MANISPAA YA UBUNGO KUJENGA OFISI ZA KISASA

Halmashauri ya manispaa ya Ubungo imesaini mkataba wa ujenzi wa ofisi za halmashauri hiyo za kisasa na wakala wa majengo nchini (TBA).

Kutoka kushoto ni meneja wa TBA Dar es salaam Edwin Godfrey (katikati) meya wa manispaa ya Ubungo Boniface Jacob na kulia ni mkurugenzi manispaa ya Ubungo Beatrice Kwai wakisaini mkataba wa ujenzi wa ofisi za kisasa za manispaa hiyo.

Ujenzi huo wa ofisi za kisasa ambao utagharimu jumla ya shilingi bilioni 6.2 utachukua muda wa mwaka mmoja hadi kukamilika kulingana na mkataba waliosaini leo kati ya manispaa ya Ubungo na TBA.

Kutoka kushoto ni meneja wa TBA Dar es salaam Edwin Godfrey (katikati) meya wa manispaa ya Ubungo Boniface Jacob na kulia ni mkurugenzi manispaa ya Ubungo Beatrice Kwai mkataba wakikabidhiana wa ujenzi wa jengo la ofisi la manispaa hiyo.

Akizungumza baada ya makubaliano hayo Meya wa manispaa hiyo Boniface Jacobo amesema kuwa ofisi wanazotumia kwa sasa ni za kukodi hivyo wamekuwa wakitumia takribani shilingi milioni 192 kwa ajili ya kodi ndani ya mwaka mzima hivyo kukamilika kwa jengo lao jipya kutasaidia kupunguza gharama ndani ya manispaa hiyo.

Meya wa manispaa ya Ubungo Boniface Jacob akizungumza juu ya ujenzi wa ofisi hizo za kisasa za manispaa hiyo.

“Kwa miaka miwili tumeshatumia zaidi ya sh. milioni 400 kwa ajili ya kulipia kodi kwani kila mwaka tunalipa takribani shilingi milioni 192, hivyo tukikamilisha ujenzi tutaokoa fedha nyingi ambazo zitakwenda kutumika kwenye miradi mingine” amesema Jacob.

Aidha meya huyo ametoa ufafanuzi kwanini wameamua kuwatumia TBA katika ujenzi huo na si watu wengine na kusema,

“Pana muongozo wa serikali kwamba sisi wote ambao hatuna halmashauri tuliambiwa tumtumie wakala mkuu wa majengo ya serikali ambao ni TBA, kwahiyo rai ya kwa TBA msiiangushe serikali huenda ningepewa nafasi ya kuchagua ninyi msingekuwepo lakini tuna imani na nyie” amefafanua Jacob.

Mkurugenzi manispaa ya Ubungo Beatrice Kwai akiongea baada ya makubaliano ya mkataba juu ya ujenzi wa jengo la ofisi za manispaa hiyo.

Pia mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Ubungo Beatrice Dominic Kwai ameishukuru serikali kwa kuwapa fedha za ujenzi na kuwataka TBA kutekeleza vipengele vyote kwenye mkataba huo.

“Ninategemea mkataba tuliosaini leo utatekelezwa kama vipengele vinavyosema kwenye mkataba, na mimi nikuhakikishie mstahiki meya nitasimamia mkataba huu na kuhakikisha taratibu zote za kimkataba zinatekelezwa na tunawaomba TBA nyie ni serikali mkitakiwa kuwa site muda huo basi muwe huko na tuhakikishe tunatekeleza kwa wakati” amesema Beatrice Kwai.

Naye meneja wa TBA mkoa wa Dar es salaam Edwin Godfrey amesema wamepokea yale yote yaliyosemwa na manispaa na wataongeza muda wa kufanya kazi ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati.

Kutoka kushoto ni meneja wa TBA Dar es salaam Edwin Godfrey akizungumza baada ya kuingia mkataba wa ujenzi wa jengo la ofisi za manispaa ya Ubungo.

“Kwenye ujenzi huu hapa tutaongeza kidogo muda wa utendaji wa kazi na hatutakuwa na wikiendi,sikukuu wala jumapili ukija tu eneo la kazi utatukuta TBA pale hiyo yote ni kutembea kwenye maneno ya mkurugenzi hivyo tunaahidi ufanisi” amesema Edwin Godfrey.

Utilianaji saini mkataba huo wa ujenzi wa jengo la kisasa la manispaa ya Ubungo umehudhuriwa na wakuu mbalimbali wa idara, madiwani na wageni waalikwa.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.