KUFUATIA WITO WA MEMBE NA KATIBU MKUU CCM, PIUS MSEKWA AMKOSOA DKT BASHIRU.

 

Baada ya Mvutano na majibizano kati ya Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dakta Bashiru Ally na Mwanachama wa CCM Bernard Membe, hatimaye aliyekuwa Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa, ameibuka na Kuzungumzia sakata hilo.

“Dkt Bashiru Ally, hivi majuzi alimwambia Membe, kuwa kumpa sharti la kukutana naye si utaratibu wa chama hicho, lakini mtendaji huyo mkuu wa CCM naye ameelekezwa utaratibu unaotakiwa.” hayo yanatoka kwa Msekwa, ambaye pia ameshangazwa na kitendo cha kutumia jukwaa kuita wanachama ofisini.

Msekwa alisema hayo wakati alipoulizwa na Mwananchi Media, kuhusu malumbano baina ya Dkt Bashiru na mtu anayeitwa Bernard Membe ambaye alijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kujibu tuhuma kwamba anataka kumkwamisha Rais John Magufuli kurudi Ikulu mwaka 2020.

Ijapo Waziri mstaafu (Membe) huyo hajajitokeza kuthibitisha kama akaunti iliyomjibu Dk Bashiru ni yake, lakini mwishoni mwa wiki iliyopita, Dk Bashiru aliwaambia wanachama wa CCM kuwa wanahitaji umoja hata kama baadhi walishindwa katika uchaguzi.

Alisema hata waliotaka kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho wameonyesha mshikamano na ameshazungumza nao isipokuwa Membe tu, na akamtaka afike ofisini kwake kujibu tuhuma kuwa anataka kumhujumu Rais Magufuli.

Hata hivyo, akaunti hiyo ilimjibu Dk Bashiru kuwa Membe yuko tayari kukutana naye, lakini ikataka na mtu anayetoa tuhuma hizo awepo siku hiyo ili athibitishe tuhuma zake, kitu ambacho katibu huyo wa CCM alisema si utaratibu wa chama kuweka sharti.

Aidha, Vuguvugu hilo limemuibua Mzee Msekwa, ambaye aliliambia Mwananchi kuwa njia aliyotumia Dk Bashiru iko nje ya utaratibu wa CCM pale kinapohitaji kushughulikia tuhuma dhidi ya mwanachama wake.

Msekwa alisema alichotakiwa kukifanya, ni ama kumpigia simu Membe au kumwandikia barua ambayo ingemtaka afike ofisini kwake, badala ya kutumia jukwaa la mkutano wa hadhara.

“Hii approach (njia) sijaipenda, mimi nimewahi kuwa katibu mkuu mtendaji wa chama, sikufanya hivyo na hata kama ningekuwa sasa, kama nahitaji kuonana na kiongozi au mwanachama fulani nilikuwa ninamuita moja kwa moja kwa simu ofisini kwangu.

“Kutangaza hadharani haina maana yoyote. Kuna taratibu za kazi, sasa kukiuka siyo jambo jema hata kidogo, hilo sikulipenda.” alisema Msekwa, ambaye pia aliwahi kuwa spika wa Bunge la Jamhuri kwa vipindi viwili.

Mzee Msekwa aliongeza kwa kusema kuwa kama Bw Membe angekuwepo katika mkutano huo, angeweza kumuagiza waonane baadaye.

“Lakini wewe uko mkoa mwingine yeye yuko mkoa mwingine, halafu wewe unaagiza tu aje, je asiposikia tangazo lako? Unajuaje alikuwa anasikiliza wakati huo? Je, asipokuja utamlaumu? Kuna utaratibu wa kazi, anapigiwa simu ama anaandikiwa barua.” alisema Mzee Msekwa.

Bernad Kamilius Membe alikuwa mmojawapi kati ya wanachama 38 wa CCM waliochukua fomu kutaka kugombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka 2015, lakini aliishia tano bora alipoenguliwa na Halmashauri Kuu.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu amekuwa hajishughulishi na siasa zaidi ya kuonekana katika shughuli za kijamii.

Swali linakuja kuwa Bw Membe anamkwamishaje Rais Magufuli?

Kwa utaratibu wa CCM, huwa ina utamaduni wa kumuachia mwanachama aliyeshinda uchaguzi wa Rais apitishwe kugombea urais bila ya ushindani ndani ya chama na kauli ya Dk Bashiru inaonekana kutaka kuendeleza utamaduni huo.

Hata hivyo, Mwananchi ilipomuuliza katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (siasa, uhusiano na kimataifa), Kanali Ngemela Lubinga kama kauli hiyo ya Dk Bashiru inaweza kujenga hofu wanachama na kujizuia kuchukua fomu za urais mwaka 2020, alijibu haitawazuia kwa kuwa katiba ya chama hicho ya 2012 na mabadiliko ya 2017 yameweka wazi suala hilo.

“Wanachama wanaruhusu kugombea, lakini si utamaduni (wetu) mpaka miaka kumi iishe. Lakini hakuna kizuizi, Katiba inasema kila miaka mitano tutafanya uchaguzi. Tafuta katiba ya 2017 hata ile ya 2012, inaeleza yote.” alisema Lubinga.

Kanali huyo mstaafu alisema hakuna mwiko wa kugombea nafasi hiyo kubwa ya kisiasa kushindana na rais aliyeko madarakani, bali akasema cha muhimu ni kuzingatia muda wa kutangaza hiyo nia.

“Kwani kugombea ni mwiko? Usisahau 2015 kulikuwa na zaidi ya wagombea 40. Kugombea si tatizo, kutangaza nia mapema ni kosa. Kuna wakati wa kutangaza nia, siyo muda wowote.

“(Kitendo cha kutangaza nia) Kitamkwamishaje (Magufuli)? Haimkwamishi chochote, isipokuwa tumeweka utaratibu kwamba kuna wakati wa kampeni. Mimi ndiyo niliandika utaratibu huo kwamba ni kosa kwa mujibu wa kanuni zetu.” alisema Kanali Lubinga.

“Kuhusu Dkt Bashiru na Membe
Mwaka 2014, Membe alikuwa mmoja wa wanachama sita wa CCM waliofungiwa kwa miezi 12 kujihusisha na siasa kwa madai ya kuanza kampeni za urais mapema. Wengine ni Edward Lowassa na Frederick Sumaye, ambao baadaye walihamia Chadema, William Ngeleja, January Makamba na Stephen Wasira.

“Na Dk Bashiru anakariri taarifa zinazomtuhumu Membe kuwa anafanya vikao ya kutafuta urais kabla ya muda na ndio maana anataka aende ofisini kwake kujibu tuhuma.

“Iweje watu waseme kwamba wewe (Membe) unafanya vikao vya kutafuta kura za 2020..kwamba unataka kumkomesha Rais Magufuli, halafu unakaa kimya tu? Sasa mimi nakualika uje ofisini kama ni mwanachama wa kweli aliyetoa ahadi ya uanachama wa CCM.”

Hata hivyo, Chama hicho (CCM) tawala nchini kilitoa msimamo wake kuhusu hatua hiyo ya Dkt Bashiru kwa Membe.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, alisema kauli ya Bashiru kumtaka Membe kufika ofisini kwake ni ya kawaida ndani ya CCM.

“Ni utaratibu wa kawaida wa katibu mkuu kukutana na viongozi na wanachama wa CCM kuimarisha umoja na mshikamano. CCM inapenda kuwafahamisha kuwa imefuatilia kwa ukaribu mjadala unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu wito alioutoa Bashiru kwa Membe.

“Utaratibu wa kawaida wa Katibu Mkuu kukutana na viongozi na wanachama wa CCM katika kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa wanachama.” inaeleza taarifa hiyo.

Chama hicho kimetoa rai kwa Watanzania kuwa wito huo ulikuwa ni wa kawaida hivyo uzushi, uchonganishi, fitina na uvumi mwingine wowote unaoendelea katika mitandao ya kijamii una hila mbaya kwa CCM.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.