KUSUASUA KWA MIRADI YA MAJI KYERWA NAIBU WAZIRI AAGIZA MKANDARASI KUONDOLEWA

Na mwandishi wetu-Kagera.

Kufatia kusuasua kwa miradi ya maji wilayani Kyerwa na kushindwa kutoa huduma ya maji kwa wananchi wilayani humo,Naibu waziri wa maji Mhe.Jumaa Aweso amemuagiza mhandisi wa maji mkoa wa Kagera kumsimamisha kazi mkandarasi anayetekeleza miradi ya maji wilayani Kyerwa kutokana na kutokuwa na uwezo pamoja na vigezo.

Naibu waziri ametoa agizo hilo januari 12 mwaka huu akiwa ziarani katika wilaya za Karagwe na Kyerwa ambapo imeonekena miradi mingi ya maji katika wilaya hizo ni kutokana na makandarasi wanaopewa kazi ya kujenga miradi hiyo kutokuwa na uwezo.

Aweso amesikitishwa na kutokamilika kwa mradi ambao unathamani ya zaidi ya shilingi milioni 600 wa Kaisho Isingilo uliokwama kwa zaidi ya miaka 5 ukiwa utekelezaji wake ni 50% na kumuagiza mhadisi wa maji mkoa kumuondoa mkandarasi huyo haraka sana iwezekanavyo na kutafutwa mkandarasi mwingine mwenye uwezo wa kufanya kazi pamoja na uwezo wa kifedha atakayetekeleza mradi huo kwa wakati ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata maji.

“Nikuulize mhadisi wa maji mkoa, huyu mkandarasi ana uwezo ama hana? Basi kama hana nakuagiza kamuondoe haraka sana kama kuna mtu anasema lazima mkandarasi huyu abaki tutaona, tafuteni mkandarasi mwenye uwezo wa kufanya kazi lakini pia mwenye uwezo wa kifedha atekeleze mradi alete satifiketi na sisi tutamlipa” alisema Aweso.

Aidha Aweso amewataka wahandisi wa maji nchi kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao na kuwasimamia makandarasi wanaotekeleza miradi ya maji kotenchini kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kutoa huduma ya maji kwa wananchi na wala sio kuwatetea kwa namna yoyote ile maana wapo pale kwa niaba ya serikali.

Aweso amemwagiza pia mhandisi wa maji mkoa kuiandikia halmashauri ya wilaya Karagwe kukabidhi mradi wa maji wa itera  kwa halmashauri ya wilaya ya Kyerwa ili waweze kuusimamia kwa ukaribu zaidi kwakuwa wao ndio wamiliki halali wa mradi huo na kuuagiza uongozi wa wilaya ya Kyerwa kukabidhi miradi ya maji inayosusua kwa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Bukoba(BUWASA)ili wakaisimamia kwakuwa miradi yote iliyosimamiwa na mamlaka hiyo inafanya vizuri na inatoa maji kwa wananchi.

Akitoa changamoto za maji zinazoikabili wilaya ya Kyerwa, mbunge wa jimbo hilo mhe.Innocent Bilakwate amemweleza naibu waziri kuwa wilaya hiyo inachangamoto kubwa ya maji licha ya kuwa na vyanzo vingi vya maji.

Bilakwate amemuomba naibu waziri kuwasaidia wananchi wa wilaya ya Kyerwa ambao miradi mingi ya maji imesimama na mingine haizarishi maji na mingine iliyosimama kuhakikisha inatekelezwa ili kutoa maji kwa wananchi wa wilaya ya Kyerwa.

Naibu waziri akiwa wilayani Karagwe amesema kuwa wizara ya maji tayari imeshatenga fedha kwaajili ya mradi mkubwa wa maji katika mji mdogo wa kayanga wilayani karagwe ili kupunguza kero kubwa ya maji wilayani humo.

Hata hivyo naibu waziri hakulidhishwa na namna mhadisi wa maji wilayani Karagwe inavyotekeleza na kusimamia miradi ya maji suala linalowapelekea wananchi kukosa imaani na serikali yao kuhusu kuwasogesea maji karibu na kumuagiza mhandisi wa maji mkoa Kagera kuja wilayani Karagwe kukagua miradi yote ambayo haitoi maji kwa wananchi na kuifanyia kazi.

Naibu waziri wa maji Jumaa Aweso anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Kagera ikiwa na lengo la kuangalia na kukagua miradi ya maji katika mkoa huo.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.