timu hiyo kusafiri kwa uhakika safari hizo .

Akielezea kuhusu mafanikio ya timu hiyo alisema kuwa timu imeendelea kufanya vizuri zaidi kwani ukiacha mchezo wake wa kwanza iliyocheza ugenini Mwanza kwa kufungwa goli 7-1 na Alliance kutokana na wachezaji kuingia uwanjani wakiwa wamechoka na safari ndefu kutoka Iringa hadi Mwanza michezo yake ya nyumbani imekuwa ikishinda kwa kishindo yote .

Kwani alisema mchezo kati ya timu yake ya Panama Girls Fc na Mapinduzi Queens (Njombe) panama ilishinda kwa goli 7-0 na mchezo uliofuata kati ya BaoBab (Dodoma ) Panama Girls Ilishinda kwa goli 5-0 hivyo na mchezo huu wa kesho dhidi ya Evergreen Queens wanategemea kupata pointi 3 .

Godwin alisema timu hiyo imepanda kwenye msimamo wa ligi na kutoka nafasi ya 9 hadi nafasi ya 5 kwa sasa na kuwa kutokana na timu kuendelea kuhitaji msaada aliomba wanaohitaji kusaidia kuweza kuisaidia timu hiyo kupitia namba 0754026 299 na kuwa mbali ya pesa wanahitaji vifaa vya michezo pia.

Aidha alisema katika mchezo wake wa leo wameweka kiingilio cha shilingi 1000 ili kuwezesha wapenzi wengi wa soka kuingia uwanjani na pesa hiyo inaweza kuchangia mahitaji ya wachezaji kambini na wakati wa safari ya kwenda Arusha .

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.