KANUNI MPYA ZA MATUMIZI YA GESI KUONGEZA GHARAMA KWA WATUMIAJI.

Kanuni mpya za matumizi ya huduma za gesi za majumbani zinazotarajiwa kuanza kutumika hivi karibuni zimepigiwa kelele na wadau wa maswala ya gesi kwa kile ambacho kinaonekana ni kuwatwisha mzigo watumiaji wa mwisho wa nishati hii muhimu sana katika maisha ya kila siku ya mwananchi.

Hayo yamesemwa leo katika mkutano wa wadau ulioitishwa na mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati nchini EWURA ukihusisha wadau mbalimbali wa sekta ya gesi wakiwemo wamiliki wa makampuni yanayohusika na uuzaji na usambazaji wa gesi hapa nchini pamoja na watumiaji wa kawaida wa gesi nchini.

Mkutano huo uliofanyika leo katika ukumbi wa ofisi za mamlaka ya udhibiti wa huduma za gesi nchini zilizopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Awali akifungua mkutano huo Kaimu Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya udhibiti wa nishati nchini Bw. Nzinyangwa Mchani amesema sekta ya gesi inakuwa kwa kasi kubwa hivyo mamlaka hiyo inao wajibu wa kuhakikisha kuwa inaweka mazingira rafiki kwa wafanyabishara wa sekta hiyo kuweza kufanya biashara katika mazingira salama.

Bw. Mchani ameeleza kuwa wao kama serikali wanao wajibu wa kuwalinda watumiaji wa nishati hiyo ambao ni wananchi ili kuepuka matatizo ama changamoto zinazojitokeza.

Akichangia katika mkutano huo, ndugu, Khamis mbaye ni mkurugenzi wa kampuni ya kitanzania ya MIHAN gasi ameishukuru EWURA kwa kitendo chake cha kuona umuhimu katika kuwashirikisha wadau wa maswala ya gesi katika maandalizi ya kanuni hizo huku akisisitiza kuwa sekta ya gesi hapa nchini inakabiliwa na changamoto kadha wa kadhaa ambazo zinawafanya wao kama wafanyabiashara wa gesi kuweza kufanya kazi katika mazingira ambayo si rafiki.

Ndugu Khamis aliongeza kwakuiomba serikali kupitia EWURA kuweza kuwa makini katika mapitio ya sheria mpya ambazo zinatarajiwa kupitishwa hivi karibuni kwa ajili ya kuhakikisha kuwa haziwaumizi wafanyabiashara hasa wa ndani ya nchi kwani uwezo wao wa kushindana na makampuni makubwa umekuwa ni mdogo.

Aidha Mkurugenzi huyo wa kampuni ya MIHAN akiiwakilisha kampuni yao aliomba kuwepo na utaratibu wa kuruhusiwa kuingiza bidhaa mpya ya gesi iitwayo Propane.

”Ndugu Mkurugenzi, katika mapendekezo haya ya sheria mpya kuna swala la msingi naomba kulizungumzia, kwa kipindi kirefu sasa nchi yetu imekuwa ikiagiza product moja tu ya gesi ambayo ni Butane, sisi kama MIHAN tumepokea kwa mikono miwili mapendekezo ya tume ya wataalamu wa chuo kikuu cha Dar es Salaam ambao walipewa kazi ya kufanya utafiti wa product mpya iitwayo propane na mapendekezo yao yote yalithibitisha. pasi na shaka kwamba makampuni yote yanao uwezo wa vifaa vya kuhifadhi product mpya ya Propane bila tatizo ukiondoa ORXY.”

“Kwa maelezo haya ya watumiaji wa mwisho wa gesi inaonekana kabisa hii product ya Butane ina matatizo na suluhisho ili kupunguza malalamiko haya ni kuingiza product mpya ya propane na sisi kama MIHAN GAS tayari tumejenga miundombinu ambayo ni wezeshi na rafiki kwa ajili ya kuagiza product mpya hiyo ya Propane ambayo kimsingi hata bei yake sokoni ni ndogo hivyo kupelekea kupunguza gharama kwa walaji wa mwisho” alifafanua Khamis.

Kwa upande wa wafanyabiashara wadogo wa gesi wameitahadharisha serikali kuwa makini katika kupitisha sheria mpya kwani kitendo cha serikali kufikiria kupanga bei ya nishati hiyo kinaweza kufanya nishati hiyo ikawa adimu katika maeneo ya pembezoni mwa nchi kutokana na gharama za usafiri.

”Hivi sasa bei ya gesi karibu kila mahali ni sawa kwa sababu makampuni ya uuzaji gesi yanafidia bei za mijini na vijijini, hivyo hofu yetu sisi watumiaji wa mwisho wa gesi ni pale ambapo serikali kupitia EWURA itakapoanza kupanga bei kitu ambacho kinaweza kupelekea watu ambao wako maeneo ya vijijini kununua bidhaa hiyo kwa gharama ya juu sana” amesema mmoja wa wauzaji rejareja wa gesi kutoka Tegeta aliyejitambulisha kwa jina la John.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.