KAMPUNI YA KICHINA YALALAMIKIWA KUWANYANYASA NA KUTOWALIPA WATUMISHI STAHIKI ZAO

Wafanyakazi wa kampuni ya Beijing New Building Material (BNBM) inayotengeneza vifaa vya ujenzi, wameilalamikia kampuni hiyo kwa kushindwa kuwalipa stahiki zao pale wanapoachishwa kazi.

Wakizungumza na Darmpya wafanyakazi hao walisema kuwa kampuni hiyo imekuwa na tabia ya kuwaachisha kazi wafanyakazi wake bila kuwapa malipo yao wanayostahili hasa wale wanaoonekana kutetea haki zao.

Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi katika kampuni hiyo Ramadhani Shukuru amesema “Wafanyakazi wengi wamefukuzwa kazi na wana mikataba lakini stahiki zao hawakuzipata, malalamiko haya tumeshayapeleka hadi ngazi ya wilaya wakasema watafuatilia lakini mpaka muda huu hatujawaona”.

Ameongeza kwa kusema kuwa ndani ya kampuni hiyo kuna manyanyaso yanayoendelea kama kutukanwa na hata kupigwa bila hatua yoyote kuchukuliwa jambo ambalo linawakera wafanyakazi hao.

Emmanuel Yakom ni miongoni mwa waliopitia kadhia hiyo amesema kuwa amefanya kazi ya ulinzi ndani ya kampuni hiyo kwa muda wa miezi miwili tangu mwezi Novemba mwaka jana hadi Januari 2 mwaka huu na amesimamishwa kazi bila malipo ya miezi yote hiyo kwa madai kuwa yeye ni kiziwi.

“Mimi tarehe 1 mwezi huu sikuhudhuria kazini nilikuwa naumwa nilipokuja kesho yake nikakuta wameshaweka watu wengine na nilipouliza nilijibiwa kuwa nimeachishwa kazi, nikawaambia basi wanilipe hela yangu lakini mpaka sasa hawataki kunilipa na wananizungusha tu” amesema

Hata hivyo juhudi za kuwapata viongozi wa kampuni hiyo ziligonga mwamba baada ya kuzuiliwa getini na afisa rasilimali watu wa kampuni hiyo Israel Martin akidai ndani ya kampuni hiyo hakuna mtu anayeweza kuzungumzia sakata hilo mpaka kwa afisa uhusiano wa kampuni ambaye yupo kwenye ofisi za makao makuu ya kampuni hiyo zilizopo jijijni Dar es salaam.

Aidha waandishi wa habari walifika hadi ofisi za mkuu wa mkoa Pwani idara ya kazi na kuzungumza na kaimu afisa kazi mfawidhi mkoa Richard Muhenga kutaka kujua malalamiko hayo yamewahi kuwafikia katika ofisi zao na kusema ndiyo kwanza wamepata taarifa na ijumaa watafuatilia kwenye kampuni hiyo.

“Kama ofisi mkoa hatujapata malalamiko yoyote kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo lakini kwa kuwa mmetupa taarifa hizo siku ya ijumaa tutaenda hapo kukagua kampuni hiyo na kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi hao” alisema Richard Muhenga.

Mtandao wa Darmpya unaendelea kufuatilia kwa kina na kutoa taarifa baada ya maafisa idara ya kazi kwenda kukagua kampuni hiyo siku ya ijumaa.

Related posts

Leave a Comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.