MAKAMU WA RAIS, MHE.SAMIA SULUHU HASSAN AZINDUA JENGO LA BILIONI 1.8 CHUO CHA MISITU ARUSHA.

 

Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameupongeza Ubalozi wa Ufalme wa Norway nchini kwa kutoa ufadhili katika Taasisi za elimu ya uhifadhi wa misitu na mazingira ili ziweze kutoa elimu bora.

Ametoa pongezi hizo leo katika chuo cha Misitu, Olmotonyi jijini Arusha wakati akizindua jengo la mihadhara lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 240 na Bweni la wanafunzi wa kike lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 100 ambayo yamegharimu jumla ya shilingi za kitanzania Bilioni moja mia nane milioni mia saba na nne elfu mia sita(1,800,704,600/=).

Ujenzi huo umefadhiliwa na Serikali ya Kifalme ya Norway kupitia Mradi wa Kujenga uwezo wa Jamii kwa njia ya mafunzo katika Usimamizi Shirikishi wa Misitu, MKUHUMI na Mabadiliko ya Tabianchi maarufu kama ECOPRC.

Amesema majengo hayo yatasaidia kupunguza uhaba wa madarasa pamoja na adha kwa wanafunzi wa kike ambao wamekuwa wakiishi nje ya chuo hicho.

Katika hatua nyingine, Mhe, Samia ameushukuru Ubalozi huo kwa kutoa ufadhili wa masomo katika ngazi ya Astashahada na Stashahada katika chuo hicho kwa wanafunzi 128, kati ya hao 56 wakiwa ni wanawake.

Mbali na hilo, Mhe Samia ameushukuru Ubalozi huo kwa kukiwezesha chuo hicho kuunganishwa na Mkongo wa Taifa, kuboresha maktaba pamoja na kukiwezesha kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya kufundishia.

Kufuatia ufadhili huo, Mhe.Samia amesema uboreshaji huo utasaidia sana kuimarisha mazingira na mafunzo yatakayotolewa na chuo na hivyo kukiwezesha kuzalisha watalaam wenye ujuzi wa kiwango cha hali ya juu.

Awali, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga alieleza kuwa kutokana na uhaba wa mabweni na kumbi za mihadhara, Chuo kilikuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 600 wakati mahitaji halisi ni zaidi ya wanafunzi 1,000.

Mhe, Hasunga amesema kuwa kupitia uboreshwaji wa miundombinu hiyo kutasaidia sana katika utoaji wa mafunzo ya kiwango cha juu.

Aidha, Naibu Waziri Hasunga ameuomba Ufalme wa Norway kuendelea kushirikiana na Chuo hicho ikiwemo kuongeza mabweni ya wavulana, madarasa pamoja na kuboresha vifaa vya mafunzo ili chuo kiweze kufikia lengo lake la kuongeza udahili.

Kwa upande wake, Balozi wa Norway nchini, Elizabeth Jacobsen amesema nchi yake imefadhili mradi huo lengo lake ni kuhakikisha miti iliyopo haikatwi ovyo badala yake jamii ijikite kupanda zaidi miti ili kuepukana na mabadiliko ya tabianchi.

Chuo cha Misitu-Olmotonyi kilianzishwa mwaka 1937 kwa madhumuni ya kufundisha elimu ya uhifadhi wa misitu kwa ngazi ya ufundi-sanifu na kimekuwa tegemeo kubwa hapa Tanzania na katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.