KONDOMU ZAADIMIKA MJI WA MAKAMBAKO,MADIWANI WAMPA SIKU SABA MKURUGENZI KUSHUGHULIKIA

Na.Amiri kilagalila

Baraza la madiwani la Halmashauri ya Mji wa Makambako Mkoani Njombe limetaarifu kuadimika kwa Kondomu kote madukani halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe hivyo kuwaagiza wataalamu wake kutafuta mwarobaini kwani ni kikwazo katika jitihada za kukabiliana na maradhi ya Ukimwi.

Wajumbe wa Baraza hilo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo hanana mfikwa walisema licha ya kuadimika hata zile zinazopatikana zimekuwa zikiuzwa hadi Tsh 800 kwa pakiti kiwango ambacho wanakitaja kutokuwa rafiki kwao.

Madiwani wa kata mbalimbali katika Halmashauri ya Mji wa makambako wamekutana katika kikao cha baraza la madiwani kujadili masuala ya maendeleo,lakini Baada ya kamati ya kudhibiti ukimwi kuwasilisha taarifa zake madiwani walisimama na kuhoji juu ya upungufu wa kinga katika halmashauri hiyo

Mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Makambako Ernest Kiungu alisema kwa muda sasa wahisani ndio wamekuwa wakisambaza mipira hiyo ya kiume lakini kwa sasa Bohari ya dawa ya Mjini Iringa haijatoa kinga hizo.

Aidha Baraza la madiwani limempa muda wa siku saba mkurugenzi wa halmashauri hiyo Paul Malala kuhakikisha kinga zinapatikana katika maeneo yote yanayopaswa kuwapo ili kunusuru afya za wananchi.

Inaelezwa Kinga zimeadimika katika nyumba za kulala wageni ,zahanati , vituo vya afya na katika maeneo mengine hali ambayo inakuwa changamoto katika kukabiliana na maambukizi ya ukimwi katika mkoa wa Njombe ambao ni kinara nchini kwa maambukizi kwa asilimia 11.8.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.