LEGAL SERVICE FACILITY (LSF) YAZINDUA KAMPENI MKOMBOZI KWA WANAWAKE NA MAKUNDI MBALIMBALI

Shirika lisilo la kiserikali la Legal Service Facility (LSF) linalofanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki kwa wote hasa kwa wanawake limezindua kampeni kwa jina la ‘Siyo tatizo tena’ yenye lengo la la kuongeza ufahamu kwa jamii kuhusu upatikanaji wa huduma za kisheria.

Mkurugenzi mtendaji wa Legal Service Facility  (LSF) Kees Groenendijk akizungumza na waandishi wa habari juu ya kampeni ya ‘Siyo tatizo tena’ kwenye ofisi zao.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi zao zilizopo Mikocheni B mkurugenzi mtendaji wa LSF Kees Groenendijk amesema lengo kuu la kampeni ya ‘Siyo tatizo tena’ ni kuongeza nguvu ya uelewa kwa jamii juu ya upatikanaji wa huduma za misaada ya kisheria bure kwa wasaidizi wa sheria (paralegal).

“Kampeni hii inalenga kuongeza nguvu ya uelewa kwa jamii juu ya upatikanaji wa wa huduma za bure kwa za misaada ya kisheria kutoka kwa wasaidizi wa sheria, LSF kwa dhati inalenga kuleta unafuu zaidi kwa wanawake wenye hali ngumu ambao haki zao za msingi zimekuwa zikifinywa au kukosekana, hali inayochangiwa zaidi na ukosefu wa usaidizi wa sheria” amesema Kees Groenendijk.

Ameongeza kuwa watu zaidi ya asilimia 70 hawajui masuala ya haki za binadamu wala wapi pa kupata msaada wa kisheria na kupelekea kukosa haki zao za msingi lakini kupitia kampeni hiyo ya ‘Siyo tatizo tena’ itaenda kumaliza tatizo hilo ambapo kampeni hiyo itafanyika nchi nzima Tanzania bara na Zanzibar.

Mkurugenzi wa mipango wa Legal Service Facility  (LSF) Scholastica Julu akifafanua jambo juu ya kampeni ya ‘Siyo tatizo tena’ wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi zao zilizopo Mikocheni B.

 

Kwa upande wake mkurugenzi wa mipango wa LSF Scholastica Julu amesema kampeni hiyo itadumu kwa muda wa miezi sita na watazunguka wilaya zote Tanzania bara na Zanzibar kuujulisha umma wa watanzania kwamba huduma za usaidizi wa kisheria ni bure na kuvisaidia vikundi vya wasaidizi wa kisheria ambavyo vinajikita katika kutoa bure huduma ya kisheria kote nchini.

“Kampeni hii ya ‘Siyo tatizo tena’ lengo lake ni kuifanya jamii ielewe kwamba msaada wa kisheria upo na ni bure na upo kila wilaya, hivyo jamii iendelee kuwatumia wasaidizi hawa wa sheria waliotapakaa katika wilaya na mikoa zote nchini ambao kazi yao kubwa ni kutoa huduma za usaidizi wa kisheria bure, hivyo kwetu sisi ‘Siyo tatizo tena” amesema Scholastica Julu.

Mkurugenzi mtendaji wa Legal Service Facility  (LSF) Kees Groenendijk akipeana mikono na mabalozi wa kampeni hiyo ya ‘Siyo tatizo tena’ Mwasiti Almas na Lameck Ditto baada ya kuzindua rasmi kampeni hiyo itakayodumu siku 60.

 

Kwa upande wa mabalozi wa kampeni hiyo ambao ni wasanii wa mziki wa kizazi kipya Lameck Ditto na Mwasiti wamesisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata msaada huo wa wasaidizi wa sheria ili kupata haki zao.

Balozi wa LSF kupitia kampeni ya ‘Siyo tatizo tena’ Lameck Ditto akizungumza na waandishi wa habari juu ya kampeni hiyo.

“Najivunia sana kuwa kwenye kampeni hii na ninawasihi wananchi kuwa matatizo yao wanayopitia ya kisheria sasa yanaweza kupata usaidizi ambao utayakomesha ama kuyamaliza kabisa na niwapongeze paralegal wote nchini kwa kazi wanayoifanya” Lameck Ditto.

Balozi wa LSF kupitia kampeni ya ‘Siyo tatizo tena’ Mwasiti Almas akieleza jambo kuhusu kushiriki kwake kwenye kampeni hiyo mbele ya waandishi wa habari.

Naye Mwasiti ameongeza na kusema, “Kuna watu furaha zimewatoka na huu ni wakati mzuri wa kuwa karibu na hawa wasaidizi wa sheria waliotapakaa kote nchini na kuzirudisha furaha zetu, watanzania tujitokeze kwa wingi hawa ni watu wamekuja kutusaidia” ameongeza Mwasiti.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.