LISU AISHUKIA SERIKALI AITAKA IWEKE WAZI KUONDOKA BALOZI EU

Na Waandishi Wetu.

Kumekuwepo na sintofahamu juu ya kuondoka nchini Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), Roeland van de Geer, jambo ambalo limeibua hisia tofauti huku zikisambaa taarifa kwenye baadhi ya mitandao ya Kijamii ikiituhumu Serikali ya Tanzania kumfukuza nchini.

Hata hivyo Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Dk.Augustine Mahiga, alikanusha kufukuzwa kwa Balozi huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha Waziri Mahiga alisema Balozi Roeland aliyeondoka Novemba 3 mwaka huu kurejea kwao hakufukuzwa bali aliitwa makao makuu ya umoja huo Brussels Ubelgiji.

“Balozi ameitwa na umoja wa nchi za Ulaya, kuitwa kwake tumeshauriana na tumejulishwa hivyo amerudi pengine kuna majukumu na kazi zingine, hajafukuzwa ameitwa na Shirika lake na huwa huwa inatokea mtu kuitwa na Serikali yake kwa majukumu mengine,” alisema Mahiga.

Waziri huyo aliongeza kuwa Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya nao kazi nzuri na kushauriana zikiwemo taarifa mbalimbali na kwamba kazi ya Balozi ni kuwakilisha nchi au Shirika lake kama kuna maswala yanahitajika.

“Hata mimi nilipokuwa Balozi niliitwa nyumbani tushauriane na kutoa taarifa na tathimini kuhusu yale niliyotumwa,” alisema Mahiga.

Aidha Balozi msaidizi, Charles Stuart, wakati akizungumza na waandishi wa habari alisema  Balozi Roeland ameitwa makao makuu  Brusssels kwa majadiliano na ngazi za juu za kisiasa kuhusu matukio ya hivi karibuni yaliyotokea.

Kuwepo kwa sintofahamu za kufukuzwa Balozi huyo, Umoja wa Ulaya umekanusha juu taarifa hizo.

Lisu  aishukia Serikali ya Tanzania

Mwanasheria ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lisu, na aliyewahi kuwa Rais wa chama cha wanasheria nchini Tanganyika Tundu Lisu akiandika kupitia mitandao ya kijamii Novemba 4 mwaka huu akiwa Tienen Begium amejadili swala la Balozi wa Umoja wa Ulaya Tanzania, Ndugu. Roeland Van Der Geer, ambae ameitwa Makao makuu ya Umoja huo Jijini Brussels Ubelgiji kwa ajili ya ushauri.

Anaanza kwa kueleza kuwa swala hilo ni muhimu  lingepatiwa mjadala wa wazi ikiwa ni pamoja na maelezo kutoka kwa Waziri wa Mambo ya nje Dk Mahiga.

Alisema kuwa inapofikia hatua ya Mwanadiplomasia kama Balozi kuitwa kwa ajili ya ushauri na Utawala uliomuagiza, kwa kawaida kuna viashiria vya kuwepo kwa uhusiano mbovu kati ya Utawala uliomtuma (Umoja wa Ulaya) na Utawala uliompokea ( Tanzania).

“Katika shughuli za kidiplomasia hii hua ni hatua ya awali kabla ya kuvunjwa kwa uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania,” alisema Lisu.

Lisu alieleza kuwa Umoja wa ulaya kama chombo kinachounganisha Mataifa 28 ambao ni washirika wa umoja huo, Mataifa mengi kati ya hayo yamekuwa na uhusiano mzuri sana na Tanzania  Kidiplomasia,kiuchumi na kisiasa tangu Uhuru nakwamba Umoja wa Ulaya umekua nguzo Muhimu ya kiuchumi kwa Tanzania kwa miongo mingi sana.

“Kwa takwimu za karibuni zinaonyesha kwamba uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni kutoka Umoja wa Ulaya kwa Tanzania umekuwa sana kutoka Euro Bilioni 1 mwaka 2009 hadi Euro Billioni 2.2 ambazo ni sawa na Trilion 5.5 za Kitanzania kwa mwaka 2013 sawa na ongezeko la 120%. Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya kwa sasa imefikia Euro Bilion 2 sawa na Trilion 5 za Kitanzania,” alisema Lisu.

Aliongeza “Tanzania pia inapokea misaada ya kifedha kutoka Umoja wa ulaya kwa miaka mingi sasa.
” Makubaliano ya kibiashara kati ya sisi na Umoja huo umetufanya kuwa tunapokea msaada wa mamilioni ya Euro ili kuisaidia bajeti ya serikali jambo ambalo limesaidia wananchi wa Tanzania katika nyanja mbalimbali hasa katika huduma za jamii na miradi ya maendeleo ikiwemo (TASAF),” alisema Lisu.

Mwanasheria huyo alisema kuwa Mnamo Machi 3 2017 Balozi aliyeitwa , Van Der Geer, alisaini makubaliano na Tanzania ambapo Umoja wa Ulaya uliamua kuipa Tanzania Euro Milion 205 sawa na Bilion 512 za Kitanzania kusaidia bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano 2016/17-2020/2021 na hii jumla ni sehemu ya Euro Million 676 sawa na Trilion 1.7 ambazo zimetolewa na Umoja wa ulaya  mwaka (2014-2020)

Alisema kuwa kuitwa kwa Balozi huyo wa Umoja wa Ulaya makao makuu ni jambo ambalo linatakiwa kuangaliwa bila kuacha uhusiano wake kwa wananchi wa Tanzania.
Ni muhimu Serikali ya Tanzania ikaelezea sababu ya kipi kimemrudisha Balozi huyu makao makuu kwa ushauri zaidi.

“Kuharibika kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya utagharimu sana na zaidi ya yote watakaoumia ni hali ya maisha ya Watanzania kuwa mbaya zaidi,” .alisema.

“Sisi wananchi wa Tanzania hatutakiwi kugeuzwa “HARAMU” ya Mataifa mengine ,Katalio la ulimwengu  “kwa  maneno ya Mandela enzi za ubaguzi huko Afrika ya Kusini kama unataka ueleza hali ambayo inaenda kutukumba kwa sasa,” alisema Lisu.

Aidha mwanasheria huyo alisema kuwa, “Kujitenga kwetu kutaleta madhara makubwa hasi kwenye uchumi wetu na hali nzima ya kimaisha.

“Kwa hali hii serikali ya John Pombe Magufuli inatakiwa kuja na maelezo ya wazi juu ya nini kimetokea katika uhusiano wetu na Umoja wa Ulaya,” alisema Lissu.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.