MAWAKALA WA CHADEMA JIMBO LA MONDULI WATEKWA NA WATU WASIOJULIKANA

Monduli, ARUSHA.

Zoezi la upigaji kura katika Uchaguzi mdogo wa Ubunge na Udiwani katika baadhi ya maeneo, Tanzania Bara limeanza rasmi mapema asubuhi ya leo Septemba 16, 2018, ambapo majimbo mawili ya Ukonga jijini Dar es Salaam na Monduli mkoani Arusha, yapo kwenye mchakato wa kuwachagua wabunge wao baada ya waliokuwepo kujiuzulu.

Taarifa tulizopokea mapema leo kutoka kwa mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema), mawakala saba (07) wa Chama hicho, waliokuwa wamepangwa kusimamia uchaguzi katika vituo kadhaa jimbo la Monduli, wameshindwa kusimamia uchaguzi kwa madai kuwa wametekwa na ‘watu wasiojulikana’ usiku wa kuamkia leo.

“Ndugu zangu kati vituo vyangu 09 mawakala waliopo vituoni ni 02 tu, 07 wametekwa tangu asubuhi, nilipo maliza kuzungukia vituo nikaenda Makuyuni polisi, kufika OCS kanipeleka kukagua mahabusu, hakuna mtu hata moja mahabusu, na kasema vijana wake hawajahusika,

“Muda huu wakala na ambae ni mwenyekiti wa kata ya Mswakini kanitumia sms kuwa wamepelekwa pori la Ndoroboni Monduli, wanaambiwa mkifuatwa tunawachinja. Sieelewi wananitumia hizi sms ili tukiwafuata nasi tujumuishwe huko, sielewi tunawaokoaje!!” Amesema Mh Gekul.

Aidha, mbali na taarifa hizo Darmpya.com imepokea taarifa kuwa baadhi ya mawakala katika eneo la kituo cha Pugu jimbo la Ukonga jijini Dar es Salaam, wamezuiwa kuingia katika vituo vyao vya kupigia kura, kwa madai kuwa hawana barua za utambulisho.

Kutokana na sintofahamu hiyo, Darmpya imeamua kumtafuta msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Monduli, Bw Steve Ulaya, kuthibitisha juu ya tuhuma hizo, ambapo amesema hakuna malalamiko yoyote aliyopokea mpaka sasa kuhusu mawakala kuondolewa vituoni.

“Muulize huyo mbunge ameniambia mimi kuhusu hilo tukio, kama amekuambia wewe ni kama alikuwa anapiga stori tu, na ikitokea kuna mawakala waliokuwa hawapo vituoni, hao wameshindwa kutimiza vigezo vya kusimamia uchaguzi.” Amesema Bw Ulaya.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.