KWAHERI MFALME DROGBA.

MAKALA.

Nikiwa mdogo sana mwaka 2004 ,nakumbuka nilikuwa shule ya msingi Mwalim Nyerere ,wilayani Kinondoni mkoani Dar es salaam.

Nilikuwa napenda sana mchezo wa soka hila sikujua klabu gani ni sahihi kwangu kushangilia lakini nakumbuka nyumba yetu ilikuwa na watu wengi na wengi walikuwa mashabiki wa klabu ya Liverpool na Manchester united ni mimi tu ndio nilikuwa nimesalia kuchangua timu ya kushabikia nilikuwa napenda kuchagua timu inayocheza vizuri.

Nakumbuka siku moja mzee wangu (Baba) aliniletea jezi mgongoni imeandikwa Pires na nikienda uwanjani kucheza mpira wa makaratasi wezangu walikuwa wananiita Pires walahi lile jina lilikuwa kubwa na sikuwahi kulipenda.

Siku moja nilikuwa na rafiki zangu kwenye soka la nguo za mitumba Tandale ,nakumbuka tulienda kununua nguo za mitamba kipindi hicho nilichagua jezi mmoja ya blue mgongoni ilikuwa imeandikwa Drogba namba 11 nikachukua hile nguo nikaja nayo nyumbani nikaiweka chini ya uvungu wa kitanda nikihofia mama ataiona na kuuliza nilipata wapi pesa ya kununua nguo ukwel ulibaki kichwani kwangu kama pesa nilikuwa nimeiba kwenye mkoba wake wa kazini.

Nakumbuka siku moja nikiwa napita mitaani nikapita banda ambalo wanaonyesha mpira nikasikia Mtangazaji wa mpira wa kingereza anasema Goal Goal ,sababu nilikuwa mdogo na pia kingereza sikuwa nakijua nikasikia mtangazaji anasema “what a Fantastic goal from Didier Drogba ”

Alikuwa ni Peter Drury huyu ambae mnamsikia sasa hivyi akitangaza mpira kunako ligi kuu soka nchini Uingereza , nikasogea kuchungulia nikaona mtu amevaa jezi ambayo mimi niliweka uvunguni kuogopa mama ataiona imeandikwa namba 11 na jina Drogba.

Sikuogopa tena nikaenda nyumbani nikachukua hile jezi na kuivaa bila woga nikaenda uwanjani kucheza mpira (Chandimu) watu wakaanza kuniita Drogba nilikuwa na amani na jina hilo .

Jana tarehe 22 mwezi 11 mwaka 2018 ,aliyekuwa mshambuliaji wa klabu ya Marseille ,Chelsea , Garatasray Dider Drogba ametangaza rasmi kuachana na soka la ushindani.

Kama ukipata nafasi ya kusoma moja ya mabango ndani uwanja wa Chelsea Stamford Bridge upande wa magharibu mwa uwanja huo utaona majina ya wachezaji yameandikwa Super Frank Lampard ,mbele utakuta kitu kimeandikwa Drogba Legend .

Sio rahisi kwa wazungu kutuheshimu watu wenye asili ya ngozi nyeusi tena kutokea Afrika wakiamini rangi nyeusi ni rangi dhaifu kwa watu weupe (wazungu ) lakini jina la Drogba linalala na kuamka ndani ya uwanja wa Chelsea pale jijini London.

Ukienda jijini Munich ukiwauliza nini zaidi kinawafanya wamkumbuke Drogba watakujibu Drogba ni mchawi wa kiafrika kwani zilibakia dakika 3 kwa Bayern Munich kutangazwa mabingwa wa Ulaya mwaka 2012 lakini kichwa cha Didier Drogba dakika ya 88 ndio kiliwanyima Bayern Ubingwa

Wao hawaongelei kuhusu penati ya mwisho wao wanawaza ile kona iliopigwa na Juan Mata ikaenda kichwani kwa Drogba na ubao ukasoma 1-1 na mwisho Chelsea haijaweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kutokea jijini London kushinda taji la klabu bingwa.

Tembo Drogba anaondoka kwenye soka la ushindani akiwa amefunga jumla ya mabao 164 akitoa assist 86 katika michezo 380 kwa mchezaji wa Afrika si haba.

Kwaheli Tembo mfalme wa usiku wa Munich.

Unajua kwamba Drogba ni mchezaji pekee wa kiafrika aliyefunga mabao 100 katika ligi kuu soka nchini Uingereza ?

Je unajua Drogba ameifunga klabu ya Arsenal magoli mengi kuliko michezo waliocheza?

Je unajua Drogba amekuwa muafrika wa kwanza kufunga mabao kwenye michezo 4 ya kombe la Malkia (FA).

Kwaheli Mfalme wa Abdjan …

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.