KIONGOZI WA IKHWANUL MUSLIMIN, AHUKUMIWA KIFUNGO KINGINE CHA PILI CHA MAISHA JELA

Cairo, MISRI.

Katika mwendelezo wa utoaji hukumu za adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa kiongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin, Mahakama ya Misri imemhukumu Muhammad Badie na washtakiwa wengine watano kifungo cha maisha jela katika kesi nyingine iliyokuwa ikiwakabili.

Hukumu hiyo imetolewa jana Desemba 05, 2018 na Mahakama ya Jinai ya mjini Cairo, kufuatia kesi ya mwaka 2013 inayojulikana kama “Matukio ya Ofisi ya Miongozo”, iliyokuwa inawahusisha Dr. Badie na wanachama wengine wa Ikhwanul Muslimin, ambapo wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha jela wote kwa pamoja.

Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka wa Serikali ya Misri, Badie na wanachama wengine kadhaa wa Ikhwanul Muslimin walitoa msaada kwa kundi moja la watu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha na mada za miripuko na kupanga shambulio na hujuma iliyotekelezwa na kundi hilo.

Hivi karibuni Mahakama moja ya mji mkuu Cairo ilimhukumu Muhammad Badie, vifungo vya maisha jela katika kesi nyingine kadhaa, na inasemekana kuwa adhabu ya kifungo cha muda wa zaidi ya karne moja imeshatolewa dhidi ya kiongozi huyo mmoja wa Ikhwanul Muslimin.

Baada ya Rais wa sasa wa Misri, Abdel Fattah el Sisi, kushika hatamu za madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2013, kumetokea ukandamizaji kwa wapinzani na hasa viongozi, wanachama na wafuasi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin katika utawala wake.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.