KERO YA USAFIRI WA MELI KUPUNGUA.

Ujio wa Meli mpya ya safari za Baharini umeleta matumaini mapya kwa wasafiri wanaofanya safari za Dar es salaam na Zanzibar

Meli hiyo mpya ya Kampuni ya Sea Star, ina uwezo wa kubeba Mizigo tani 1,400 na Abiria 1,500, imewasili Bandarini Zanzibar kwa ajili ya kuongeza huduma za usafari wa Baharini katika mwambao wa Bahari ya Afrika Mashariki

Hivi karibuni kumekua na ongezeko kubwa la wanaofanya safari za Baharini, hususani safari za Dar – ZNZ, ambapo awali ilikua unafika Bandarini kukata tiketi na kusafiri Siku hiyo hiyo.

Hivi sasa hali ni tofauti, kumekua na msongamano, baadhi ya wasafiri kukosa tiketi na kutakiwa kurudi kesho yake, ikiwa wengi wao hukata tiketi siku moja kabla ya safari.

Meli hiyo yenye sehemu kubwa ya kubeba mizigo, vyumba vya watu mashuhuri (VIP) na Abiria wa kawaida, itaanza safari za Unguja – Pemba – Tanga, Zanzibar – Dar es salaam, Zanzibar – Mtwara, na baadae kuendelea na safari za mbali kwa kuanzia visiwa vya Comoro.

Mwakilishi wa Kampuni ya Sea Star Mh. Salum Turky, akitoa maelezo ya Meli hiyo alisema, Uongozi umejidhatiti kutoa Huduma bora za usafiri wa Baharini kwa watu wote.

Amesema miongoni mwa mambo yatakayozingatiwa na Uongozi huo katika uendeshaji wa Biashara ni kufuata taratibu zote zilizoainishwa na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Nchini.

Mh. Salum Turky ameeleza kuwa Abiria wa kawaida atalipa Tsh 25,000/= ambapo watoto watalipiwa nusu nauli na wenye umri kuanzia siku moja hadi miaka sita watachukuliwa bure.

Safari za Zanzibar – Dar es salaam zitachukua muda wa saa 3, na zile za Zanzibar – Pemba zitachukua wastani wa saa 4.30.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akiwa na baadhi ya viongozi na watendaji wa Mamlaka zinazosimamia Usafiri wa Baharini alipata nafasi kuikagua meli hiyo iliyopo Bandarini na kuridhishwa na ubora wake.

Katika kuimarisha usafiri wa Baharini, Mh. Salum Turky aliiomba Serikali iwapatie sehemu maalum na ya kudumu kwa ajili ya kuuzia tiketi.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.